1985 - 2007

 

12. Agizo Kuu

Support Pages   Index To All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Mdo 1:1-26 na Mdo 2:1-4

Mstari Wa Kukariri
 
‘…Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.’ (Mdo 1:11). 

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Ni kwa njia gani tunaweza kumfuata Yesu kwa kupitapita tukifanya mema, tukihubiri na kufundisha? Je, unaweza kutaja njia ngapi? Orodhesha vitu utakavyofanya baada ya hapo.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Kusanyikeni na kuombeana kila mtu na mwenzake ili mpate kubatizwa kwa Roho Mtakatifu (au kujazwa tena na Roho Mtakatifu) kama ilivyotukia mara kwa mara kwa kanisa la kwanza katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Paulo anasema katika Efe 5:18, ‘…bali mjazwe Roho’. Hapa inamaanisha kwamba mwendelee kujazwa na Roho Mtakatifu.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika ukurasa mmoja au mbili za maelezo ukiainisha Yerusalemu yako, Yudea yako, Samaria yako, na miisho ya nchi kwako ni wapi.

Tafakari Neno Kwa Neno
Mdo 1:8

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Iran

Idadi ya watu: 65,000,000; Yapo makabila 65;
Waislamu ni 99%; Kanisa linakua katika mateso.

 


Hakikisha umewafundisha wengine somo hili.
Kila mara omba na kujiandaa ukiongezea mistari mingine ya Biblia
na mifano yako mwenyewe ili kufanya somo lieleweke vizuri zaidi.

 

Katika Kitabu cha Matendo ya Mitume  mlango wa kwanza tunagundua maagizo sita yenye nguvu na ambayo yanatuwezesha kumtumikia Mungu, na kuwahudumia vema watu wa ulimwengu huu.

1. Tenda Mema

Matendo 1:1 yatuambia kwamba Yesu alianza kufanya mambo fulani na kufundisha. Kazi hiyo bado hajaimaliza kwa sababu leo hii, akiwa kichwa, anafanya kazi kupitia mwili wake, yaani kanisa. Sisi tu mikono yake, miguu yake, macho yake, na midimo yake.

Baadhi ya madhehebu wanapenda kuwa midomo tu, lakini katika Mdo 10:38 tunaona kwamba Yesu alipakwa mafuta kutenda mema. Yeye alituonesha upendo mkuu wa Mungu kwa wanadamu kwa yale aliyoyatenda; na kisha alituelezea Mungu alivyo kwa maneno ya kinywa chake.

2. Ujazwe Roho Mtakatifu

Kwanini? Kwa sababu tunaambiwa katika Mdo 1:2 kwamba Yesu mwenyewe alihudumu kwa kumtegemea Roho Mtakatifu.

Kwanini jambo hili kuwa muhimu kiasi hicho?
Yesu alipokuja duniani akiwa mtoto mchanga, aliacha uweza wake wa kimbingu mbinguni (Flp 2:7). Alipotamka neno au kufanya miujiza alifanya hivyo kama mwanadamu aliyejua kuhudumu kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Yesu anasema kwamba leo watu wanaweza kufanya kazi alizozifanya, naam na hata zilizo  kubwa kuliko hizo, kwa uweza uleule wa Roho Mtakatifu (Yn 14:12).

Je, umejazwa Roho Mtakatifu?
Yesu alijua umuhimu wa tukio hili ndio maana katika Mdo 1:5 anawaahidi wafuasi wake ubatizo wa Roho Mtakatifu; maana yake kuzamishwa ndani ya Roho Mtakatifu (Mt 3:11-17) (Mdo 2:39).

Roho Mtakatifu anakuwezesha
Katika Mdo 1:8 Yesu alisema wafuasi wake wangepokea dunamis  yaani nguvu atakapowajilia Roho Mtakatifu. Kutoka neno dunamis tunapata maneno yenye nguvu kama dynamo na dynamite. Mamlaka, hata ile iliyotoka kwa Mungu, haina nguvu bila Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu dunamis ni ule uweza wa kuonesha ile mamlaka tuliyonayo.Unaweza kukumbuka jinsi wafuasi wa Yesu walivyomkimbia usiku ule alipokamatwa. Lakini angalia jinsi mambo yalivyobadilika baada ya kujazwa Roho Mtakatifu; walipata ujasiri wa ajabu. Mtazame Petro kama mfano mzuri (Mdo 2:14-).

Ni nini madhumuni ya uweza huo?
Roho Mtakatifu huja kwa sababu moja, kushuhudia kwa uweza kwamba Yesu yu hai.

3. Uwe Shahidi

Shahidi ni nani? Iwapo magari mawili yangegongana na kisha madereva wa magari hayo kupigana; polisi watakapofika kwenye tukio watauliza, ‘Ni nani aliyeona?’  Kwa maneno mengine, ‘Ni nani aliyeshuhudia mambo hayo yakitukia?’ Polisi wanataka ushahidi. Wajibu wa shahidi ni kusema kile alichokiona na/au kusikia. Hapaswi kutoa maoni au mawazo yake; wala hapaswi kutoa hukumu. Hahusiki na lo lote tena baada ya kutoa ushahidi wake, ingawa ushahidi huo unaweza kusababisha mtu akafungwa au akaachiliwa huru. Huko ndiko kuwa shahidi kazi ambayo sisi tumewajibishwa kuifanya.

Tumeona nini?
Tumemwona Yesu akitenda kazi ndani yetu; akisamehe, akiponya na kubariki, na kwahiyo tunayo mengi ya kusema. Roho Mtakatifu anafanya kazi kupitia maneno yetu akishawishi watu kwamba yale tunayoyasema ni kweli. Wakiamini na kumpokea Yesu wanawekwa huru, la hawakuamini watabakia katika utumwa wa dhambi na Shetani. Je, twende wapi kueleza habari hizi? Kila mmoja wetu ameshagawiwa sehemu yake katika shamba la Bwana ili atumike (2 Kor 10:13).

Yerusalemu
Watu wengi lazima wasimulie habari njema hizi kwa watu wa Yerusalemu ambayo ni ule mji wa nyumbani kwao ambako wanaelewana lugha na kufahamiana mazingira yao (Lk 8:39).

Yudea na Samaria
Wengine wataitwa kwenda Yudea na Samaria ambayo ni miji au mikoa ya jirani ambako wanatofautiana kidogo kwa lugha na pengine wasikubalike mara moja kwa ajili ya tofauti ndogo ndogo.

Hata miisho ya nchi
Baadhi wameitwa kwenda nchi za mbali mahali ambako mazingira yake ni tofauti kabisa; watu wake, hali ya hewa, lugha, utamaduni, na hata vyakula ni tofauti kabisa. Lakini wanapokuwa katika nchi hizo za ugenini hawaachi kusema kwamba Yesu yu hai.

4. Tenda Kazi Haraka

Tunapaswa kutenda kazi kwa bidii hata Yesu atakaporudi tena; maana atarudi tena kama malaika walivyoahidi ( Mdo 1:11). Tunapaswa kuongeza bidii kwa sababu kurudi kwake kumekaribia; baadhi ya dalili za kurudi kwake zimeonekana. Sasa ni wakati wa kuomba na kisha kuwaleta kwa Yesu ndugu na marafiki. Atakaporudi hatakuja tena kama mtoto mchanga bali atakuja kama Bwana na Mfalme atakayetawala miaka elfu moja.  Katika utawala wake hapa duniani Yesu ataweka mambo sawa kwa kweli yake na haki yake, na hatimaye katika kukamilisha historia ya mwanadamu, ataumba mbingu mpya na nchi mpya.

5. Mfanye Yesu Kuwa Bwana Na Mfalme

Jambo hili ni muhimu kwa sababu katika Mdo 1:3 tunaambiwa kwamba Yesu alitumia siku 40 akiwafundisha wafuasi wake habari za Ufalme wa Mungu.

Ufalme maana yake anayetawala ni Mfalme; kwahiyo mahali po pote ambapo Yesu ni Bwana, utawala wa haki ya Mungu upo. Na mahali Yesu anapofanywa Mfalme maisha ya watu yanabadilika, familia zinabadilika, vijiji na kanisa pia.

6. Ombeni Bila Kukoma

Jambo la kwanza walilolifanya waamini wa kwanza, mara ya kwanza walipokuwa bila Yesu ni kurejesha mawasiliano naye kwa njia ya maombi.

Katika Mdo 1:12-15 tunaambiwa kwamba wafuasi wanawake pamoja na ndugu zake Yesu waliungana kuwa kitu kimoja, wakiomba bila kukoma. Maria, mama wa Yesu alifanya maombezi, akiongea na Mwanaye katika maombi. Kutoka katika Lk 24:49 tunajua kwamba maombi yao yalikuwa, “Njoo Roho Mtakatifu, utuwezeshe”, na kweli katika Mdo 2 walipokea jibu la nguvu.

7. Teua Viongozi Wapya

Katika Mdo 1:15-26 tunaona jinsi wafuasi wa Yesu walivyomchagua  Mtume mwingine badala ya Yuda Iskariote. Walimchagua mtu aliyejua kwamba Yesu yu hai. Haifai mahali pakakosa kiongozi; watu wanahitaji mtu wa kuwapa maelekezo ili waweze kuzitumia nguvu zao za kiroho na za kimwili kwa ajili ya Injili. Kwahiyo iwapo Mungu amekupa changamoto ya kusimama na kuwajibika katika kazi yake, sema , “Ndiyo Bwana” hata leo.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu
Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili Ya Yesu Kristo


 

Burkina Faso (2)

Jina la Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Toussian (Win, Tusia)

Toussian, Northern

19,500

Viewo (Vige, Vigu, Viemo)

Vigue (Viemo)

10,000

Yarsi (Wala, Dagaari Jula)

Yari (Dagaari-Jula, Wala)

15,000

 

 





 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index To All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk