1985 - 2007

 

13. Agizo La Mwisho
Ni nani atakayekwenda? Kama si wewe, ni nani?
Kama si sasa, ni lini?

Support Pages   Index To All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Mt 28:11-20;  Mk 16:15-20;  Lk 24:45-49; Yn 20:19-23.

Mstari Wa Kukariri
Basi Yesu akawaambia tena, ‘Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi’ (Yn 20:21).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, mmemwona Yesu akifanya nini maishani mwenu? Na kama umefanya safari ya kimishenari, je, una lo lote jema la kuwashirikisha wenzako?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Katika utulivu wa moyo wako tafakari uone jinsi ambavyo ungeitikia mwito wa Mungu kama angekuita leo kuwa Mmishenari. Je, ungepatwa na mashaka au hofu gani? Mwombe Bwana akupe uwezo wa kushinda mashaka na hofu zako.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Soma Ufu 7:9,10. Umewaona akina nani? Je, unaweza kuandika majina machache? Na unafikiri hao watu uliowaona wamefikafikaje hapo? Na Biblia inasema nini kuhusu watu hao katika mstari wa 15,16,na 17?

Tafakari Mistari Hii Neno Kwa Neno
Mwa 12:1-3

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Nicaragua. Idadi ya watu: 5,000,000; Kumekuwako na historia ya matetemeko ya ardhi na vita. Watu wengi wamemgeukia Mungu; Majeraha mengi yanahitaji uponyaji.

 


Hakikisha umewafundisha wengine somo hili.
Kila mara omba na kujiandaa ukiongezea mistari mingine ya Biblia
na mifano yako mwenyewe ili kufanya somo lieleweke vizuri zaidi.

 

Je, Agizo Kuu Ni Kwa Ajili Yako?

Agizo hili ni kwa watu wote, wake kwa waume, wa rangi zote, walio maskini, walio tajiri, vijana au wazee. Mashujaa ya Umishenari ni wale watu waliodhani kwamba wao hawafai kwa huduma hiyo kwa sababu ama ni wazee sana au ni vijana wadogo sana; au pengine kwa sababu ya kuishiwa sana; au kwa ajili ya rangi yao au jinsia yao. Lakini hebu tuwaulize watu waliomfahamu Yesu vizuri.

1. Hebu Tuanze Na Mathayo

Mathayo anasema kwamba kabla hatujaenda po pote Yesu mwenyewe hufanya kazi ya umisheni ndani yetu. Anasema katika Mt 28:11-20, kwamba kwake yeye Agizo Kuu lina maana zifuatazo ~

Kuwa Mtiifu Kwa Yote Asemayo Yesu
Yesu aliwaambia wafuasi wake waende Galilaya, huko ndiko watakakomwona, na walienda. Hilo lilikuwa ni jaribio la utiifu, na kama wasingetii wasingefika mbali. Yesu hutujaribu mara nyingi kwa siku katika mambo madogomadogo ya maisha ili tumtii
(Mt 28:10,16).

Ni Kumwona Yesu Wewe Mwenyewe
Umishenari unaanzia kwa sisi wenyewe kumwona Yesu, halafu tutakuwa na jambo la kusisimua la kuwaeleza wengine (Mt 28:17).Ni lazima upo wakati ambapo inabidi Yesu aruke kutoka kwenye theolojia na kufanyika katika maisha yetu Mwokozi kweli, Bwana kweli na Mfalme milele. Tunapokuwa tumemwona Bwana, Yesu mfufuka, akiingia katika maisha yetu, na kuona yale aliyotufanyia na yale anayoendelea kutufanyia, basi tunakuwa na jambo zuri la kuwaeleza wengine.

Ni Kumwabudu Yesu
Mstari wa 17 unasema hivi, ‘Nao walipomwona, walimsujudia;…’ Ibada ya kweli inatokana na upendo wetu kwa Mungu na jinsi tunavyomsujudia (Rum 12:1).

Ni Kuyashinda Mashaka Yako
Katika Mt 28:17 tunaambiwa kwamba baadhi waliona shaka. Yawezekana wewe huoni shaka, vema, lakini je, unaamini ahadi zake kwa ajili yako? Katika Mt 26:32 Yesu alisema, ‘…nitawatangulia kwenda Galilaya.’ Katika kuitunza ahadi aliyowapa wafuasi wake, ilibidi Yesu, kwa kupitia Msalabani, afe, ashuke kuzimu, afufuke, na hatimaye awatangulie kwenda Galilaya. Ikiwa Yesu aliyafanya hayo yote, je, tutathubutu kulitilia shaka neno lake?

Ni Kusikia Agizo La Kwenda
Watu wengi husikiliza mahubiri yenye kusisimua kutoka Mt 28:19,20 kuhusu hitaji la kuwafikia watu ambao hawajafikiwa katika miisho ya nchi, lakini je, tunasikia Mungu analosema, na kutii? Kama sio wewe, ni nani aende?

2. Sasa, Hebu Tumsikilize Marko

Marko ni mwandishi wa Petro na anasema kwake yeye Agizo Kuu lina maana zifuatazo ~

Kushughulikia Kutokuamini
Marko 16:14 ni mwanzo wa aya inayohusu Agizo Kuu na Yesu anaanza kwa kuwakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao.

Kutumia Zana Za Kiroho
Katika Mk 16:17-20 tunaona zana zenye uwezo usio wa kawaida kwa ajili ya umishenari usio wa kawaida. Mstari wa 20 unasema Bwana alikuwa akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.

3. Luka Aliguswa Sana Na Agizo Hili

Katika Lk 24:45-49 inaonekana kwamba Luka alilielewa vizuri Agizo Kuu kiasi kwamba baadaye yeye mwenyewe akawa Mmishenari ~

Inabidi Yesu Atufunulie Akili Zetu Kwenye Maandiko

Kujua kwamba Agano la Kale  na Agano Jipya yote yanakubaliana katika Kristo..

Kukubaliana Na Mpango Wake

Kama ilivyo kwenye Maandiko.

Peleka Ujumbe Wa Msamaha Kwa Mataifa Yote

Kwa Jina la Yesu, kwa njia ya toba, tukianzia nyumbani.

Tambua Muda Wa Bwana

Kuna muda wa kukaa na kuna muda wa kwenda.

Uvikwe Uweza

Kabla ya kwenda kwenye ulimwengu wa watu wasioamini na walio wabishi.

4. Na Hatimaye Tumsikie Yohana

Yohana anajulikana pia kama Mtume wa Upendo. Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyependwa sana na Yesu; na kwa mujibu wa Yn 20:19-23, Agizo Kuu kwake lina maana ifuatayo ~

Uweza Wa Bwana Mfufuka
Wakati wafuasi wake walipokuwa wamejifungia ndani, Yesu alionesha uweza wake wa kuingia ndani na kusimama katikati yao.

Gharama Kubwa Ya Kumwokoa Mwanadamu
Yesu aliwaonesha mikono yake na ubavu wake nao wakaona alama za Msalaba: mateso na mauti yake. Hii ndiyo bei ya wokovu wa mwanadamu; kwamba huyu Yesu asiyekuwa na doa, asiye na dhambi, Mwana wa Mungu, aliadhibiwa kwa dhambi isiyo yake. Aliadhibiwa kwa dhambi zetu sisi wanadamu, tulioishi maisha ya uasi mbele za Mungu. Hiyo ilikuwa ni bei ya juu kabisa ambayo ingeweza kudaiwa au kulipwa.

Kuitikia Wito Wa Mungu
Yesu alikubali kuuacha uzuri wa mbinguni na kuja kwenye ulimwengu wa dhambi, ili kuyafanya mapenzi ya Baba katika huduma ya kimishenari, akiutoa uhai wake ili wengine wapate kuishi (Ebr 10:5-7). Na sasa anasema, ‘Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo’ (Yn 13:15).

Kupokea Uweza Wa Roho Mtakatifu
Yesu aliwavuvia, na siku si nyingi baadaye, ule uvuvio wa kimungu ukawa uvumi wa upepo wenye nguvu uliowajaza watu hawa waliokuwa wakisubiri.

Kujua Kazi Yetu, Kusamehe Dhambi
Wakristo wamefungua shule na hospitali katika maeneo mbalimbali katika ulimwengu huu, na huu ni ushuhuda tosha wa jinsi Bwana anavyowahurumia wanadamu.

Hata hivyo imethibitishwa kwamba iwapo mwanadamu hatarejesha ushirika na Muumba wake, hawezi kupata maendeleo ya kweli. Yesu anasisitiza, ‘Ni lazima uzaliwe mara ya pili’. Yesu anatilia mkazo umuhimu wa kumleta mwanadamu na kumfikisha mahali ambapo anaweza kupokea msamaha wa dhambi kutoka kwa Mungu na kurejesha ushirika naye. Hivyo Mungu anaweza kuingia ndani ya mwanadamu na kubadilisha maisha yake kuanzia ndani. Mtu huyu sasa anaweza kutumiwa na Mungu kubariki jamii yote (Yn 3:3,7).

Hayo ndiyo tuliyoweza kuyasikia kutoka kwa watu waliokuwa karibu sana na Yesu, kuhusu Agizo Kuu.

Sasa wewe sema hivi, ‘Ndiyo, Bwana, ingia ndani mwangu kwa ajili ya ulimwengu wa watu uliowafia’. 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu
Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili Ya Yesu Kristo


 

Kampuchea

Jina La Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Kru'ng

Kru'ng 2

10,000

Kui (Suai, Kuoy)

Kuy

16,000

 





 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index To All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk