1985 - 2007

 

51. Wito Wa Mungu

Jimmy Carter alifuata wito wa Mungu na akawa Rais wa Marekani

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Warumi 12 na 1Samweli 3

Mstari wa Kukariri
Akawaambia, “Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu”. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata (Mt 4:19,20).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Kila mmoja amweleze mwenzake lile analoamini Mungu anamwitia kuwa na kulifanya, lijapokuwa dogo au kubwa kiasi gani.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Chukua hatua moja kuingia katika wito wako. Omba, tafakari, na kisha fanya jambo muhimu au la kinabii. Na baadaye mnapokutanika mwambiane yale mliyoyafanya.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika orodha ya mifano mingi kadiri uwezavyo kutoka kwenye Biblia kuhusu njia mbalimbali alizozitumia Mungu kuita watu, wake kwa waume.

Tafakari Mistari Hii Neno Kwa Neno
Amosi 7:14,15

Tumia Muda Mfupi Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Paraguay. Idadi ya watu ni 5,000,000. Watu hawa wanaishi Amerika Kusini. Asilimia 92% ni Wakatoliki, na asilimia 6% ni wa madhehebu ya Kiinjili

 

Tumeitiwa Nini?

Milango 11 ya kwanza ya Waraka kwa Warumi inahusiana na wema wa Mungu kwa watu wasiostahili, Wayahudi na wasiokuwa Wayahudi pia. Na Paulo anasema katika Warumi 12 kwamba kwa sababu ya huruma kama hiyo, sisi tumeitwa ili:

1. Kumtolea miili yetu kuwa sadaka iliyo hai, ukilinganisha na sadaka mfu katika Agano la Kale.

2. Tukome kuenenda katika njia za ulimwengu huu.

3. Tufanywe upya fikra zetu kwa neno la Mungu.

 

Kwanini? Kwa sababu tutakapoyafanya hayo Mungu anaahidi kwamba tutamfahamu na kuyakubali mapenzi yake.

 

Tumeitiwa Kuyajua Mapenzi Ya Mungu

Kwanza kabisa tunagundua kwamba mapenzi ya Mungu kwetu ni mema, kwamba anatupenda na anatutakia kila lililo jema sisi na wengine pia. Baadaye tunagundua pia kwamba matakwa yake ni ya kufurahisha. Na mwishoni kabisa tunagundua kwamba mapenzi ya Mungu ni makamilifu na hivyo tunajisalimisha kwake kabisa na kwamba hatuzitaki tena njia zetu wenyewe (Rum 12:2).

 

Tumeitwa Ili Tuweze Kujiona Wenyewe Kwa Usahihi

Si wenye kuvimba kwa kiburi, wala wenye kujiona hatufai kama wadudu. Hatufai, sawa, lakini ni wenye thamani kubwa mbele za Mungu (Rum12:3).

 

Tumeitiwa Nafasi Zetu

Hakuna mtu anayeweza kumtumikia Mungu akiwa amejitenga, akifanya mambo yake mwenyewe. Sisi tu sehemu ya mwili, ambao Kristo ndiye kichwa. Watu wengi hupenda kuwa mdomo; lakini hebu fikiria habari za domo kubwa linalotembea barabarani lakini miguu midogomidogo, na mikono midogomidogo, na kiwiliwili chembamba. Kiumbe wa ajabu! Mwombe Mungu naye atakuweka kwenye nafasi ikupasayo katika mwili huo (Rum 12:4,5) (1Kor 12:12-26).

 

Tumeitwa Kuzitumia Karama Zetu

Kama vile kifaa kinachofanya kazi kwa nguvu za umeme, tunapokuwa tumechomekwa kwenye nafasi tunayostahili, uweza wa Mungu unaachiliwa, na karama zake pia, kupitia kwetu na kuubariki mwili (Rum 12:6-8).

 

Tumeitwa Ili Tuwe Watu Tofauti

Katika Rum 12:9 hadi 13:10 Paulo anaifanyia kazi theolojia yake na kutoa maelezo ya kina kuhusu mtindo wa maisha wa Kimungu ambao kila mmoja ameitiwa kuufuata, kuufurahia na kushuhudia kwa huo.

Mungu Anaitaje?

Hapa kuna kanuni sita; nne zinamhusu Mungu, na mbili zinakuhusu wewe:

  1. Wakati wote Mungu yuko kazini hapa ulimwenguni.
  2. Mungu anatafuta uhusiano wa kirafiki na upendo wa kweli kati yake na wewe binafsi.
  3. Mungu husema nawe kwa Roho Mtakatifu kupitia Biblia, maombi, hali au mazingira mbalimbali, na kanisa ili kujidhihirisha mwenyewe, makusudi yake na njia zake.
  4. Siku moja Mungu atakuita ili ujiunge naye katika yale anayoyafanya hapa ulimwenguni. Wito wa Mungu si wewe kutenda yale unayoweza kutenda, yajapokuwa mazuri sana, bali ni wewe kujihusisha na kazi yake inayoendelea. Mahitaji ya ulimwengu huu si wito wa Mungu, bali ni fursa tu ya kutumika kwa sasa.
  5. Wito wa Mungu kuja kutumika pamoja naye mara nyingi unakuwa na mgogoro wa kukosa imani; na kinachotakiwa hapa ni imani na tendo. Shetani mara kwa mara hupenda kuleta ubishi, akiuliza, “Je, ni kweli Mungu alisema?”
  6. Kujiunga na Mungu katika kazi yake, unatakiwa kufanya marekebisho makubwa katika maisha yako, familia yako na katika kazi yako.

Hayo Yanatukiaje?

Ibrahimu, Musa, Gideon, Samweli, Yeremia na Amosi, wote waliisikia sauti ya Mungu. Yoshua, Sauli, Daudi, Elisha, wale Saba (Mdo 6:3-6) na Timotheo waliitwa na Mungu kupitia manabii na viongozi. Yesu aliwatokea wale wanafunzi na pia alimtokea Paulo (Mdo 9).

Mungu Huwaita Wanawake Pia!

Kwa kweli asilimia 75% ya wamishenari wote ni wanawake. Katika nchi kama vile Filipino, viongozi wengi wa kanisa ni wanawake.

 

Wanafaa Kwa Kazi Gani?

Ingawa makanisa yana maoni tofauti kuhusu suala hili, Biblia ina haya ya kusema:

 

Debora, alikuwa nabii, akaongoza taifa la Israeli (Waamuzi 4:5).

Ruthu, alikuwa bibi mkubwa wa Yesu.

Hulda, alitoa unabii kwa makuhani na viongozi (2Fal 22:14).

Esta, aliokoa taifa.

Wale mabinti katika Hes 27:3-7 walipokea urithi kamili walipokosekana warithi wanaume.

Binti zake Filipo walitabiri (Mdo 21:9).

Dorkasi, alijaa matendo mema, alisaidia maskini (Mdo 9:36).

Mariamu Magdalene, alikuwa wa kwanza kumwona Bwana mfufuka (Yn 20:17).

Yunia, alionekana na viongozi wa kanisa kuwa ni mtume.

 

Fibi, aliyekuwa mhudumu wa kanisa aliwasaidia wengi, mwanamke juu ya wengine, nafasi yenye mamlaka kubwa kimaandiko. Nimfa, alikuwa na kanisa nyumbani kwake; Kloe, alikuwa na watu waliokuwa chini ya Paulo; na Priska, mama Rufu, Loisi na Eunike na Afia ni washirika katika kazi ya injili (Rum 16:1) (Kol 4:15) (1Kor 1:11) (2Tim 1:5) (Flm 1:2).

Unaitwa Kwenda Wapi?

Je, ni kwenda Saudi Arabia au ni kuvuka tu barabara na kwenda mtaa wa pili? Kwanza ni vema tuelewe kwamba hatuitiwi mahali bali tunaitiwa mtu, yaani Yesu (Mt 9:35-10:10).

Anayekuita Wewe Ni Yesu

Kwa sababu mavuno ni mengi na watenda kazi ni wachache.

 

Unaitiwa Yesu

Wito wa kwanza kabisa ni kwenda kwa Yesu, kukaa naye ili kujifunza utii.

 

Anayekuandaa Wewe Ni Yesu

Kwa mamlaka yote ya kiroho unatakiwa kuponya wagonjwa na kutoa mapepo.

Analijua jina lako, na anakusaidia katika madhaifu yako mpaka utakapokuwa tayari kwenda (Mt 10:2-4).

 

Anayekupeleka Ni Yesu

Kwa wakati wake na maelekezo ya kueleweka (Mt 10:5).

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Myanmar (Burma)

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Malay, Salon

Malay

23,000

Punjabi

Panjabi, Eastern

54,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk