1985 - 2007

 

43. Watendakazi Wa Saa Ya Kumi-Na-Moja

Nawe pia nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Mathayo 20

Mstari wa Kukariri
Nitayainua macho yangu niitazame milima; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika Bwana, aliyezifanya mbingu na nchi (Zab 121:1,2).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Utakubali kuwa mtenda kazi wa saa ya kumi-na-moja? Kama Mungu amekuita uende kwenye shamba lake na wewe usijue fedha zitakavyopatikana, je, utathubutu kwenda?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Andika mchezo wa kuigiza kumhusu Lazaro na yule tajiri, kisha muone kama mnaweza kuufanyia mazoezi halafu muuoneshe kwenye makanisa. Igizo lenyewe lilenge pia kupinga tabia ya ombaomba miongoni mwa Wakristo.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Zungumza na wachungaji na wainjilisti mbalimbali na uwaombe wakupe habari zao kuhusu uaminifu wa Mungu kwao. Andika taarifa ya kurasa mbili.

Tafakari Mstari Huu Neno Kwa Neno
Lk 15:31

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Ethiopia. Idadi ya watu ni 53,000,000. Watu wake wamepata madhara ya njaa, vita, na siasa za Umaksi.

Ni moja ya mataifa ya zamani sana; Ukristo umekuwepo tangu karne ya 4; na sasa Wakristo ni asilimia 58%.  

 

1. Kwanini Wawepo Watenda Kazi Wa Saa Kumi-Na-Moja?

Katika Mt 20:1-15 ndipo ulipo mfano uliotolewa na Yesu kuwahusu watendakazi walioajiriwa katika nyakati mbalimbali za siku. Baadhi waliajiriwa tangu alfajiri, na wengine baadaye na wote waliahidiwa ujira wao. Lakini wale walioajiriwa saa kumi-na-moja, mwisho wa siku, waliambiwa tu, nendeni mkafanye kazi, bila kuahidiwa ujira wo wote. Walitumaini tu kwamba bwana wao angewafikiria.

Mungu Yuko Radhi Kufadhili
Yule bwana anasema, “mimi ni mkarimu”, (Mt 20:15) ikionesha asili ya kweli ya Baba yetu wa Mbinguni. Katika mfano wa mwana mpotevu, (Lk 15:11-31), wakati kaka yake alipoonesha kuwa na uchungu na msimamo mkali (ms 28-30) baba yao anaonesha moyo wa ukarimu wa Mungu (ms 31).

Kwa mujibu wa saa ya kinabii ya Mungu ni saa 5.55 usiku na saa 6.00 Bwana Yesu anarejea. Kwahiyo watendakazi wa saa kumi-na-moja walioitwa na Mungu kwa mavuno ya mwisho hawataahidiwa ujira lakini pia hatakuwepo atakayejuta. Usijali hata kama hujui la kufanya. Unaweza kujifunza kwa wengine kwa sababu wengi wametembea kwenye njia hii ya imani yenye umri wa miaka 2000 na Mungu ana uzoefu mkubwa wa kuwawezesha watu wake kufanya sasa mambo yaliyofanywa zamani (Mhu 1:9).

2. Mtendakazi Wa Saa Kumi-Na-Moja Anaishije?

Ni gharama kubwa sana kuishi katika ulimwengu huu, lakini kuishi si tatizo. Kwa viwango vya Mungu ni kwamba sisi tumepewa vya kututosha na ziada kubwa kwa ajili ya kuwagawia na wengine (2Kor 9:8-11). Inawezekana na hapa unaweza kuchagua miongoni mwa mambo maarufu:

Waweza Kufuata Mfano Ulio Bora
Kimsingi mambo yako hivi, “Kanisa langu linanipa kila kitu ninachohitaji ili niweze kwenda”. Huo ndio utaratibu wa nchi za Magharibi wa kuwalipa viongozi wa kanisa na kuwategemeza wamishenari. Kazi yao imegusa zaidi ya nusu ya ulimwengu wote katika kipindi cha miaka 200 iliyopita na tunamshukuru Mungu kwa ajili ya makanisa yaliyofanikisha jambo hilo.

Lakini kuna tatizo kubwa kwa sababu utaratibu huu hauwezekani kwa mengi ya makanisa yaliyoko katika nchi zinazoendelea. Wanao watendakazi wa kutosha, kinachokosekana ni fedha kwa ajili ya kuwalipa wainjilisti, wachungaji na wamishenari, ambao wako tayari kutumika.

Kwahiyo si kila mtu anayetazamia kwamba anaweza kutumwa na kulipwa. Kwa vyo vyote si rahisi kuweza kuwalipa watu wote walio tayari kumtumikia Bwana katika nchi zinazoendelea. Ni nini kingine wanachoweza kufanya?

Njia Mbadala: Mfano Wa Lazaro

Lazaro katika Lk 16:19-22 alikuwa ombaomba aliyekuwa na majeraha na vidonda kila mahali na alitumia muda mrefu kila siku kumwangalia yule tajiri akitoka nje. Sasa Lazaro alimwamini Mungu ndio maana alipokufa alichukuliwa moja kwa moja kifuani kwa Ibrahimu, lakini yule tajiri hakumwamini Mungu na alipokufa alikwenda kuzimu.

 

Je, Maskini Wanapata Nini?

Michubuko na vidonda kutokana na kupuuzwa kusiko haki. Ni watu waliodharaulika, na watu wanakwepesha macho yao wasionane. Na mara nyingi ombaomba wanapata sarafu chache za fedha wanazorushiwa na wapita njia.

 

Je, Inafaa Kuwa Hivyo Kweli?

Wachungaji wengi katika nchi zinazoendelea nao wameamua kuutumia utaratibu wa Lazaro wa kukusanya fedha. Huandika barua kwa watu wa  nchi za Magharibi wakijaribu kusimulia hadithi ya kusikitisha na kutuma picha za kutia uzito katika madai yao. Picha inayoonekana katika hali hiyo ni Yesu akiwa amenyoosha mikono ya kuomba badala ya mikono ya kukomboa ulimwengu wa watu walio katika uhitaji mkubwa. Yesu wao anaweza kuokoa ulimwengu lakini hana uwezo wa kumpatia chakula mtumishi wake mmoja.

 

Siku Moja Yule Maskini Alikufa

Hii ni kwa mujibu wa Lk 16:22. Ikiwa hata sasa yu hai moyoni mwako, tafadhali mrudishe kaburini kwake anakostahili kuwa, leo!

Je, unaweza kuona kosa la makusudi katika mstari huu kwenye Zaburi ya 121? Inashangaza sana kuona watu wengi wakiisoma hivi:

"Nitayainua macho yangu niitazame milima,

Msaada wangu utatoka wapi?

Msaada wangu unatokea nchi za Magharibi,

Wanaozimiliki mbingu na nchi"

Je, umeliona kosa? Msaada wetu hutoka kwa Bwana peke yake. Kwahiyo ondoa macho yako kutoka nchi za Magharibi, na kutoka mahali pengine po pote, na macho yote yamwangalie Yesu ambaye msaada wetu unatoka kwake. Kwa vyo vyote hakuna hata moja kati ya hadithi zako inayoweza kuwafanya watu wa Magharibi wakusaidie; lakini neno moja kutoka kwa Yesu litakusaidia.

3. Mtumishi Wa Mshahara

Unaweza kukutana na mtu huyu katika Yn 10:11-15. Mtu huyu anafanya kazi ya mchungaji kwa sababu ya fedha na zaka, si kwa sababu anawajali kondoo. Yeye si mchungaji wa kweli kwa sababu wakati mbwa-mwitu wa hali mbaya anapotokea yeye hukimbia na kuwaacha kondoo waangamie. Makanisa mengi mazuri yameharibiwa na watu kama hao.

Jiunge Nasi Tutakununulia Pikipiki!
Baadhi ya makanisa makubwa wanaweza kuwashawishi wachungaji wa makanisa ya vijijini kujiunga nao kwa ajili ya fedha. Ni mchungaji wa mshahara pekee anayeweza kukabidhi kundi lake kwa mtu mwingine, kwahiyo atakapokujia mtu na wazo kama hilo, mwambie kwamba wewe si wa kuuza. Ulimwenguni hapa hakuna fedha ya kutosha kumnunua mtu wa kweli wa Mungu.

4. Je, Utapata Wapi Fedha?

Tutazungumzia jambo hili kwa undani zaidi baadaye kidogo, lakini hapa pana kanuni moja muhimu ya kujifunza kwa moyo. Katika Yn 5:1-9 utakutana na mtu mmoja aliyekuwa dhaifu na asiye na thamani kwa muda mrefu. Alipoulizwa swali, alitoa sababu tatu kusema kwamba hawezi kufanya lo lote au kwenda ko kote-

1       Sina mtu wa kunisaidia.

2       Ninajaribu, lakini

3       Mtu mwingine hunitangulia na kuipata hiyo baraka.

Ilikuwa ni kweli kwake, na inaweza ikawa kweli kwako pia, na ni kweli kwa watu wengine wengi pia, lakini kama ilivyokuwa kwake, wewe pia unaye Yesu anayezungumza nawe. Yeye alimsikia Bwana, akatii, akainuka na kutembea kuelekea kwenye maisha ya maana kwa neema ya Mungu.

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Laos

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Hani

Hani

30,000

Lor

Lor

10,000

Pacoh (Bo)

Pacoh

21,000

Shan (Thai Yai)

Shan

24,000

Sila

Sila

22,000

Tai, White (Thai Trang)

Tai Don

38,000

Thai Nung

Nung 2

47,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk