1985 - 2007

 

41. Kupakwa Mafuta Kwa Ajili Ya Maskini

Nendeni kwenye mitaa ya mji, na kumwalika kwenye karamu ye yote mtakayemkuta

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Isaya 61; Mathayo 22:1-14

Mstari wa Kukariri
Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa (Lk 4:18,19).

Baadaye Fanyeni Jambo Hili
Katika mji wako, ni watu gani hawa wanaozungumziwa katika Isaya 61? Andika majina yao, shughuli wanazofanya, na mahali walipo. Waombee.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Ninyi kama kikundi, fanyeni maombi pamoja mkizifunga nguvu za giza, na kuwafungua wale waliofungwa na nguvu za giza. Baada ya maombi ya kina tembeleeni eneo la mji wenu lenye makahaba wengi. Anzeni kuimba, na kisha kumhubiri Yesu. Onesheni upendo na urafiki kwa watu waliopotea na kushikiliwa na dhambi na Shetani.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Fanya mapitio ya Warumi 1:18-32 na kisha andika ukurasa mmoja ukielezea namna mwanadamu anavyoweza kuporomoka na kujikuta akiwa na hali mbaya ya maisha, kama ilivyo dhahiri katika maisha.

Tafakari Mistari Hii Neno Kwa Neno
Ezekieli 36:37,38

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Uganda. Idadi ya watu ni 22,000,000.

Asilimia 84% ni Wakristo; asilimia 8% ni Waislamu.

Kuna yatima wengi na tatizo la ukimwi

 

Katika Isaya 61:4 Kuna Ahadi Maalum

Nao watajenga mahali pa kale palipoharibiwa, watapainua mahali palipokuwa ukiwa zamani, watatengeneza miji iliyoharibiwa, mahali palipoachwa kizazi baada ya kizazi.

Sehemu nyingi za katikati ya miji ni nzuri kwa sababu fedha nyingi zimetumika kuzipendezesha ili kuwa na mazingira mazuri ya watu kufanyia kazi, na kuvutia wageni pia. Lakini kwa mamilioni ya wanaume, wanawake na watoto wanaoishi katika hiyo miji, ukweli ni tofauti kabisa. Wao wamekuja kutafuta ajira, mishahara na maisha bora; lakini wanachokutana nacho ni:

Ukosefu wa ajira, umaskini, unyonyaji, uchafuzi wa mazingira, madawa ya kulevya, uhalifu, magonjwa, fujo na vurugu. Kwao, na kwa Mungu, miji imekuwa ni maeneo ambayo maadili yameporomoka na maisha yameharibika kwa muda mrefu. Ni kwanini imekuwa hivyo?

1. Kuteleza Kuelekea Bondeni

Warumi 1:18-32, inatuambia kwamba watu wanapomsahau Mungu aliye hai na wa kweli huangukia katika mtego wa ibada ya sanamu, na huo ndio mwanzo wa utelezi kuelekea bondeni (ms 21-23).

Matokeo ya ibada ya sanamu ni utelezi mwingine kuelekea kwenye uchafu na ukosefu wa maadili mema (ms 24,25).

Kwa kuwa ukiukwaji wa maadili hauleti utoshelevu wa muda mrefu, wanaume na wanawake wanazidi kutelezea bondeni kwa kuishi na kufanya vitendo ambavyo ni kinyume na maumbile (ms 26,27).

Hatimaye utelezi unawafikisha bondeni ambako wanakuwa na maisha mabaya sana. Watu wanakosa ufahamu, hawana tena imani, hawana huruma, ni wakatili na hayo ni maisha yaliyoko katika mitaa ya ndani ya mji ambako kuna udanganyifu, chuki, mvutano, na mauaji (ms 28-32).

Habari njema ni kwamba Mungu ameahidi kwamba watajenga upya magofu na kurejesha upya maeneo yaliyoharibika.

2. Hawa Watu Ni Akina Nani?

Hapa kuna jibu la kushangaza. Hapo mwanzo walikuwa watu maskini, wanaume na wanawake waliovunjika mioyo. Walikuwa wameshikiliwa na dhambi, ubinafsi, na Shetani katika ulevi na matusi. Hapo mwanzo walikuwa wafungwa, pengine hata gerezani, na maisha yao yalikuwa ni giza tupu, kukata tamaa na huzuni kubwa.

Sasa wanapata faraja.

Sasa ni watu wazuri.

Sasa wana furaha.

Sasa wako imara, hawayumbi.

Wanaitwa ni makuhani wa Bwana,

Na watumishi wa Mungu.

Wanao utajiri wa kuwatosha.

Wanafurahia hata kipimo mara mbili.

Wanatazamia kurithi.

Uzao wao wanawabariki mataifa.

Na kila mtu awaonaye hukiri ya kwamba Mungu amewabariki. Haishangazi kuona wakishereheka na kumsifu Mungu (Isa 61:1-11).

Hayo Yalitokeaje?
Mabadilishano ya mtindo wa maisha ya namna hii ni lazima uwe mwujiza wa Mungu. Ufunguo upo katika Isa 61:1 ambapo mtu mmoja, mwokozi, anasema, “Roho wa Bwana Mungu yu juu yangu, kwa sababu Bwana amenipaka mafuta…”. Kupakwa mafuta maana yake ni kuitwa na kuwezeshwa (1Sam16:13).

3. Ni Nani Aliyempaka Bwana Mafuta?

Bwana Mungu ndiye aliyempaka mafuta Mwanaye Yesu. Lk 4:16-21 inatuambia kwamba Yesu alienda kwenye sinagogi, akasoma ahadi ya Isaya waziwazi na kutamka kwamba siku ile ndipo unabii ulipotimia. Ndipo Yesu alipoanza kuyatenda yale yote aliyokuwa ameahidi Mungu.

4. Kwanini Yesu Akapakwa Mafuta?

Ili Awe Habari Njema Kwa Watu Maskini
Mtu maskini ni yule anayejinyenyekesha mbele za Mungu na kumwomba msaada, kama yule mwenye ukoma katika Lk 5:12-15. Mtu anaweza kuwa ni tajiri lakini kama moyoni mwake analia akiomba msaada, huyo ni mtu mnyenyekevu. Mtu ombaomba asiye na cho chote anaweza kuwa na kiburi na kusema, “Achana na mimi”.

Kuleta Uhuru Kwa Waliofungwa
Wakati Paulo na Sila walipokuwa gerezani katika Mdo 16:16-40, walikuwa wakimsifu Mungu usiku wa manane. Bwana akatuma tetemeko la ardhi lililotikisa gereza, kusababisha uhuru wa Paulo na Sila, na kuleta wokovu kwa yule askari magereza. Hata leo anao uwezo wa kuwaweka huru wafungwa wa madawa ya kulevya na magonjwa.

Kuwapa Vipofu Uwezo Wa Kuona
Baadhi ya watu ni vipofu wa macho ya kimwili, lakini walio wengi hawawezi kuuingia wala kuuona Ufalme wa Mungu kwa sababu wana upofu wa macho ya kiroho. Yesu alisema hawa wanapaswa kuzaliwa mara ya pili (Yn 3:3,5).

Kuwaweka Huru Wanaokandamizwa
Yesu ndiye anayewaweka huru watu wanaosumbuliwa na mapepo yanayowatesa kwa njia ya hofu, hasira, chuki, kukataliwa, kujihurumia, kushindwa, na maono na sauti za usiku.

Kutangaza Mwaka Wa Bwana Uliokubalika
Hao watu wa mitaani waliokuwa maskini sana, waliokuwa wamevunjika moyo na kushikiliwa na dhambi walikutana na Yesu na kugundua kwamba hadi leo hii anaendelea kuwarejeshea uzima, afya njema, na tumaini; na kuwapa heshima na maisha yenye malengo. Na baraka zinaendelea.

5. Mungu Huwapaka Mafuta Watu Wa Mitaani Pia

Yesu alisema kwamba huyo Roho wa Bwana atakapokuja mtapokea uwezo wa kuwaambia watu kwamba Yesu yu hai leo, na kufanya miujiza (Mdo 1:8).

Yesu alisema kwamba kama mtu akimwamini ataweza kutenda zile kazi alizokuwa akizitenda Yesu, na hata kubwa kuliko hizo (Yn 14:12).

Yesu alisema kwamba kama Baba alivyomtuma kuokoa watu wanaume na wanawake katika ulimwengu uliozidiwa na dhambi na kujawa na mapepo wachafu, vivyo hivyo anawatuma wafuasi wake kuiendeleza hiyo kazi ya wokovu. Kwahiyo wale watu ambao hapo kwanza walikuwa mitaani, sasa wanafanya kazi ya kuokoa. Ndio hao ambao Yesu alipakwa mafuta kwa ajili yao, akawajia, akawabadilisha, akawapaka mafuta, na kuwatuma kwenda kujenga upya na kurejeshea uzima watu walioharibiwa na dhambi, magonjwa, na Shetani.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina.

Kazakhstan

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Chechen, Shishan

Chechen

52,000

Kurd, Northern (Kermanji)

Kermanji (Kurmanji)

27,000

Parsee

Parsi (Parsee)

110,000





 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk