1985 - 2007

 

50. Kwanza Mfuasi

Ili kumwona Yesu unalazimika kuwa pale alipo

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Yohana 12

Mstari Wa Kukariri
“…Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayeipoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona” (Mt 16:24,25).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, umewahi kumwomba Mungu jambo na ukapata jibu tofauti kabisa? Hebu sasa mjulishane ni nini alichojibu Mungu.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Andika orodha ya mali zako zote; kisha ilete na kuiweka madhabahuni mbele za Bwana wakati wa maombi kama ishara ya hadhara ya kukabidhi umiliki wa mali hizo.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika maelezo ya ukurasa mmoja ukifafanua maana ya mwamini kuubeba msalaba wake katika siku zetu. Toa na mifano.

Tafakari Mistari Hii Neno Kwa Neno
Lk 24:30,31

Tumia Muda Mfupi Kuubadilisha Ulimwengu

Waombee Mbilikimo walioko katika eneo la dunia liitwalo Aktiki. Idadi yao ni 32,000.

Wanateseka kutokana na mfumo wa maisha wa nchi za Magharibi. Wengi wao wameokoka kuanzia mwaka 1982.

 

Njia bora ya kumwona Yesu ni kuwa pamoja naye, hivyo utaweza kumwona na kumsikia vizuri (Lk 8:1). Wale waliomfuata Yesu aliwaita wanafunzi, neno lenye maana ya watu wanaojifunza. Somo hili linapatikana katika Yn 12:19-33 na linahusiana na gharama za kuwa mfuasi wa Yesu, gharama ambazo hazihusiani na fedha.

Ulimwengu Mzima Unamfuata Yeye

Baadhi wa watu kutoka Ugiriki walimjia Filipo, mmoja wa wanafunzi wa Yesu, ambaye naye pia alikuwa Mgiriki, wakitaka kumwona Yesu. Filipo aliwasiliana na ndugu yake Andrea na kwa pamoja wakamwendea Yesu ili kumwomba apate kukutana na rafiki zao wapya (Yn 12:21).

Bila shaka Yesu angependezwa na ombi hilo kwa sababu muda mfupi uliopita alikuwa amesema,”Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta, na sauti yangu wataisikia, …”. Yawezekana kwamba Magiriki hawa ndio wa kwanza kumjia Yesu kutoka mataifa ya kigeni.

Tunataka Kumwona Yesu
Je, umeshagundua kwamba wakati mwingine Yesu hutoa majibu yasiyotazamiwa kwa maswali na maombi yetu? Majibu yake yanashughulika na masuala halisi, ambayo si lazima yawe yale tuyaombayo! Tungetazamia jibu kama vile, ‘saa 9 kamili’ au ‘kesho saa 4 asubuhi’. Lakini jibu alilolitoa, tukilielewa vizuri, litatuelekeza sisi jinsi ya kumwona Yesu na kumjua kwa undani. Je, alisema nini? (Yn 12:23-28).

Saa Imewadia
Ikiwa na maana ya ndiyo, ni wakati wa wanadamu kuuona utukufu wa Mwana wa Mungu. Bado muda ungalipo, na sasa ni muda mzuri kuliko mwingine wo wote.

Ni Lazima Ufe
Maneno hayo yanatisha, lakini Yesu hakumaanisha kifo cha kimwili. Mbegu ya ngano isipofukiwa chini haiwezi kukua na kuzaa. Ni lazima izikwe, ipoteze ganda lake la nje, na kwa wakati muafaka itajitokeza tena ikiwa na uzima mpya na uwezo wa kuzaa matunda mengi. Vivyo hivyo kwa maisha yetu na asili ya zamani. Ni lazima utu wa kale ufe na ubinafsi wake na tamaa zake, uzikwe pamoja na Kristo na kufufuka tena, na kuzaliwa mara ya pili katika maisha mapya. Unapokuwa umezaliwa mara ya pili, kiroho unaweza kumwona Yesu vizuri (Yn 3:3) (Rum 6:1-14).

Mfuasi Pia Anapaswa Kufa Kila Siku

Kikwazo kikubwa cha kumwona Yesu mara zote ni ubinafsi, yaani kufanya mambo yetu wenyewe, kwa namna yetu wenyewe, na pengine hata kwa kutumia jina la Yesu. Je, mfuasi afe namna gani? Yesu anasema hivi:

Kwa Kutokujipenda Mwenyewe
Maana yake ni kwamba hatutakiwi kujipigia debe wenyewe wala mipango yetu, kama alivyofanya Kora na kumezwa na nchi iliyokuwa chini yake wakati Mungu alipoiruhusu kufunua kinywa chake (Hes 16:32).

Maana yake hakuna kupigana ili kuifanikisha njia yako mwenyewe kama alivyofanya Musa kabla Mungu hajamfundisha njia iliyo bora, lakini hiyo ilimchukua miaka 40 nyikani (Kut 2:12).

Maana yake hakuna kumsaidia Mungu katika kutimiza ahadi zake, kama alivyofanya Abramu na Sara na maamuzi yao yakasababisha kuzaliwa kwa Ishmaeli baba wa Uislamu. Gharama ya kukosa subira ambayo tunailipa hata leo (Mwanzo 16).

Kwa Kuyachukia Maisha Yake
Yesu kamwe hakuwa na maana kwamba tuyachukie maisha mapya tuliyopokea kutoka kwa Mungu, bali tuyachukie maisha yetu ulimwenguni humu. Maisha yaliyopo ulimwenguni ni kula na kunywa na kufurahi maana kesho tutakufa na ndiyo mwisho wa kila kitu. Ulimwengu unasema waziwazi – kunywa, jaribu madawa ya kulevya, fanya ngono, na maisha ya ubinafsi. Haishangazi kwamba Yesu alisema tufe kwa habari ya mambo hayo. Sema hapana. Yachukie.

Mwanafunzi Ni Lazima Amfuate Yesu
Kuwa na Yesu maana yake ni kugundua mahali alipo na kisha kuzishika amri zake. Tunasoma kutoka Lk 14:25-33 kwamba mwanafunzi ni sharti:

Ampende Yesu Kuliko Mtu Mwingine Ye Yote
Kuliko hata baba, mama, mke na familia. Ikiwa kwa mfano baba atakushawishi kuiabudu sanamu ya familia, wewe sema, ‘Hapana, nampenda Yesu’. Na iwapo shemeji yako atakualika kwenda kucheza kamari, sema, ‘Hapana, mimi nampenda Yesu’ (Lk 14:26).

Aubebe Msalaba Wake
Hapo ni kuchukua mzigo na mateso unayoweza kuyapata kutokana na uamuzi wako wa kumtii Mungu, kama alivyofanya Yesu (Lk 14:27).

Aache Vyote Alivyonavyo
Maana yake ni kwamba yote uliyodhani ni mali yako, kwa kweli ni ya Mungu, kwa matumizi yake na kwa matumizi ya ndugu zako kama Mungu anavyoelekeza (Lk 14:33). Na mara zote mwanafunzi atataka awepo mahali Yesu alipo, si katika kuomba kukombolewa na mateso, majaribu na kifo, bali kuomba utukufu wa Mungu (Yn 12:26,27).

Mungu Akasema, “Ndiyo, Sawa Kabisa”

Baba alipendezwa sana na maneno aliyokuwa akiyasema Mwana wake na akasema kutoka mbinguni akiuthibitisha ujumbe wa Yesu. Wasioamini walisema ilikuwa ni radi, na watu wa dini wakasema aliyesema alikuwa ni malaika; lakini Yesu akasema hiyo ni sauti ya Mungu (Yn 12:29,30).

Kisha Yesu Akatabiri

Kwanza, hukumu ijayo na kushindwa kwa Shetani, ambapo watu aliowashikilia watakombolewa (Yn 12:31). Halafu, kifo chake mwenyewe, na makusudi yatakayotimizwa Msalabani, na hivyo kufungua mlango wa kumwendea Mungu ili kwamba wale wote wanaotaka kumwona Yesu waweze kumwona na kumjua wenyewe (Yn 12:32,33).

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Myanmar (Burma)

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Chaungtha

Chaungtha

121,700

Danau

Danau

10,000

Hani

Hani

180,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk