1985 - 2007

 

25. Neno La Mungu

Biblia ni Neno la Mungu lililo hai

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Zaburi 119: 9-11,105;
Waebrania 4:12;  Marko 4:21-29.

Mstari Wa Kukariri
Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema           (2Tim 3:16, 17).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, unaamini kuwa Neno la Mungu ndilo lenye mamlaka yote katika maisha?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Jitahidi kutenga muda maalum kila siku kwa ajili ya kutulia na kutafakari. Tekeleza mpango wa kusoma Biblia. Andaa alama saba za kuweka katika Biblia yako pale unapoachia kusoma ili uweze kupapata kirahisi utakapoendelea kupasoma tena wiki inayofuata.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Kutoka katika 2Fal 22:8-13 na 2Fal 23:1-32 andika mageuzi yote aliyoyafanya mfalme Yosia baada ya kulisikia neno la Mungu.

Tafakari Andiko Hili
Mathayo 7:24-27

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Ujerumani.

Idadi ya watu: 80,000,000. Idadi ya Wakristo ni 75%

Ujerumani Mashariki maskini na Ujerumani Magharibi tajiri sasa zimeungana. Makanisa ya zamani yanapoteza watu. Uamsho unatakiwa haraka

 

1. Biblia Ni Neno La Mungu

Kwa kila mwamini neno la Mungu ni la kipekee na la thamani kubwa. Kwa karne nyingi zilizopita watu wengi wametoa maisha yao katika kuhifadhi kweli ya neno la Mungu kwa ajili yetu ili tupate kusoma. Kwa kuzingatia thamani kubwa ya neno la Mungu, na andiko kutoka Mk 4:21, swali ni hili, ‘Biblia iko wapi katika maisha yako?’

Je, imefichwa mbali;

Au imewekwa mahali pa juu ili ipate kumulika kila eneo la maisha yako?

2. Baraka Katika Neno La Mungu

Neno lake li hai, linanena nawe na kutenda kazi ndani yako (Ebr 4:12,13).

Neno lake ni kioo kinachokufanya ujione ulivyo kadiri unavyoendelea kulisoma. Neno lake kamwe halitakufanya ujidanganye mwenyewe, wala kuficha ukweli (Yak 1:22-24) (Mk 4:22).

Neno lake litakuandaa kikamilifu ili uwe, na ufanye kile Mungu anachotaka (2 Tim 3:15-17).

Kuanzia ulipokuwa mtoto hadi sasa umeyajua Maandiko Matakatifu yanayoweza kukupa hekima unayoihitaji kwa ajili ya kupata wokovu kwa imani katika Kristo Yesu. Maandiko yote yana pumzi ya Mungu na yanafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.

Inasemekana, na ndivyo ilivyo, kwamba Biblia ni Mwana wa Mungu katika maandishi, kwa sababu Yesu anaitwa ni Neno, na vilevile anaitwa Kweli (Yn 1:1).

Je, Unataka Kufanikiwa Na Kustawi?
Basi fanya yale Yoshua aliyoagizwa kufanya (Yos 1:8). Na kama unataka kustawi kwa kila kitu zingatia Zab 1:1-3.

3. Je, Unaposoma Unasikia?

Je, umewahi kugundua kuwa unaposoma neno la Mungu ‘unasikia’ kwa ndani na si kwa masikio ya nje? Hiyo ni sauti ya Mungu. Yapasa tuwe makini na kile tunachosikia kwa sababu kwa kipimo kilekile tunachotumia, ndicho tutakachopimiwa (Mk 4:24).

4. Je, Unalitumiaje Neno La Mungu?

Unalitumia hilo neno kufanya upya moyo wako (Rum 10:17).

Unalitumia hilo neno kufanya upya mawazo yako Rum 12:2).

Unalitumia hilo neno kufanya upya maneno yako (Rum 10:10) (Mit 18:2).

Ulitumie hilo neno kufanya upya matendo yako (Yn 14:15).

Ulitumie hilo neno kuimarisha ushindi wako. Shetani hakuwa na usemi Yesu aliposema, ‘Imeandikwa’! (Mt 4:1-11)-zingatia mistari ya 4,7 na 10.

Litumie Neno Kuhuisha Maombi Yako
Waamini wa kwanza mara kwa mara walinukuu maandiko ili yawaongoze katika maombi, na Mungu alijibu haraka (Mdo 4:23-31). Iwapo utaomba kwa kutumia neno la Mungu, yafuatayo yataanza kutokea:

Kwanza, unapanda mbegu ya neno.

Kisha kwa uvumilivu katika kuliomba neno, na saburi, huja masuke. Na kwa kadiri unavyoendelea kuwa na imani kwa Mungu na katika neno lake, huja ngano pevu, nafaka kukomaa na hatimaye mavuno.

(Mk 4:14, 26-29) (Isa 55:10, 11) (Mwa 8:22).

 

Ni Muhimu Kuwapa Wengine Neno La Mungu
Ni muhimu kwa sababu ye yote mwenye neno la Mungu anaweza kuokolewa na kupewa zaidi, mathalani: uponyaji, uhuru, uongozi, baraka na ustawi, kwa kuliamini. Lakini mtu asiye na hilo neno la Mungu ili kuliamini na kulifanyia kazi, hana baraka yo yote katika hizo zilizotajwa, na atapoteza hata hicho alichonacho, yaani maisha yake na nafsi yake milele (Mk 4:25).

5. Unapataje Kulisikia Neno?

Mungu amefanya iwe rahisi sana kuisikia sauti yake. Wewe kaa peke yako na Yeye, na kisha fungua Biblia yako. Kiri udhaifu wako na omba kujifunza kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Chukua muda kutafakari yale uliyosoma na kusikia, kwa sababu kwa njia hiyo utashangaa kuona jinsi Mungu atakavyozungumza na wewe na kujibu maswali yako.

Nikiwa mwamini mpya sikuyajua mambo haya.  Nilihudhuria kwenye kusanyiko la maombi na kimyakimya niliomba kwa ajili ya kazi yangu, nikamwombea mke wangu na watoto kwa sababu ya matatizo yote tuliyokuwa nayo. Baada ya muda mfupi nilihisi msukumo wa kuichukua Biblia yangu na ikafunguka yenyewe katika Zaburi ya 128. Na nilipoanza kusoma Mungu alinistusha na baadaye akanipooza  kwa neno lake akiuambia moyo wangu:

“Wamebarikiwa wote wamchao Bwana na kutembea katika njia zake.

Utakula matunda ya kazi yako, baraka na kustawi vitakuwa vyako.

Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, na wanao kama matawi ya mtende mezani pako”.

Naliliamini neno la Mungu na leo hii, baada ya miaka kadhaa kupita naweza kuona jinsi Mungu alivyoitunza ahadi yake kwa kuibariki familia yangu na kazi yangu.

6. Namna Ya Kufurahia Usomaji Wa Biblia

Watu wengi huanza na kitabu cha Mwanzo na baadaye huacha wanapokutana na sehemu ngumu katika Agano la Kale ambazo hawazielewi. Sisi sote tunapenda kula vyakula mbalimbali siku kwa siku, na hivyo ndivyo ilivyo hata kwa chakula cha kiroho. Jaribu kufuata mpangilio ufuatao nawe utapata mlo tofauti kila siku. Kila siku soma Zaburi za kuabudu na Mithali kwa ajili ya kupata hekima.

Jumatatu

Hadithi za watu mashuhuri na za historia ya Biblia. Anza na kitabu cha Mwanzo na kuendelea hadi kitabu cha Esta.

 

Jumanne

Taarifa za watu waliomjua Yesu vizuri. Anza na injili ya Mathayo  na kuendelea hadi ya Luka.

Jumatano

Tembea katika vilima na mabonde ya ushairi. Anza na kitabu cha Ayubu  hadi Wimbo Ulio Bora.

Alhamisi

Nyaraka za upendo kutoka kwa Yohana. Anza na injili yake, ikifuatiwa na nyaraka zake, na kuishia na Ufunuo wake.

Ijumaa

Unabii wa Biblia. Anza na Isaya na kuendelea hadi Malaki; utastaajabu.

Jumamosi

Nyaraka kutoka kwa watu mashuhuri wa Mungu. Anza na Warumi, endelea hadi Petro na Yuda.

Jumapili

Tembelea makanisa yaliyo hai na misheni zilizoko mstari wa mbele kwa kusoma kitabu cha Matendo ya Mitume.

 

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Bado Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

 

Georgia

Jina la Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Zaza, Northern

Kirmanjki

35,000






 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk