1985 - 2007

 

42. Saumu Ya Kweli

Je, siku hizi ni mfungo au ni karamu?

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Isaya 58; Mathayo 6:16-18

Mstari Wa Kukariri
Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga (Mt 17:21).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Ni njia zipi zinazotumika kutekeleza mfungo aliouchagua Mungu nchini mwako? Ni nini kingine kinachoweza kufanyika mbali na sala?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Tafakari kitabu cha Yoeli mlango wa 1 na 2 ili ugundue chanzo cha tishio. Soma mstari kwa mstari uone ushauri alioutoa Bwana katika mlango wa kwanza ms 13 na 14, na mlango wa pili ms 12-17. Jaribu kuchora picha kwenye mawazo yako ili uone utekelezaji wake unaweza kuwa namna gani kivitendo. Je, matukio kama hayo yanaweza kutokea katika siku zetu; na kwa namna gani?

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika taarifa za matukio baada ya mfungo uliotajwa katika 2Nya 20:3.

Tafakari Mistari Hii Neno Kwa Neno
Mathayo 6:16-18

Tumia Muda Mfupi Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Hispania. Idadi yao ni 40,000,000. Kanisa limeteswa kwa muda mrefu.

Asilimia 1% ni Waprotestanti; asilimia 27% ni Wakatoliki; na asilimia 60% ya ukuaji wa kanisa ni kabila la Waromani!

 

Ingawa somo hili linalenga kwenye kile Mungu anachokiita mfungo aliouchagua yeye, yaani saumu ya kweli, lakini tutaanza kwa kuangalia mfungo wa kawaida, yaani kusitisha chakula na wakati mwingine hata maji, kwa kusudi maalum.

Kwanini Mtu Afunge?

Kufunga kunauambia mwili, tumbo na hamu ya chakula kwamba roho zetu ndizo zinazohusika na uzima; na kwa kuutumia ule muda wa kula tunaweza kumkaribia Mungu. Wakati mfungo ukiwa umeagizwa na Mungu, huleta uwezo mkubwa sana wa kiroho (Mt 17:21). Madaktari wengi pia wanajua kwamba mifungo ya mara kwa mara huuweka mwili katika hali nzuri.

1. Hivi Ni Kweli Tunalazimika Kufunga?

Katika Mt 6:16-18 Yesu anachukulia kwamba wafuasi wake watafunga mara kwa mara. Anasema, ‘mtakapofunga’ na wala sio, ‘kama mkifunga’. Mfungo ni jambo linaloonekana katika mtindo wa maisha ya Kimungu tangu zamani za kale.

Mfungo Unatakiwa Uwe Na Sababu Sahihi

Mfungo hautamlazimisha Mungu kukusaidia wewe.

Mfungo hautakusaidia katika njia zako mwenyewe, vinginevyo ni mgomo wa chakula!

2. Je, Tufunge Wakati Gani?

Katika Biblia zipo nyakati ambapo watu walifunga, ama mmoja peke yake, au kwa pamoja.

1       Waliposikia kuhusu taarifa mbaya (Neh 1:4) (2Sam 1:12).

2       Wakati kuna wagonjwa (2Sam 12:16) (Zab 35:13).

3       Wakati wa msiba (1Sam 31:13) (2Sam 3:35).

4       Wakati wa hatari, (Esta 4:16) (Dan 6:18) (Mdo 27:33, 34).

5       Wakati wa tishio la janga la kitaifa, (Amu 20:26) (2Nya 20:3) (Yoeli 1:14; 2:12-15).

6       Wakati wa tishio la hukumu, (Yer 36:9) (Yona 3:5-10).

7       Kabla ya safari, (Ezra 8:21-23).

8       Wakati wa maungamo ya hadhara ya dhambi (Neh 9:1, 2) (1Sam 7:6).

9       Wakati wa toba ya binafsi, (1 Fal 21:27-29) (Ezra 10:6).

10  Wakati wa maombezi, (Dan 9:3).

11  Wakati wa kushughulikia ufunuo kutoka kwa Mungu (Dan 10:1-3) (Mdo 9:9).

12  Wakati wa kuwasimika au kuwatuma watumishi, (Mdo 13:3; 14:23).

 

Wakati Wa Mfungo Tunapaswa Kufanya Nini?

Tunapaswa kuomba, (Dan 9:3) (Yer 14:12).

Tunapaswa kunyenyekea, (Kum 9:18) (Neh 9:1)

Tunapaswa kusoma Maandiko, (Yer 36:6).

 

Aina Mbalimbali Za Kufunga

Kwa kuanzia unaweza ukaacha mlo mmoja kwa ajili ya kufanya maombi, au unaweza kufunga kuanzia jioni hadi jioni inayofuata. Katika mazingira yasiyokuwa ya kawaida Musa, Elia na Yesu wote walifunga kwa siku 40 kila mmoja (Kut 24:18) (1Fal 19:8) (Mt 4:1,2). Kwa kawaida unapaswa kupata kinywaji kwa wingi, na ni kwa nadra sana utafunga hata kunywa maji. Unaweza pia kufunga kula vyakula vitamu na vya anasa; kama alivyofanya Danieli kwa wiki tatu (Dan 10:2,3). Yafaa pia kufanya mifungo ya mara kwa mara ya vitu kama TV, michezo, na mahusiano ya ndoa ili kupata fursa ya kumkaribia Mungu zaidi (1Kor 7:5). Na kama ilivyokuwa kwa Daudi, wanafunzi wa Yohana, Anna, Paulo, na Kornelio, baadhi ya watu wamefanya kufunga kuwa mtindo wa maisha.

 

Soma (Zab 109:24) (Zab 69:10) (Mt 9:14) (Lk 2:37) (Mdo 10:30) (Mdo 13:3) (Mdo 14:23) (2Kor 11:27).

3. Saumu Aliyoichagua Mungu

Itakuwa vema kwetu kufunga mara kwa mara na kama Roho Mtakatifu atakavyoelekeza. Lakini kuna aina nyingine ya mfungo wenye nguvu sana. Tunaweza kuuita mfungo wa kuishi maisha ya kufunga.

Si Kila Mfungo Unampendeza Bwana
Katika Zek 7:5,6 Bwana anawahoji watu na makuhani kama kweli wanafunga kwa ajili yake, au wana ajenda nyingine! Saumu iliyotajwa katika Isa 58:1-5 hakika haikumpendeza Mungu. Hata siku ya kufunga kwao mbele za Mungu, watu waliendelea kuwanyonya watumishi wao, waliendelea na ugomvi na mapigano miongoni mwao, waliendelea na unafiki wao, walijaribu kumlazimisha Mungu kukubaliana na matakwa yao, huku wakilalamika na kuziacha amri za Mungu. Anasema, “Msitazamie kusikizwa kutoka juu!”.

4. Ni Saumu Gani Basi Inayompendeza Mungu?

Mungu anasema katika Isa 58:6 -12, "Je, saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii?...” na kisha anaipendekeza kwetu. Aina hiyo ya saumu haihusiani sana na suala la kujinyima tu chakula kwa muda, lakini ni suala la kujikana mwenyewe na kumwishia Mungu. Na hilo si jambo la siku moja, bali ni la kudumu, la maisha yote.

Anataka Tujikane Wenyewe Na Kisha:
Kufungua vifungo vya uovu,

Kuzilegeza kamba za nira,

Kukutana na mahitaji ya wanaokandamizwa.

Kuvunja kila nira,

Kuwagawia wenye njaa chakula chako.

Kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani mwako,

Umwonapo aliye uchi, umvike nguo.

Msaidie mwenye damu moja nawe.

Ondoa nira, isiwepo kati yako.

Usinyooshe vidole, wala kunena maovu.

Aina hii ya saumu huubadilisha ulimwengu lakini kuna hitaji kubwa la kiroho, msisimko na mali; lakini jionee mwenyewe ahadi za miujiza ya Mungu kwa ajili ya wale wote wanaothubutu kujikana wenyewe na kuishi kwa ajili ya maskini na wale wanaokandamizwa.

Nuru yako itapambazuka kama asubuhi.

Uponyaji wako utatokea mara.

Haki yako itakutangulia.

Utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.

Utakapoita, Bwana atakuitikia.

 

Utakapolia kuhitaji msaada, atasema, Mimi hapa.

Nuru yako itapambazuka gizani.

Na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.

Naye Bwana atakuongoza daima.

 

Atakutana na mahitaji yako.

Ataitia nguvu mifupa yako.

Utakuwa kama bustani iliyotiwa maji.

Utakuwa kama chemchem ambayo maji yake hayapungui.

Watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa.

Utaiinua misingi ya vizazi vingi.

 

Soma pia Zek 7:8; 8:16-19

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Kyrgyzstan

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Azerbaijani

Azerbaijani, Kaskazini

17,000

Azerbaijani

Azerbaijani, Kusini

16,000

Waturuki

Kituruki

22,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk