1985 - 2007

 

20. Kutafuta Msaada

Support Pages   Index To All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Wafilipi 1

Mstari Wa Kukariri
Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kwa kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo (Flp 1:19).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Thamani ya urafiki na maana yake kwako. Je, unao marafiki wa karibu? Kama huna mwombe Mungu na baada ya muda utaona yale atakayokufanyia.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Unaonaje ukiandaa tafrija nyumbani kwako na kuwaalika rafiki zako na kuwafahamisha yale Mungu anayokuagiza na kile unachokusudia kukifanya katika maisha yako. Tafuta marafiki na wala si fedha,usiitaje hiyo.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Fanya mazoezi kwa kuandika ukurasa mmoja wa waraka ukiwaeleza rafiki zako na kanisa lako kile unachokifanya. Waeleze unachokifanya na kwanini unakifanya. Waambie unakotaka kwenda, lini , na utakuwa na nani. Waambie namna utakavyofikia lengo lako na gharama zake.

Tafakari Mistari Ifuatayo
Ayu 16: 20,21

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la The Pacific. Idadi ya watu: 28,000,000.

Wakristo ni 75%. Kuna makabila machache hawajafikiwa.

 

Katika kuitikia wito wa Mungu  kuhusu Agizo Kuu, kwa vyo vyote utahitaji kutafuta namna ya kujikimu ama kwa kufanya kazi au kwa kutegemezwa na kanisa au huduma yako.

Angalia Sehemu ya Uchumi Wa Ufalme

Hapo utapata maelezo ya kutosha kuhusiana na namna ya kuweza kupata fedha na namna ya kuanza na kutekeleza Agizo Kuu.

Je, Itakuwaje Iwapo Kanisa Lako Litashindwa Kukutegemeza?

Si jambo la ajabu kanisa likishindwa kukutegemeza. Lakini hata ikitokea hivyo usijali kwa kuwa zipo njia nyingine ambazo pengine zaweza kuwa bora zaidi kuliko kupokea cheki kutoka kwa mweka hazina wako.

 Watu Wanahitajiana

Iwapo utaamua kuchangisha fedha, vema , utapata fedha kwa ajili ya matumizi. Lakini iwapo badala yake utaamua kutafuta marafiki, utapokea kutoka kwao upendo, watakuombea na kukushauri. Hekima yao na urafiki wenu waweza kudumu kwa muda mrefu na ukawa baraka kwako. Wakati mwingine fedha zinaweza kuwa na thamani ndogo kuliko marafiki. Soma habari za Paulo katika Wafilipi mlango wa kwanza.

Somo Kutoka Kwa Mungu Kwa Mambo Ya Asili
Mfano: Fikiria kuhusu mti uliokua na kusimama imara. Kumbuka kwamba chini ardhini mti huo una mtandao wa mizizi iliyosambaa na kufika mbali kwa kazi ya kuusimamisha huo mti na kutafuta maji. Hata upepo ukivuma, hata mvua kubwa ingenyesha, miti yetu inabaki imesimama.

Mtandao Wa Buibui

Sasa mtazame buibui. Utando wake uliosambaa unamwezesha kupata taarifa ya kiumbe cho chote kitakachosogelea. Buibui hukaa katikati ya mtandao imara aliousuka kwa ustadi. Makazi yake huyatumia pia kunasa chakula kwa ajili yake.  Upepo ukivuma buibui huyo ataendelea kubaki salama salimini.

Kupata Marafiki ni Muhimu, Si Fedha Peke Yake

Huduma ya umishenari inatakiwa kuwa ya njia mbili, ya kwenda na ya kurudi. Huduma kwa ajili ya watu ambao hawajafikiwa ni ya muhimu sana; lakini usisahau kuwarudia wale waliokutegemeza. Watu hao wangependa washiriki binafsi katika zoezi hilo la umishenari lakini kwa sababu ya majukumu ya nyumbani, umri au udhaifu wanashindwa. Wewe unafanyika kuwa mikono yao, miguu yao, na midomo yao. Wangependa kuona  unachokiona, kusikia unachosikia, na kuhisi unachohisi wewe. Hakikisha unawashirikisha.

Wanaokutegemeza Wanahitaji Kutegemezwa Pia
Kumbuka kwamba si kila anayekutegemeza ana kanisa linalomjali au hata mchungaji. Na upo uwezekano kwamba mtu pekee anayewaombea na kuwajali ni wewe. Hakikisha unatimiza wajibu wako mbele za Bwana.

Watendee Wengine Kama Ambavyo Wewe Ungependa Kutendewa
Ikiwa utapanda mbegu za huruma, fadhila, na kuwajali wengine, basi utarajie kuvuna yayo hayo. Zawadi ndogondogo na postikadi ni muhimu hasa kwa wale watu wanaokaa nyumbani.

Kuna Mtu Mahali Fulani Anasubiri Kusikia Kutoka Kwako
Watu siku hizi hawajali sana suala la mawasiliano. Wanaonekana wako ‘bize’ kiasi kwamba hawana nafasi ya kutuma wala kupokea habari. Wewe usiwe kama hao. Tuma postikadi yenye mistari michache ya maneno ya kumtia moyo; wakumbuke katika matukio mbalimbali ya kukumbukwa kama vile sikukuu ya kuzaliwa. Fanya mawasiliano kwa njia ya posta, simu, faksi, barua pepe mesenja, na njia nyingine yo yote itakayokuwezesha wewe kuwasiliana na rafiki zako na kuwaambia ‘asante kwa msaada wako’.

Mtazame Yesu
Hatuwezi kupuuzia umuhimu wa rafiki zako. Kikundi cha watu sita au hata kumi na wawili kinaweza kuwa cha thamani kubwa sana kwako kuliko ushirika mzima uliokusahau katika kipindi kifupi. Nyuma ya kila mmoja wetu ipo neema ya Mungu, nawe unapaswa umtumaini Yeye huku ukiishi maisha matakatifu na ya maombi. Pia uwe na imani na kuzitazamia ahadi zake.

Utaanzia Wapi?

Jambo la kwanza, ni lazima uanze; ukikumbuka kwamba ishara zitakufuata, lakini ni mara chache sana zitakuja kama hujafanya lo lote kwa imani (Mk 16:17).

Waache Watu Wafahamu
Je, unakumbuka kufufuliwa kwa Lazaro? Yesu alifanya ule mwujiza na watu wengi walihusika siku ile. Watembelee watu majumbani kwao, na marafiki Mungu atakaokupa. Wafahamishe maono yako ili upate kutoka kwao imani na maombi. Mungu anaweza kuwagusa wakakuuliza kama utahitaji msaada wo wote wa kifedha wakati huo au baadaye. Vinginevyo uwe na juhudi katika kutafuta marafiki; suala la fedha litafuatia baadaye. Watakapoamua kukupa fedha ni lazima uwe na moyo wa shukrani kwa sababu wao ni neema ya Mungu kwako.

Tambua Mahitaji Yako, Andaa Bajeti
Gawanya mahitaji yako ili kuufanya mzigo kubebeka kirahisi. Kwa mfano: tuchukulie kwamba hitaji lako ni Sh. 10,000 kwa mwezi; unahitaji watu 10 watakaotoa Sh. 1,000 kila mmoja. Ni vyepesi zaidi kuzungumzia Sh. 1,000 kuliko kuzungumzia Sh. 10,000 kwa mtu mmoja.

Tahadhari: Ulinde Sana ‘Mshipa Wako Wa Fedha’!
Yule adui atapenda sana kuubana mshipa wako wa fedha kwa sababu anajua akifanya hivyo mwendo wako kimaisha utapungua sana. Chukua tahadhari kubwa kutokana na mashambulizi yake, na usikubali kuanguka kwenye majaribu yake ya kukufanya uishi kiujanjaujanja, au kukurudisha nyuma katika kumtolea Mungu kwa uaminifu. Anaweza akakujaribu katika wito wako, au katika fedha, na pengine kukutegea katika kuchukuliana na watu hata wale wasiofaa kwa sababu tu wana fedha. Mkaribie Mungu, wasamehe wale wote wasiokuwa tayari kukusaidia; na sikuzote wafanye rafiki zako kuwa watu muhimu kwako.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Bado Hawajafikiwa Na Habari Njema Za Yesu

 

 

China

Jina La Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Wunai

Bunu, Wunai

13,000

Yang Huang

T'en

20,000

Younuo

Bunu, Younuo

13,000

Yung-Chuun

Yongchun

12,000






 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk