1985 - 2007

 

21. Hatua Za Kwanza

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Mdo 2:22-47

Mstari Wa Kukariri
"…Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu (Mdo 2:38).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, nyote mmetubu, mmebatizwa, mmempokea Roho Mtakatifu, na kujiunga na familia ya Mungu? Kama bado fanya mipango sasa.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Andaeni orodha ya vitabu vya kujifunza Biblia vinavyoweza kupatikana miongoni mwenu, au majumbani kwa waamini wengine, na hata maktaba. Tafuteni vitabu vya itifaki, kamusi za Biblia, na vya mafafanuzi na kamusi za lugha za zamani kwa mfano za Kiebrania na Kiyunani. Vitawasaidia sana katika huduma.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Chunguza ili kupata idadi ya mabatizo ya maji katika Agano Jipya, na kisha andika taarifa ya kurasa mbili.

Tafakari Andiko Hili
Kol 3:1-10

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea Saudi Arabia . Gharama ya kumfuata Yesu katika taifa hilo ni kifo. Karibu watu wote wapatao 17,000,000 ni Waislamu.

 

 

Katika Biblia Takatifu tunasoma jinsi Petro alivyowahubiri kundi kubwa la watu waliomkimbilia kuja kuona mwujiza wa waamini wa kwanza waliojazwa Roho Mtakatifu. Waliposikia habari za kuja kwa Yesu,  Mwana wa Mungu  na maisha yake, kifo chake kilichotokea mikononi mwa viongozi wao, kufufuka kwake na Ubwana wake mkono wa kuume wa Mungu, walimwuliza Petro swali muhimu sana ~

 

1. Je, Tufanyeje?

Jibu la Petro katika Mdo 2:38 linatujulisha mambo matatu muhimu ya kutuwezesha kujiunga na familia ya Mungu. Je, ni mambo gani hayo?

Tubu
Tunaweza tu kutubu wakati Roho Mtakatifu anapozungumza na mioyo yetu nasi tukapata kufahamu madhara ya dhambi zetu mbele za Mungu Mtakatifu. Kwa kweli tunajutia dhambi zetu na kukiri na kisha tunatubu. Toba maana yake ni kugeuka nyuma na kuelekea huko ulikogeukia. Tunatubu tunapoacha kutembea katika njia za dhambi za ulimwengu huu na kuchagua kutembea katika njia za Mungu, na kumwomba atuwezeshe kufanya hivyo.

Ubatizwe
Petro alisema baada ya toba, kila mmoja abatizwe kwa jina la Yesu Kristo kudhihirisha kwamba amepokea msamaha wa dhambi zake. Ubatizo ni jambo la kimila ambalo walifanyiwa watu walioamua kujiunga na imani ya Kiyahudi, kwahiyo watu waliokuwa wakimsikiliza Petro walimwelewa. Lakini ubatizo wa wafuasi wa Yesu ulikuwa na maana zaidi ya mila tu au sherehe. Ni kumfuata Bwana, ni mlango wa kuingilia katika maisha mapya kwenye familia mpya.

Pokea Zawadi Ya Roho Mtakatifu
Hatuwezi kamwe kuishi maisha ya ushindi bila uwezo na uwepo wa Roho Mtakatifu. Ni Yeye anayeweza kumbadilisha mtu kutoka dini iliyokufa na kumfanya kuwa na uhusiano ulio hai na Mungu. Tunamhitaji huyo atujaze maisha yetu na maisha ya waamini wenzetu. Kumpokea Roho Mtakatifu maishani mwetu ni muhimu sana na Petro anasema hilo ni moja ya mambo muhimu ya kwanza ya kufanya. Baada ya ubatizo tunapewa Roho Mtakatifu tumnywe (1 Kor 12:13).

 

2. Yesu Mwenyewe Alibatizwa

Katika Mt 3:13-17 tunaweza kusoma habari za Yesu ambaye ni mfano bora wa maisha. Yeye alianza huduma yake baada ya kubatizwa.

Kubatizwa Kunadhihirisha Utii Kwa Yesu
Katika Mt 28:19 Yesu aliagiza kwamba watu wabatizwe; na katika Yn 15:14 alisema sisi ni rafiki zake kama tutazishika amri zake. Hebu soma pia Mdo 5:32.

Ni Nani Abatizwe?
Katika Biblia tunaona kwamba wanaobatizwa ni waamini pekee. Kila mwenye uwezo wa kuamini na abatizwe.

Je, Tendo La Ubatizo Linafanyikaje?
Neno ‘kubatiza’ katika Biblia lina maana ya kuchovya au kuzamisha; kwahiyo ina maana waamini wa kwanza walizamishwa ndani ya maji kwa muda mfupi, na kuibuliwa tena.

Ni Nini Kinachotukia Wakati Wa Ubatizo?

1.    Ubatizo ni ungamo la hadhara la Imani mtu aliyonayo kwa Mungu kupitia kwa Yesu; na ni tamko kwa Mungu, kwa malaika, kwa mapepo, na kwa wanadamu kuhusu nia ya mwamini kumfuata Yesu (Mk 8:38).

2.    Katika ubatizo mwamini anatambua kwamba Yesu alipokufa Msalabani utu wake wa kale ulikufa pamoja na Bwana. Dhambi zake zimeoshwa na sasa maisha ya zamani yanazikwa kama vile Yesu alivyokufa na kuzikwa. Mwamini anapoibuka kutoka majini anatambua na kwa imani anapokea maisha mapya akiwa ameunganishwa na Yesu katika nguvu ya ufufuo (Rum 6:3-6).

3.    Ubatizo ni tamko la mwamini kwamba anajiunga na familia ya watu wa Mungu (1 Kor 12:12,13).

Je, Ni Lini Mwamini Abatizwe?
Mapema iwezekanavyo. Katika Mdo 2:38 wale watu walibatizwa siku ileile walipomwamini Yesu. Ubatizo ni namna ya kupokea neema ya Mungu, na mwamini mpya anaihitaji neema hiyo mwanzoni anapookoka ili imwezeshe kusimama.

 

3. Karibu Kwenye Familia Ya Mungu

Unapoamua kumfuata Yesu kwa kweli unajiunga na familia kubwa. Haiwezekani ukamfuata Yesu na huku unajifanyia mambo yako tu. Ni muhimu sana ufanyike sehemu ya familia ya Mungu, yaani kanisa lake. Utagundua kwamba kujiunga na kanisa kunaleta usalama na uimara katika maisha.

Je, Mwamini Ajiunge Na Kanisa Lipi?
Siku hizi kuna makusanyiko mengi ya waamini; mengine ni ya kizamani, na mengine ni ya kisasa; lakini kanisa zuri ni lile lenye sifa kama zile zilizoonekana katika kanisa la kwanza, yaani kanisa la Agano Jipya (Mdo 2:42-47).

·         Kudumu katika mafundisho ya mitume, ambayo leo hii tunayo katika Biblia. Mambo ya kwanza kabisa tunayopaswa kujifunza ni toba, imani kwa Mungu, mabatizo, kuwekea mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele (Ebr 6:1,2).

·         Kudumu katika urafiki wa kweli.

·         Kudumu katika kupokea neema ya Mungu katika kumega mkate.

·         Kudumu katika maombi.

·         Kulikuwepo pia heshima na ibada mbele za Mungu, miujiza na waamini kuongezeka. Watu walishirikiana mali zao, walisaidia maskini, na walikusanyika ili kumtukuza Mungu majumbani mwao na hekaluni.

Lakini kumbuka kwamba toba, kubatizwa, kujazwa Roho Mtakatifu na kujiunga na familia ya Mungu, ni mwanzo tu wa mambo. Yapo mengi zaidi ya kugundua.

 

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili

 

Misri

Jina La Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Albanian (Shqip)

Albanian, Tosk

18,000

Dom Gypsy (Nawar, Ghagar, Helebi)

Domari

234,000

Waarabu wa Libya

Kiarabu, Kibedawi cha K/Mashariki

300,000






 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk