1985 - 2007

 

14. Umisheni Ni Nini?

Usiniambie ni starehe kukaa nyumbani!

Support Pages   Index To All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma 
2 Kor 5:11-6:10

Mstari Wa Kukariri
Maana , upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote,basi walikufa wote; tena alikufa kwa ajili ya wote,  ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao (2 Kor 5:14,15).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Kufanya uinjilisti katika eneo unakoishi hakuna shida, lakini umisheni unaanzia wapi kwako, na utendaji wake unakuwaje? Je, unafikiria kwenda mahali?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Tafakari Zaburi ya 116 mstari kwa mstari uone ni mambo mangapi  aliyokutendea Bwana. Na kisha fanya uamuzi wa kuwa mwaminifu kwake na kuomba.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Angalia hatua za kuwafikia waliopotea kama zilivyoainishwa katika Rum 10:14,15. Zitambue na kuzielezea kwa maelezo ya kurasa mbili.

Tafakari Mistari Hii
Yn 1:40,41

Tumia Dakika moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Ugiriki
Idadi ya watu: 10,000,000; Dini: Orthodox, Waprotestanti ni 2% tu.

 

1. Umisheni Ni Nini?

Kila mwamini anajua kwamba cho chote alichonacho katika maisha haya na milele yote ni mali ya Mungu. Wakati tulipokuwa wenye dhambi na kuwa machukizo mbele za Mungu, Mungu mwenyewe alitutafuta na kutukomboa kutoka kwa Shetani kwa damu ya Mwanaye; na sasa ametufanya wana katika familia yake, akitubariki baraka nyingi (Yn 1:16).

Mwandishi Wa Zaburi Anauliza Kwa Niaba Yetu Sote
’Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote alionitendea?’ (Zab 116:12). Jibu letu leo halitofautiani na lile alilolitoa miaka mingi sana iliyopita, ‘Nitakipokea kikombe cha wokovu; na kulitangaza Jina la Bwana’ (ms 13).

Hatua Inayofuata Ni Umisheni
Tukiwa na moyo uliojaa upendo na shukrani kwa Yesu, tunakwenda hatua moja zaidi, ng’ambo ya eneo tulilozoea kufanya uinjilisti; na kukiinua juu kabisa  kikombe cha Mungu cha wokovu, ili kila mtu akione hata miisho ya nchi, na wao pia watake kukinywea kikombe hicho chenye maji ya uzima.

Biblia inasema kwamba tunapaswa kushuhudia Yerusalemu, ambayo ni mji wa nyumbani kwetu, kisha Yudea na Samaria ambayo ni miji na mikoa ya jirani, na kisha tuende hata miisho ya nchi. 

Paulo anapowaandikia rafiki zake wa kanisa la Korintho huko Ugiriki anawapa sababu nyingine zaidi na nzuri za umisheni.

2. Kumcha Bwana Kunatuhamasisha

Kumcha Bwana, phobos, kuna maana ya kuwa na hofu ya kumwudhi Mungu kwa kutokutii amri zake, pamoja na unyenyekevu na upendo kwake ndiko kunakotuhimiza sisi kumtii Yeye (2 Kor 5:11).

3. Mahitaji Ya Watu Yanatuhamasisha

 Tunapoona uovu ukiwa umewakamatia watu kwenye dhambi, magonjwa, kukosa haki, umaskini, kutokuamini, ubinafsi, na madhara yake yote, na mateso yanayosababishwa na uovu huo; mioyo yetu inataka tufanye kitu fulani; kwa sababu tunaufahamu wema wa Mungu na yale yote Yesu aliyotufanyia. Paulo anasema ni lazima tujaribu kuwashawishi watu kila mahali wapate kubadili misimamo yao wakubali kumfuata Yesu (2 Kor 5:11).

4. Tunasukumwa Na Upendo

Upendo kwa watu wote na kwa kujali hatima yao ndio uliompeleka Yesu Msalabani, na sasa upendo huo umeujaza moyo wa Paulo na kumfanya ashiriki katika mpango mkuu wa Mungu wa wokovu.

Nasi Pia Tunapaswa Kusukumwa Na Upendo
Tunapotambua kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya watu wote, nasi pia tunachagua kufa kwa kumpa maisha yetu na mipango yetu kama shukrani zetu; na kuanza kuishi kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya watu wengine po pote walipo (2 Kor 5:14).

5.Tunahamasishwa Na Umilele

Paulo anasema hatupaswi kuwatambua watu kwa mafanikio ya ulimwengu huu; tusiangalie cheo, wala utajiri, au nafasi ya mtu. Badala yake tuwaone kwa mtazamo wa kweli za kutisha za kaburi. Uchaguzi ni lazima ufanyike sasa kuhusu mahali pa kuishi milele kati ya mbinguni na jehanamu.

Je, Ni Kweli Watu Wamepotea?
Mtu wa kwanza, Adamu, kwa hiari yake aliamua kutokumtii Mungu na kuchagua kufuata uongo wa Shetani. Mungu naye akaamua kumwacha Adamu, na roho ya Adamu ambayo ndiyo iliyomjua Mungu ilikufa ndani yake. Adamu akabakiwa na mwili na nafsi tu, huku akimfuata bwana mkatili kifoni na kuelekea kwenye moto wa jehanamu ambao haukuandaliwa kwa ajili ya mwanadamu bali kwa ajili ya Shetani na malaika zake (Mt 25:41).

Mwanadamu Bado Amefungwa…
 …
na ule uamuzi wa kijinga uliofanywa na yule mwakilishi wetu na anatembea akiwa amepotea kuelekea kwenye umilele wa waliopotea ambako panatisha sana na ubaya wa huko ukishaingia huwezi tena kuukwepa na wala hauna mwisho. Kwahiyo Paulo alikuwa sahihi aliposema kwamba sisi tumekufa katika uasi na dhambi zetu tukimfuata Shetani na kuingojea hasira ya Mungu, mpaka hapo tutakapokuwa tumeokolewa na Mungu kupitia kwa Yesu ( Efe 2:1-3,5).

Kuokolewa Na Jehanamu
Neno la Mungu linasema kwamba mtu hana budi kuwa kiumbe kipya; kilichozaliwa mara mbili; mara ya kwanza katika mwili, na mara ya pili katika roho kwa uweza wa Roho Mtakatifu ( Yn 3:3-6).

6. Tunahamasishwa Na Injili

Wakati fulani tulimwona Yesu kwa namna ya kimwili, tukimwona yeye kama mwanadamu wa kawaida tu, aliyefanya historia kama watu maarufu waliopita. Lakini sasa tumegundua ya kwamba  kwa kweli alikuwa ni Mungu mwenyewe aliyekuwa Msalabani na akiwa anaupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, asituhesabie tena dhambi.

Hizi ni habari nyeti kati ya habari zilizowahi kusimuliwa katika historia ya mwanadamu na zinadai kukubalika na kupata jibu. Tuna ujumbe wa ajabu kwamba yule asiyekuwa na dhambi alifanyika dhambi na kulipa bei yake, yaani mateso na kifo, ili kwamba sisi tuliostahili adhabu tuweze kufanyika wenye haki na kuishi katika uwepo wa Mungu sasa na hata milele (2 Kor 5:18,19,21). Katika Mdo 4:12 tunaambiwa kwamba hakuna jina jingine tulilopewa litupasalo kuokolewa, isipokuwa jina la Yesu.

7. Wito Wenyewe Unatuhamasisha

Paulo anasema sisi tu mabalozi wa mbinguni, tukimwakilisha Mungu mwenyewe; Naye amekuwa akinena na watu waliotuzunguka na ambao hawana amani Naye. Na kama vile mabalozi wa kidunia wakiwa kwenye ukanda wa vita, mtindo wetu wa maisha kama wajumbe wa Mungu katika eneo la adui Shetani ni hatari na jambo linalohitaji uangalifu mkubwa (2 Kor 6:3-10). Kupitia kwetu Mungu anawahimiza na kuwataka watu wapatanishwe na Baba wa Mbinguni mwenye upendo.

Siku Iliyokubalika Ni Leo
Wakati uliokubalika ni sasa.

Kama si wewe, ni nani?

Na kama si sasa, ni lini?

(2 Kor 5:20 – 6:2)

Kwahiyo unaweza kuona kwamba kwa kumcha Mungu, mahitaji ya wanadamu, upendo wa Mungu, na kweli za umilele; habari nyeti tulizonazo za kusimulia, na wito wa Mungu, ni sababu tosha tulizonazo za kuchangia shughuli za umisheni; ikiwa ni karibu au mbali, ikiwa tunakwenda kwa maombi au kwa kutoa, ikiwa tunasafiri wenyewe au tunatuma mtu mwingine.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Bado Hawajafikiwa Na Habari Njema

 

 

Cameroon

Jina La Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Mada

Mada

17,000

Ngossi (Gevoko)

Gevoko

20,000

 






 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk