1985 - 2007

 

34. Kuwekea Mikono

Ee Bwana, tujaze na Roho wako hadi kufurika

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Kum 34

Mstari Wa Kukariri
Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri (Mdo 19:6).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, kanisani kwenu kuna kuwekeana mikono? Je, hilo ni jambo la kawaida kwenu au hutukia mara chache tu kwa mfano mnapotembelewa na Askofu?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Kwa kibali cha viongozi wenu, andaeni utaratibu wa kuwekewa mikono kila mmoja wenu ili mpokee uwezo wa kuhudumu, baraka na uponyaji.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika taarifa ya kurasa mbili ukielezea ni lini kila tendo la kuwekea mikono lilifanyika na sababu zake.

Tafakari Mistari Hii Neno Kwa Neno
Kut 31: 1-6

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea nchi zilizokuwa Yugoslavia ya zamani – yaani Serbia, Montenegro,

Bosnia, Croatia, Kosovo, Macedonia, na Slovenia. Kuna mateso na matatizo ya kikabila. Kuna wafuasi wachache wa madhehebu ya Kiinjili, lakini wanaongezeka.

 

Katika Ebr 6:1,2 mwandishi anataja mambo sita ya msingi ambayo kila mwamini mchanga anapaswa kuyajua, kabla hajaendelea kuukulia wokovu.

  1. Toba
  2. Imani kwa Mungu
  3. Maagizo kuhusu mabatizo
  4. Kuwekea mikono
  5. Ufufuo kwa wafu
  6. Hukumu ya milele

Kuwekea mikono ni mojawapo, na ndiyo maana utaona mara kwa mara watu wakiwekewa mikono katika mikutano ya maombi na kanisani. Maelezo kuhusu misingi mingine utakutana nayo kadiri tunavyoendelea na mafunzo yetu.

1. Kuwekea Mikono Ni Nini?

Unaweza kusema kwamba kuwekea mikono ni huduma ya mtu mmoja kwa mwenzake inayofanyika wakati mtu mmoja anapoweka mkono wake mmoja au yote miwili juu ya mwili wa mtu mwingine kwa kusudi maalum la kiroho. Kwa kawaida mtu anayewekewa mikono atakuwa anaombewa, au kutabiriwa wakati huohuo. Wakati mwingine kikundi cha waamini kitakuwa kimemzunguka mtu mwenye hitaji na kumwekea mikono.

2. Jambo Hili Linapatikana Wapi Kwenye Biblia?

Kwa hakika , kuwekea mikono ni jambo la baraka na la zamani sana linalojulikana na watu wa Mungu. Zipo kumbukumbu za matukio hayo tangu mwanzo wa nyakati.

Kutenga Kwa Ajili Ya Kifo
Katika Agano la Kale Wana wa Israeli waliweka mikono yao juu ya vichwa vya wanyama kabla hawajachinjwa na hatimaye kuchomwa ili kuhamishia dhambi zao kwa wanyama hao wanapotolewa kafara (Kut 29:10, 15, 19, 29) (Law 1:1-5; 4:15; 8:4; 8:18, 22; 16:21; 24:14) (Hes 8:12) (2Nya 29:23).

Kuhamishia Baraka Za Kinabii
Yakobo alihamishia baraka za mwisho za kinabii kwa wajukuu zake Efraimu na Manase, kwa maombi na kwa kuwawekea mikono (Mwa 48:14).

Kumsimika Kiongozi
Musa alimwekea mikono msaidizi wake Yoshua ili kuhamishia kwake mamlaka na hekima kama kiongozi mpya wa watu wa Mungu (Kum 34:9) (Hes 27:15-23) (Yos 1:16, 17) (Hes 8:10) (Hes 27:23).

Kuhamishia Uponyaji
Y
esu alihamishia uponyaji kwa wagonjwa kwa kuwawekea mikono. Wazee wa kanisa humpaka mafuta mgonjwa, humwekea mikono yao na kumwombea uponyaji. Waamini pia wanao uwezo wa kuhamishia uponyaji kwa mgonjwa kwa kumwekea mikono (Mk 5:23; 6:5; 8:23-25; 16:18) (Lk 4:40; 13:13) (Mdo 9:12-17; 28:8, 9) (Yak 5:14-16).

Kuhamishia Baraka
Y
esu alipenda hasa kuhamishia baraka za Mungu kwa watoto wadogo (Mt 9:13-15) (Mk 10:13-16).

Kuhamishia Amani
Y
esu alimwekea Yohana mkono na kusema, “Usiogope” (Ufu 1:17).

Kuhamishia Roho Mtakatifu
Waamini kwa ujumla, na viongozi, walihusika katika kuwahamishia wengine ubatizo wa Roho Mtakatifu kwa njia ya kuwawekea mikono (Mdo 8:14-24; 9:10-17; 19:6).

Kuhamishia Karama Za Kiroho
Karama za neema kutoka kwa Yesu zilihamishwa na Roho wa Mungu kwa njia ya kuwekea mikono (1Tim 4:14) (2Tim 1:6) (Rum 1:11).

Kutenga Wamishenari
Katika Mdo 13:1-4 Paulo na Barnaba wanatengwa na kanisa kwa kazi ya umishenari kwa kuwekewa mikono, na hivyo kupokea upako maalum kwa ajili ya huduma hiyo.

Kuwaingiza Kazini Watumishi Wa Kanisa
Kuingizwa kazini kwa wale viongozi saba wa makanisa katika Mdo 6:1-6, kulihusisha pia kuwekewa mikono na mitume. Watu hao saba tayari walikuwa waamini.

3. Je, Ni Lini Mtu Awekewe Mikono?

Ni lazima pawepo na muda wa kutosha wa kumfahamu, na kila tahadhari ichukuliwe kabla ya kumwekea mikono mfanyakazi mpya wa kanisa, mchungaji au mmishenari. Kuwekea mikono ni jambo la mwisho kabisa na la hadhara katika mchakato mzima wa kufanya maamuzi mbele za Bwana. Ni wazi kwamba usingetaka kuchagua mtu mbovu, ambaye baadaye angeweza kusababisha uharibifu na mgawanyiko kanisani (1Tim 5:22).

4. Ni Nini Kinachotokea Wakati Wa Kuwekea Mikono?

Hapa hatuzungumzii kuhusu taratibu au sherehe zinazofanyika kanisani. Hizo ni sherehe za kuweka mikono mitupu juu ya vichwa vitupu. Zingekuwa ni sherehe zisizokuwa na maana na zinazokosa kibali cha Mungu. Wakati viongozi au waamini wanapomwekea mtu mikono ni kwa sababu wanataka Mungu aachilie Roho wake na neema yake kupitia mikono hiyo wakati wa huduma inayoongozwa na Roho Mtakatifu (Kum 34:9).

Uwe Mwangalifu Ni Nani Anayekuwekea Mikono
Kwa sababu uhamisho unaofanyika wakati wa kuwekea mikono ni halisi, na wenye uweza mkubwa; na kwa sababu si Roho Mtakatifu peke yake anayeweza kuhamishwa, ni lazima uchukue tahadhari ni nani unayemruhusu akuwekee mikono yake. Usimruhusu kukuwekea mikono mtu anayejihusisha na mambo ya kichawi na ushirikina, au anayetenda dhambi kwa kukusudia; kwa sababu upo uwezekano wa mtu huyo kukuhamishia pepo mchafu na akakusumbua maishani mwako.

Mwulize Mungu kimoyomoyo katika maombi, kama alivyofanya Nehemia katika Neh 2:4 na kwa haraka tathmini tabia ya mtu anayetaka kukuwekea mikono. Kama ukikosa amani, basi unaweza kwa upole kabisa kukataa kuwekewa mikono.

5. Utawekeaje Mikono?

Isingeweza kurahisishwa zaidi kwa sababu unachopaswa kukifanya ni kukubali kuwa chombo cha baraka za Mungu kwa mtu mhusika. Roho Mtakatifu atafanya mengine yote kutokana na mwitikio wako wa upendo, utayari wako na maombi yako; na utayari na uwazi wa yule mlengwa.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Iran

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Aimaq, Jamshidi (Char Aimaq)

Aimaq, Jamshidi

30,000

Aimaq, Timuri (Teymur, Timuri)

Aimaq, Taimuri

181,000

Azerbaijani (Azeri)

Azerbaijani, South

22,000,000

Balkan Rom Gypsy

Romani, Balkan

24,000

Baluch, Southern

Baluchi, Southern

405,000

Baluch, Western

Baluchi, Western

29,000

 






 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk