1985 - 2007
31. Uzima Tele
Support Pages
Index to All Lessons School of Finances
World Christian News
Who
Are We? Site Index
Katika Biblia Yako Soma
1 Yoh 2:12-14 na Gal 5:16-26
Mstari wa Kukariri
Mwivi haji ila aibe na kuchinja na
kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele (Yn 10:10).
Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Waefeso 4:18 inatuambia kwamba
wanadamu kwa mara ya kwanza walitenganishwa na uzima wa Mungu kwa anguko. Je,
maisha kwa Adamu yalikuwaje?
Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Tafakari juu ya ufunuo uliopo
katika Rum 6:1-6 na kila siku endelea kukiri kweli hizo kwa sauti na kuzipokea
kwa imani na maombi. Mwombe Mungu aifanye hiyo kweli kuwa halisi na uzoefu
kwako. Weka kumbukumbu za mabadiliko kwa jinsi yanavyotukia.
Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Soma Gal 2:20; Kol 1:29; Efe
3:20; na Flp 2:13 na kisha andika maelezo ya ukurasa mmoja ukionesha imani ya
Paulo katika kukabiliana na maisha na huduma.
Tafakari Juu Ya Andiko Hili
Gal 2:20
Tumia Dakika Moja Kuubadili Ulimwengu
Ombea taifa la Liberia. Idadi ya watu: 3,000,000. Asilimia 37% ni Wakristo. Ni taifa lililoharibiwa na vita. Waamini wengi ama wamekufa au wameikimbia nchi. Ni kazi ngumu kuijenga upya.
1. Maisha Ya Ushindi Ni Nini?
Katika Yn 10:10 Yesu anatumia neno zoe kwa lugha yake mwenyewe, akimaanisha uzIma. Mara nyingi watu hudhani kwamba uzima hupimwa kwa kuzingatia wingi wa mali tulizonazo, lakini Yesu hakubaliani na hilo (Lk 12:15). Zoe ni maisha Yesu aliyoishi; maisha ya Mungu mwenyewe, uzima wa milele, uzima tele, uzima halisi na wa kweli; maisha motomoto na ya kiutendaji, ufuasi na utii kwa Mungu, yaliyobarikiwa sasa, na kudumu milele.
Mpango Wa Mungu Kwa Ajili Yako Ni Zoe Pia
Warumi 8:29, 30 inasema ~
Anavifanya vitu vyote vitende kazi kwa mpango na makusudi yake, kwa manufaa yako.
Alikujua wewe kabla ya nyakati kuanza.
Alikuita.
Alikufanya mwenye haki, akazichukua dhambi zako.
Anajishughulisha sana kukufanya wewe ufanane na Yesu.
Ameshakutukuza tayari, na kwa imani utukufu ni hatima yako ya uhakika.
2. Je, Ina Maana Gani Kufanana Na Yesu?
Mungu anaposema anatufanya tufanane na Mwanaye, hana maana ya kufanana kwa sura ya nje bali kwa ndani, yaani maisha maadilifu. Mungu anawachukua watoto wake katika safari ya marejesho (Mwa 1:26) akitubadilisha kidogo kidogo tuendelee kufanana na Mwana wake Yesu, tukishiriki utakatifu wake, mawazo yake, asili yake na hata ubora wa maadili yake.
Tunataka kufanana na Yesu, lakini wakati mwingine tunafanya kosa la kujaribu kumsaidia Mungu kwa kujitahidi sisi wenyewe kuwa wema, au kwa kuzitii sheria za dini zetu. Tunafanya kila jitihada ya kibinadamu na baadaye tunakata tama kwa sababu hatufanikiwi. Mara tunagundua mgongano mkubwa ndani mwetu baina ya pande mbili zenye asili tofauti zinazopingana; asili yetu ya zamani ya dhambi, na asili yetu mpya ya upendo wa Mungu. Mioyo yetu ina shauku kubwa ya kutenda yale yanayompendeza Mungu, lakini mara kwa mara tumekuwa tukitenda kinyume chake (Gal 5:17-21) (Rum 7:15-25).
3. Je, Tunawezaje Kuachilia Uzima Wa Mungu?
a. Chagua Kuenenda Kwa Roho
Ni afadhali umruhusu Roho
Mtakatifu atawale maisha yako kila siku kuliko kujaribu kuishi kwa
kufuata sheria (Gal 5:1; 16:18). Mwache Roho Mtakatifu alete ndani mwako tunda
la Roho, yaani upendo, furaha, amani, uvumilivu,
utu wema, fadhili, uaminifu, upole, na kiasi (Gal 5:22, 23).
Mabawa Mawili Ya Njiwa Wa Mungu
Watu hufukuzia sana karama za Roho
Mtakatifu lakini tunda la Roho pia ni muhimu sana kwa sababu ni tabia ya Yesu.
Unapoona tunda unakuwa na uthibitisho wa uhakika ya kwamba Mungu anatenda kazi
ndani yako ili kukufanya ufanane na Yesu zaidi na zaidi. Tunda la maisha
yaliyobadilishwa ni ushuhuda mzuri pia. Roho Mtakatifu hupanda mbegu za tunda
ndani ya mioyo yetu, lakini ni lazima tuiruhusu mbegu ikue na kutusababishia
sisi maisha yanayofanana na ya Yesu ili watu wote waweze kuona.
Kwa mtu kuwa na ujuzi wa matumizi ya karama za Roho Mtakatifu peke yake haituhakikishii kwamba mtu huyo ni mwadilifu na kwamba anaishi maisha matakatifu. Kila mara tafuta tunda.
b. Chagua Kuyafisha Maisha Ya
Kale
Soma orodha iliyoko katika Gal
5:19 ili upate picha ya mtu anayeishi maisha ya peke yake. Hiyo asili mbaya na
ya zamani imetujia kutoka kwa mtu wa kwanza Adamu, ambaye alimwasi Mungu na
kuambatana na uongo wa Shetani.
Mungu alimwacha Adamu na roho yake ambayo ndiyo iliyomjua Mungu ikafa ndani yake; akawa amebakiwa na mwili na nafsi peke yake. Kutokea hapo, matakwa ya mwanadamu yakatawala maisha yake. Sasa anataka njia zake mwenyewe, na si za Mungu. Ni hiyo asili mbaya na ya zamani anayozungumzia Paulo akisema kwamba tunapaswa kuisulibisha, yaani, kuifisha (Gal 5:24).
Je, Unaweza Kujisulibisha Mwenyewe?
Jaribu! Simama, na ujifanye kama
una msalaba, nyundo na misumari kwa ajili ya mikono na miguu yako. Sawa, huwezi
kujisulibisha! Hata ungejitahidi namna gani huwezi kamwe kuifisha asili yako
mbaya na ya kale. Lakini kuna habari njema.
Yesu Amefanya Kwa Niaba Yako
Unalopaswa kufanya ni kupokea
mauti yale na maisha mapya kwa imani. Fanya hivi: Ukisoma kitabu cha Warumi
mlango wa 1 hadi wa 5 utagundua kwamba Mungu amemweka mwanadamu kwenye kona.
Mwanadamu ni mwenye dhambi asiyekuwa na msaada wo wote na hawezi kujiokoa
mwenyewe mpaka atakapogundua kwamba Yesu alimfia. Hilo humfanya mwanadamu awe na
amani na Mungu. Ukiendelea kusoma Warumi mlango wa 5 hadi wa 7 mstari wa 25
utagundua kwamba mwamini huyu asiye na msaada anawekwa kwenye kona nyingine ya
kukata tamaa na analia kuomba msaada (Rum 7:24). Kupatikana kwa jibu kunamletea
mtu huyu amani.
Jibu Ni Nini?
Linapatikana kwa kuamini (Rum 6:1-14).
Utu wetu wa kale ulikufa mara moja tu pale Msalabani pamoja na Kristo (ms 6).
Utu wetu wa kale uliofishwa, pia ulizikwa pamoja na Yesu (ms 4, 5).
Sisi tumeunganishwa na Yesu katika ufufuo wake, maisha yake mapya, zoe yetu. Tahadhari; utu wetu wa kale hautulii tu kaburini bila kufurukuta. Unapaswa kuvumilia katika ukweli huo ili kuachilia ushindi kamili (Rum 6:4, 5, 8, 10).
Kila siku jihesabu kuwa mfu kwa habari ya dhambi.
Kila siku jihesabu kuwa hai kwa Mungu na uutoe mwili wako autumie (ms 11).
Kwa imani achilia uzima wa Kristo na kutawala katika uzima huo kama Paulo alivyofanya. Soma shuhuda zake katika maandiko yafuatayo: (Gal 2:20) (Kol 1:29) (Efe 3:20) (Flp 2:13) (Rum 5:17).
Warumi 8 ni aya tukufu inayohusu maisha yanayoongozwa na Roho. Soma jinsi waamini wanavyotupilia mbali laana na sheria ya dhambi na mauti; na kuingia kwenye sheria ya Roho wa uzima, yaani zoe, maisha ya ushindi.
c. Hatimaye, Nenda Sawasawa Na
Roho
Katika Gal 5:25 Paulo anasema
kwamba kwa kuwa sasa tunao uzima wa kweli na halisi kwa uweza wa Roho, tunapaswa
kutembea naye katika hatua zinazofanana kama askari, tupate kustawi, na kuona
mambo yakibadilika na kuwa mema. Lakini Paulo anatahadharisha kwamba katika
maisha haya yenye kuongozwa na Roho hapakosekani majaribu; kwahiyo tuwe macho
(Gal 5:26 - 6:2).
Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina
India |
||
Jina la watu |
Lugha yao |
Idadi yao |
Kanjari (Kagari, Kangari) |
Kanjari |
55,400 |
Kawar (Kamari) |
Kawari |
33,800 |
Khirwar |
Khirwar |
34,300 |
Kisan |
Kishanganjia |
116,000 |
Korwa (Ernga, Singli) |
Korwa |
14,200 |
Kurichiya |
Kurichia |
12,100 |
Majhwar |
Majhwar |
28,000 |
Maria (Madiya, Muria) |
Maria |
134,000 |
1985 - 2007
With many thanks to Pastor Dastan
Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya
for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com
© Dr Les Norman The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide
copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial
purposes. Freely you have received, so please freely give.
Support Pages
Index to All Lessons School of Finances
World Christian News
Who
Are We? Site Index
www.dci.org.uk