1985 - 2007

 

22. Kuwa Na Uhakika

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Waefeso 2

 

Mstari Wa Kukariri
“Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu” (1Yoh 5:13).

 

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Jadilianeni kila mmoja wenu aeleze mabadiliko na changamoto ambazo  ameziona maishani mwake, na zinazomfanya aamini kwamba Mungu yuko ndani yake akitenda kazi.

 

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Ruhusu huo upendo mpya ujieleze wenyewe kwa kuandaa kuibariki familia yako, jirani zako au walio maskini, kwa huduma ya vitendo. Toa taarifa ya yale yanayotukia.

 

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika taarifa ya ukurasa mmoja au mbili ukielezea tofauti unazoziona kati ya maisha yako ya zamani na maisha mapya yanayojitokeza unavyoendelea kuishi ndani ya Bwana. Tumia dondoo za Yohana kama vichwa vya aya.

 

Tafakari Mstari Huu
Yn 5:24

 

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Indonesia. Idadi ya watu: 195,000,000. Asilimia 87% ni Waislamu pamoja na watu wa imani ya Java. Kumekuwepo na ukuaji mzuri wa kanisa katika kipindi cha miaka 30.

 Pamekuwepo na mateso kwa siku za karibuni.

 

 

Biblia inaahidi kwamba tunapoiamini Injili, tukampokea Yesu awe Bwana na Mwokozi, na kuamua kumfuata siku zote za maisha yetu; tunatoka gizani na kuingia nuruni, tunatoka chini ya utawala wa Shetani na kuwa chini ya utawala wa Mungu. Tunapokea msamaha wa dhambi zetu, na nafasi miongoni mwa wale waliotakaswa kwa imani (Mdo 26:18).

 

1. Je, Tunawezaje Kuwa Na Uhakika?

Maisha kama mwamini maana yake ni kuenenda kwa imani, na wala si kwa kuona. Je, tunaweza kuwa na uhakika kwamba kweli Mungu ametuokoa kutoka utawala wa Shetani na kutuhamishia kwenye ufalme wa Mwana wa pendo lake?

Je, Tunawezaje Kuwa Na Imani Iliyotimilika Kwa Mungu Bila Kuwa Na Shaka?

(2 Kor 5:7) (Kol 1:13) (Ebr 10:22)

 

Mungu Si Mwanadamu Hata Aseme Uongo

(Hes 23:19)

Jibu lipo katika kuamini yale asemayo Mungu katika neno lake. Hilo ni la uhakika kwa kuwa Mungu wetu habadiliki.  

 

Ameahidi Wokovu

(Zab 91:16) (Isa 45:17) (Mk 16:16) (Lk 19:9) (Mdo 11:14) (Mdo 16:31).

 

Anasema Ametufanya Wake

(Yn 1:12) (Rum 8:15) (2 Kor 6:18) (Gal 3:26) (Gal 4:5,6) (Efe 1:5).

 

2. Hapa Pana Waraka Wa Upendo Kutoka Kwa Mungu

Waraka huu uliandikwa na rafiki mkubwa wa Yesu, Yohana, ambaye hujulikana pia kama mtume wa upendo. Alivuviwa na Mungu kuandika waraka huo ili kujibu swali hili kwamba ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa na uhakika kwamba Mungu amekuja maishani mwetu na anatenda kazi ndani yetu. 

Yohana anasema, ‘Ninawaandikia ninyi mnaoliamini Jina la  Mwana wa Mungu ili mpate kujua kwamba mnao uzima wa milele’ (1 Yoh 5:13).

 

Tunaweza Kujua Sisi Ni Watoto Wa Mungu

Kwa vipi? Kwa  kuona mambo mapya yanayotukia ndani yetu na katika mazingira yetu, na ambayo hayakuwahi kutukia kabla ya hapo. Huo ni utendaji wa Mungu. Ijapokuwa wakati mwingine tunashindwa na pengine kuanguka, lakini hata hivyo Mungu ameianza kazi yake ndani yetu na atahakikisha imekamilika (1 Yoh 3:2) (1 Yoh 5:19) (Flp 1:6).

 

3. Je, Waweza Kumwona Mungu Akitenda Kazi?

 

Je, Roho Mtakatifu Anatenda Kazi Ndani Yako?
Ni Roho Mtakatifu anayekupa amani moyoni mwako, na kukuhakikishia kwamba wewe ni mwana wa Mungu. Na kwa msaada wake tayari unamwita Mungu “Baba” (1Yoh 3:24) (1 Yoh 4:13) (Rum 8:16) (Gal 4:6).

Pengine umeshagundua kwako baadhi ya karama ambazo Roho Mtakatifu humletea kila mwamini.

Unapoona mstari fulani katika Biblia unakupa nuru na kuzungumza nawe, huyo ni Roho Mtakatifu anayekufundisha. Waweza kuwa na uhakika pia kwamba ameanza kukuongoza katika maombi. Na moyo wako unapotatizwa, dhambi inapokunyemelea na kujaribiwa, uwe na uhakika ni Roho Mtakatifu anayekutia moyo kuchagua njia ya utakatifu.

 

Je, Unaelekea Kufanana Na Yesu?
Tulizoea kuishi maisha ya kibinafsi, lakini sasa waonaje, hakuna upendo mpya na huruma vinavyojitahidi kujitokeza kwa ajili ya rafiki na maadui pia? Hilo ni tunda la Roho Mtakatifu; Mungu anatenda kazi ndani yako (1Yoh 3:2).

 

Je, Ndani Yako Kuna Mtiririko Wa Upendo Unaoingia Na Kutoka?
Hiyo ni ishara ya uhakika kwamba Mungu yuko maishani mwako kwa sababu Mungu ni upendo. Si kwamba ana upendo, bali Yeye ni upendo; hiyo ni asili yake (1Yoh 4:16).

Kwa kadiri unavyoishi katika upendo wa Mungu, ndivyo unavyojikuta mwenyewe unampenda. Mara atakuelekeza kuwapenda watu wengine pia kwa upendo ule atakaokupa mwenyewe; uweze kuwapenda hata wale walio wagumu kupenda. Tazamia upendo mpya katika familia yako kuwabariki wazazi na ndugu, hata kama siku za nyuma walikutukana au kukudharau. Mumeo/mkeo atabarikiwa kwa upya wako unaojitokeza na pengine anaweza kukuuliza ni nini kinachoendelea (1Yoh 5:2,3).

 

Je, Unawapenda Watu Wa Mungu?
Awali uliwaza kuwa watu wa Mungu ni wa ajabu  na pengine ni wabaya! Sasa umepata upendo mpya  ukikua ndani yako kwa ajili ya ndugu na dada zako, na unapenda kukaa pamoja nao. Na pengine unawaza ni nini unachoweza kufanya  ili kuwasaidia ndugu wenye shida (1Yoh 3:10,14,16,19).

 

Je, Unasema ‘Hapana’ Kwa Dhambi?
Awali dhambi ilikukamata nawe ukafuata matakwa yake, lakini sasa umeacha kufuata njia yako mwenyewe na kuichagua njia ya Mungu. Kila mtu hushindwa hapa na pale. Wewe utaona ongezeko la ushindi dhidi ya mawazo mabaya, tabia mbaya, na lugha mbaya (1 Yoh 3:10) (1 Yoh 5:18).

 

Je, Unazitii Amri Za Mungu?
Awali hatukuzitii, na hata tulipojaribu tulishindwa; lakini sasa kuzitii amri za Mungu  ndicho hasa tunachopenda. Na kwa kadiri tunavyoendelea kumpenda Mungu, ndivyo anavyozidi kulimimina pendo lake maishani mwetu (1 Yoh 2:3) (1 Yoh 2:5) (1 Yoh 5:3).

 

4. Ili Upate Kumjua Mungu Vizuri Zaidi, Tembea Pamoja Naye

Biblia inatuambia katika kitabu cha Amosi 3:3 kwamba tukubaliane na Mungu ili tuweze kutembea pamoja Naye. Na kwa kadiri unavyoendelea kufanya hivyo ndivyo hivyo unavyozidi kujua kwamba unao uzima wa milele, na ndivyo unavyozidi kupata ujasiri wa kumwendea Mungu aliye Baba yako na kumwomba cho chote sawasawa na mapenzi yake. Hatimaye utagundua kwamba ukiomba sawasawa na yale anayokufunulia utayapokea. Maombi yaliyojibiwa ni ishara ya uhakika ya kwamba umejizatiti katika ufalme wa Mungu. Ongeza bidii katika kumjua Yesu zaidi na zaidi (1 Yoh 5:15,20). 

 

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili  

 

Eritrea

Jina La Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Saho

Saho

76,000

Waarabu wa Saudia(Rashaida Adalah-Mu'allin)

Kiarabu, Hijazi

34,000

Waarabu wa Sudan

Kiarabu cha Sudan

75,000

Kiarabu cha Yemen  

Kiarabu, Ta'izzi-Adeni

18,000






 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk