1985 - 2007

 

46. Kutoka Kwenye Njaa Kali Hadi Kwenye Baraka Tele

Katika nchi yenye jua kali na njaa kwanini Mungu alimpelekea Isaka maji?

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Mwanzo 26

Mstari wa Kukariri
Jilindeni, kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe (Lk 17:3).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Yesu ana maana gani anaposema kwamba “ni heri kutoa kuliko kupokea”?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Kwa msaada wa Mungu, chunguza moyo wako na maisha yako ya zamani ili uweze kuwagundua adui zako. Katika nuru ya somo hili, na hitaji lako la baraka za Mungu na mafanikio, unapaswa kufanya nini, tena kwa msaada wake? Ufanye hivyo kwa kwenda mwenyewe au kwa njia ya barua kabla hatujakutana tena.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika taarifa ya ukurasa mmoja ukielezea habari za Isaka wa kisasa unayemfahamu au uliyesoma habari zake. Mtu aliyeishi maisha yasiyo ya ubinafsi, akiwabariki wengine wasio na kitu.

Tafakari Mistari Hii
Mt 5:43-48

Tumia Muda Mfupi Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Syria. Idadi ya watu ni 15,000,000. Wakristo wapo tangu enzi za Antiokia. Asilimia 90% ni Waislamu, na asilimia 0.1% ni wafuasi wa madhehebu ya Kiinjili.

 

Tunakwenda kuangalia habari za mmoja wa watu wakuu wa Agano la Kale aitwaye Isaka, kutoka Mwa 26:1-33. Tutaona namna Isaka alivyoweza kuachana na maisha yaliyojawa na ukame, njaa na hali mbaya ya kiuchumi; na kuingia kwenye maisha ya neema. Alipata vingi vya kumtosha yeye na ziada kubwa ikawa baraka kwa mji mzima.

Ni Baraka Zaidi Kutoa Kuliko Kupokea

Kibiblia mafanikio si wewe kuwa tajiri, ila kupata vya kukutosha, na ziada kubwa kwa ajili ya kuchangia shughuli za kueneza Injili, na pia kuwagawia maskini. Na hili ndilo lililokuwa lengo la Paulo katika 2Kor 9:8 na ufafanuzi mzuri alioutoa katika mlango wa 8 na wa 9. Yesu hakuja kutumikiwa bali kutumika na kuutoa uhai wake. Alisema, “Heri kutoa kuliko kupokea” (Mk 10:45) (Mdo 20:35).

Hapa Wapo Akina Isaka Wa Kileo:
George Muller - aliyepokea kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya maelfu ya watoto yatima.
Dk. Dowie - alijenga mji ulioitwa Sayuni kuwa makazi yake na ya maelfu ya watu.
William Booth - alitumia imani yake kuwasaidia maelfu ya Waingereza maskini katika karne ya 19.
Mhispania Miguel Diez - analisha maelfu ya watu na watoto wa mitaani nchini Hispania, na katika nchi nyingine 45.

Njaa Katika Nchi
Katika Mwa 26:1 tunaambiwa kwamba kulikuwa na njaa katika nchi. Njaa huletwa na ukame, na kusababisha uhitaji mkubwa sana wa chakula, magonjwa na hali ya kukosekana kwa utulivu ndani ya nchi. Nchi nyingi zinazoendelea zina tatizo la njaa la mara kwa mara. Isaka alitaka kukimbilia Misri, lakini Bwana alimtokea na kuzungumza naye. Je, alistahimili vipi ile njaa?

Isaka Alilisikia Neno La Bwana

Kwanza alimtii Mungu na kuweka imani yake katika neno la Mungu. Badala ya kula mbegu kidogo iliyokuwa imebakia, aliipanda katika ardhi iliyokuwa kame. Kwa sababu ya kumtii Mungu kwa kufanya kitu kisichotazamiwa, na mahali pasipotazamiwa; katika kipindi cha mwaka mmoja tu Isaka alivuna mara mia moja na akaanza kustawi. Kwa masikitiko makubwa, si kila mtu anafurahia unapobarikiwa. Wafilisti walimwonea wivu Isaka kwa mafanikio aliyoyapata kutoka kwa Mungu, na kufukia visima vyake vya maji kwa udongo na mawe. Na mfalme wao akamwamuru aondoke (Mwa 26:12-16).

Isaka Alikataa Kushindwa Na Udhaifu Wake Binafsi

Hata watu wakuu wa Mungu nao hawakosi mapungufu yao. Isaka alifanya kosa lilelile alilolifanya baba yake Ibrahimu. Isaka aliwaogopa Wafilisti na kusema uongo kumhusu mke wake. Mungu alihakikisha amekamatwa, amedhalilishwa na kuaibishwa kwa dhambi yake (Mwa 26:7-11).

Tunajua tu kwamba alitubu kwa sababu Mungu hamsikii mtu anayeficha dhambi bila kuitubia, na baadaye Isaka alibarikiwa. Alikataa kushindwa na mapungufu yake na udhaifu wake la sivyo kamwe asingefika katika nchi ya ahadi yake. Kama ukianguka njia pekee ya kukuwezesha kusonga mbele ni katika uaminifu, unyenyekevu, ungamo na msamaha (Zab 66:18) (1Yoh 1:8, 9) (Mit 24:16) (Mika 7:7-9).

Isaka Alivitengeneza Visima Vya Ibrahimu

Vile visima vilifukiwa na Wafilisti baada ya kifo cha Ibrahimu. Ibrahimu alikuwa amefanya kazi ngumu ya kuchimba visima hivyo kwa jasho katika joto kali (Mwa 26:18).

Je, Ni Akina Nani Wafilisti Wa Leo?

Kiroho, ni nguvu za giza.

 

Je, Visima Vya Ibrahimu Leo Ni Nini? Miaka mingi iliyopita mababu zetu katika Imani walichimba visima vya kiroho kwa kazi ngumu, kwa kuumia na kwa jasho ili kulijenga kanisa. Kwa sababu ya kupuuza kwetu na uzembe, nguvu za giza zimekuja na kufukia hivyo visima. Baadhi ya visima vya imani vya Ibrahimu ambavyo ni lazima vifukuliwe katika siku zetu ni:

 

Visima vya kumwamini Mungu, (Mwa 15: 4-6).

Visima vya maombezi, (Mwa 18: 20-33). Visima vya sadaka, (Mwa 22: 1-14). Visima vya kurejesha mateka, (Mwa 14:14-16).

Isaka Anakuwa Mstahimilivu Katika Upinzani

Kuna kutokuelewana na uadui kuhusu haki ya kutumia maji Eseki na ugomvi unatokea tena Sitna (Mwa 26:19-22). Kama Isaka angeng’ang’ania kudai haki, ungemkuta hata leo yuko palepale akidai haki; lakini aliondoka. Hatimaye Isaka anachimba kisima kingine Rehobothi, na safari hii hakuna anayempinga. Jambo hilo linamtia moyo naye anatabiri,”Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi”. Usiku ule Bwana akamtokea na kulithibitisha lile neno la unabii (Mwa 26:22-24).

Hatua Ya Mwisho Ya Kuachiliwa Baraka
Unakumbuka jinsi Wafilisti walivyomfanyia visa Isaka? Sasa mfalme wao, na mshauri wake, na mkuu wa majeshi, wanakuja kumtembelea. Safari hii hawakumtishia Isaka na badala yake wanakuja na uongo wa kushangaza na visingizio kwa tabia yao walioionesha kwanza. Eti sasa wanataka mkataba wa amani! (Mwa 26:26-30). Je, ungekuwa ni wewe ungewafanyaje maadui hawa ambao wamesababisha uharibifu mkubwa na maumivu tele?

Isaka Aliwapokea Vizuri Adui Zake

Isaka alionesha roho ya Kristo ambaye angetokea miaka elfu nyingi baadaye. Isaka akachagua kuwafanyia wema kwa kuwaandalia chakula cha urafiki na kuingia nao mkataba wa amani. Hapakuwa na ugomvi wala maneno makali (Mwa 26:3-31) (Mt 5:43-48; 6:14) (Lk 17:3-5). Mpende adui yako, la sivyo ataendelea kuwa adui yako. Upendo unaweza kusababisha ukampata.

Watumwa Wa Isaka Walipata Maji

Kwa Mungu mambo hayatokei tu kwa bahati! Siku ileile Isaka alipowasamehe adui zake baraka za Mungu ziliachiliwa kwa wingi. Wakapata maji ya kutosha visima saba, ya kutosha kumwagilia mashamba yao, ya kutosha kunyweshea mifugo yao, na ziada kubwa kwa ajili ya kuubariki mji wenye watu wengi. Akauita jina lake Beersheba, maana yake visima saba. Isaka alipokea baraka kwa ajili yake na wengine kwa kulisikia neno la Mungu na kwa kuwa mstahimilivu katika mapungufu, katika kazi ngumu, katika uadui, na katika kuwatendea mema adui zake. Maji yale bila shaka yalikuwa matamu sana!

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

 

 Malaysia

 

 

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Sama, Southern (Bajau)

Sama, Sibutu

20,000

Sinama, Northern

Sama, Balangingi

30,000

Tausug (Sulu, Suluk)

Tausug

110,000

Temuan

Temuan

10,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk