1985 - 2007

 

19. Yesu, Mmishenari Wa Mungu

Je, unakwenda mbali kwa kutumwa na Mungu? Nenda kama Yesu alivyokwenda!

Support Pages   Index To All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Mwanzo 11:1-9;   1Wathesalonike 1:1-2:16

Mstari Wa Kukariri
Ndipo niliposema, “Tazama, nimekuja (kama gombo la chuo nimeandikiwa) niyafanye mapenzi yako, Mungu”  Ebr 10:7;   (Zab 40: 6-8).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Kila mmoja amweleze mwenzake kuhusu utamaduni wake, na kutilia maanani yale yaliyoandikwa katika sehemu ya pili.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Kama umeokoka kipindi kirefu kilichopita inawezekana umeshasahau hali inavyofanana kuwa nje ya familia ya Mungu. Nenda katembelee baadhi ya mabaa, kumbi za starehe, sokoni, na michezoni. Wasikilize watu, angalia nyuso zao, jifunze kitu na kuona ni wangapi utakaowashuhudia.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Angalia dondoo ya 3 inayohusu hitaji la kuzoea mazingira. Andika taarifa ya kurasa mbili ukielezea mawazo yako kuhusu maana ya hayo yaliyoandikwa chini ya hivyo vichwa vitano. Je, wewe ungefanyaje katika mchakato mzima wa kukufanya ueleweke na watu wageni kwako.

Tafakari Mistari Hii Neno Kwa Neno
Ebr 10: 5-7

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la El Salvador

Idadi ya watu ni: 6,000,000;  Asilimia 80% ni maskini baada ya vita, matetemeko ya ardhi na mateso: Makanisa ya Kiinjili yamekuwa kutoka asilimia 2% hadi 20%.

 

Hadithi Ya Kweli

 Wapendwa fulani kutoka nchi za Magharibi waliokuwa na maono ya umishenari walikwenda nchi ya mbali bila kukaribishwa, na wala hawakujitambulisha kwa kanisa katika nchi hiyo. Hata washirika wenyeji hawakuwa na imani nao; na hatimaye wapendwa hawa wakajikuta wametengwa. Kwa miaka mingi wakabaki wametunza lugha yao, utamaduni wao, vyakula vyao, namna yao ya kufanya kazi na hata kuabudu. Hata leo mtu anayekuja kwao kwa ajili ya ibada hujisikia kama ni mtu asiyekubalika na mara huondoka.

Kwa masikitiko makubwa, huduma hiyo bado haijakuwa sana. Haishangazi kwamba huduma hiyo imedumaa, na wapendwa hawa hawaachi kuwalaumu wenyeji kwa kuwa na mioyo migumu. Lakini je, huo ndio ukweli wote?

1. Yesu, Mmishenari Wa Mungu

 Wakati Yesu alipomkubalia Baba kuja ulimwenguni katika Zaburi 2, alivuka kikwazo cha utamaduni. Aliacha usafi na ukamilifu wa nyumbani kwake mbinguni  na kuja kwenye ulimwengu uliojawa na dhambi, magonjwa, ubinafsi, mapepo wachafu na umaskini. Je, alikujakujaje?

Alikuja kwa Wayahudi akiwa mtoto mchanga na kwa wazazi Wayahudi. Yesu akachagua kuzaliwa kama watu wengi wa kawaida-maskini si matajiri, si watu wa kidini wala wenye uwezo. Aliishi kwenye familia ya mfanyakazi wa kawaida na akajifunza kuhusu maisha yao. Na kama mtu mwingine ye yote alijua joto na baridi, njaa na ukatili wa Warumi.

Wakati wa Mungu ulipofika alihudumu kama Myahudi kwa Wayahudi na kwa lugha yao akiheshimu utamaduni na mila za Kiyahudi. Alikuwa amefanana sana na watu hawa kiasi kwamba hata wale askari waliokuja kumkamata ilibidi waoneshwe Yesu ni yupi miongoni mwao. Yesu aliwachagua na kuwapa mafunzo watu wa kawaida kutoka miongoni mwa Wayahudi. Baada ya kufufuka kwake aliwaachia hawa rafiki zake hiyo kazi waifanye.

Je, Unaweza Kuona Tofauti?
Wale wapendwa katika hadithi ya kwanza walileta upendo wa Mungu lakini walidhani kwamba wale watu wangekubaliana na utamaduni wao. Wakati Yesu alipokuja na upendo wa Mungu aliingia kwenye utamaduni wetu ili aweze kutupata kwa ajili ya Mungu.

2. Je, Utamaduni Unakuwa Kikwazo Au Kibebeo?

Utamaduni ni nini? Ni mtindo wa maisha unaotambulisha kundi fulani la watu kwa lugha yao, tabia zao, mila zao, na mfumo mzima wa maisha ya jamii hiyo.

Utamaduni unahusisha tabia, lugha ya mwili, mahusiano na salamu. Ni namna watu wanavyoongea, wanavyokula, wanavyovaa, wanavyofanya kazi, wanavyoimba, wanavyocheza, na hata wanavyofanya biashara.

Unaweza kuona utamaduni katika ujenzi wa nyumba; majengo ya kuabudia, majengo ya serikali, mahakama na mashule. Unaweza kuona utamaduni miongoni mwa watu kwa jinsi wanavyoheshimiana, na vilevile misimamo katika kuheshimu faragha na kutunza muda.

Je, Utamaduni Ni Mzuri Au Ni Mbaya?
Katika kitabu cha Mwanzo mlango wa 10 na ule wa 11 mistari tisa ya kwanza, Biblia inatuonesha kwamba utamaduni ulianzishwa na Mungu alipowatawanya watu kuwa mataifa mbalimbali, na kuanzia hapo utamaduni huo umekuwa ukibadilika kwa karne nyingi. Leo hii Yesu anatupeleka kwa kila taifa, yaani kwa kila kundi lenye utamaduni mmoja, na siku ya mwisho watu kutoka kila utamaduni watakizunguka kiti cha enzi cha Mungu wakimwabudu.

Utamaduni ni kibebeo kikubwa cha injili, na wala si kikwazo. Kwanini? Kwa sababu watu wa kwanza kumpokea Kristo katika taifa wataweza kusambaza habari njema hizo kwa watu wao kwa urahisi zaidi kuliko wageni. Kama alivyofanya Yesu, wamishenari wanaweza kujiondoa na kuwategemeza hao wenyeji wa kwanza walioipokea injili ili waweze kuifanya huduma hiyo kwa uzuri zaidi.

3. Wamishenari Wazuri Mara Zote Wanajua Jinsi Ya Kuzoea Mazingira

Kuwapenda watu huleta mabadiliko makubwa yanayosababisha kujengeka kwa mahusiano. Tahadhari kama unadhani unajua sana! Ujumbe wa injili haubadiliki kamwe, lakini mbinu za kuufikisha zaweza kubadilika, la sivyo walengwa hawataelewa ni kwanini upo miongoni mwao na unachojaribu kusema.

Ukitaka kuona watu wengi wakimgeukia Kristo na kuacha kuitumikia miungu ya uongo, ni lazima pawepo na:

Uhusiano wa kirafiki,kati yako na hao watu.

Mawasiliano ya ujumbe wako.

Kueleweka, "Ndiyo, hili lina maana sawa kwangu kama kwako."

Mabadiliko katika maisha ya waamini wapya ili kuthibitisha wokovu.

Ubia katika hiyo injili.

4. Ufunguo Wa kwanza Ni ‘Mwonekano Wa Ulimwengu’

Mwonekano wa ulimwengu kwa mwanadamu ni namna ambavyo mtu mwanamume au mwanamke anavyomtazama Mungu mwenyewe na umilele. Wokovu na mabadiliko ni lazima yafanyike hapa na ndipo utamaduni ubadilike taratibu kukubaliana na Neno la Mungu. Kabla hujazungumza na watu ulioitwa kuwahudumia ni lazima uchukue muda kujifunza na ujue wao wanayaonaje maisha. Mtazamo wao wa ulimwengu unaweza kuwa wa kidini na kumhusisha Mungu au miungu, au imani zingine za kidunia kama ile ya Kimarx. Kutoka kwenye msingi huo ndiko kunakozuka imani zote, maisha na thamani zake, ziwe nzuri au mbaya.

5. Kama Paulo Alivyoweza, Na Sisi Pia Tunaweza!

Katika kitabu cha Wathesalonike wa Kwanza mlango wa 1 na wa 2 tunasoma namna wapagani walivyoacha sanamu na kuanza kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli. Paulo anasema injili haikuwajia watu hawa kwa maneno tu; kwahiyo na tujifunze vitu vingine vitatu vilivyohusika.

Mtindo wa maisha uliosababisha uhusiano wa kirafiki

Katika maisha ya Paulo waliona mambo bora yasiyopungua 12, na wakayaiga, mojawapo likiwa ni kukubali mateso (1The 2:3-8, 10-12).

Mawasiliano Na Kuelewana

Waliupokea ujumbe na kuuelewa kiasi cha kuziacha sanamu zao (1The 1:9).

Namna Paulo Alivyohudumu

Alijipatia riziki kwa kufanya kazi kama wao (1The 2:9). Alihudumu kwa uweza wa Roho Mtakatifu (1:5).

Katika miaka ya 1700 wamishenari wa Kimoravia walikubali kuishi na watu wenye ukoma ili wapate kuwaleta kwa Yesu; wakakubali kuwa watumwa ili watumwa hao wapate kumjia Yesu. Na leo hii huko nchini Philippines wamishenari wamekubali kuishi miongoni mwa maskini ili wapate kuwavuta kwa Kristo. Na huko Sahel mmishenari Keith Smith anaishi kwenye kibanda cha kabila la Fulani, anafuga ng’ombe kama watu wa kabila hilo, anakula chakula kilekile wanachokula wenyeji wake, anavaa kama wao, na kuzungumza lugha yao. Sasa ameanza kuwavuta kwa Yesu watu wa kabila la Fulani.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Bado Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

 

China (4)

Jina la Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Miao, Qiandong (Hmu Southern)

Miao, Qiandong Southern

500,000

Miao, Xiangxi (Ghao-Xong Eastern)

Miao, Xiangxi Eastern

80,000

Nunu

Bunu, Nunu

60,000

Palyu

Palyu

10,000

Shan (Tai Yay, Sha)

Shan

237,000






 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk