1985 - 2007

 

52. Je, Mungu Humwita Nani?

Billy Graham aliitwa alipokuwa kijana, naye amemtumikia Mungu maisha yake yote

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
1 Kor 1:18 – 2:16

Mstari wa Kukariri
Maana siko mashariki wala magharibi, wala nyikani itokako heshima. Bali Mungu ndiye ahukumuye; humdhili huyu na kumwinua huyu (Zab 75:6,7).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Linganisha namna wanadamu wanavyowachagua viongozi wao, na jinsi Mungu anavyoteua.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Tafuta mahali penye wachungaji au wamishenari wanaofanya huduma katika mazingira magumu na udhaifu mkubwa. Watembelee mahali walipo, au waandikie barua kuwatia moyo katika wito wao na kuwapa matumaini ya baadaye kwa maneno yako na maombi.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Chunguza katika maandiko uone ni tabia zipi Mungu anazozitafuta na uziandike katika maelezo ya ukurasa mmoja.

Tafakari Andiko Hili
1Nya 28:9,10

Tumia Muda Mfupi Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Chile. Idadi ya watu ni 15,000,000. Asilimia 27% ni wafuasi wa madhehebu ya Kiinjili, asilimia 58% ni Wakatoliki. Hii ni karne ya uamsho wa Kipentekoste, na kuwafikia watu wenye asili ya Kihindi.

 

Biblia inadhihirisha wazi kwamba Yesu ndiye ‘Ndimi’ wa nyakati zote; anayewatuma manabii, wenye hekima na walimu ili kuubariki ulimwengu kizazi hata kizazi (Mt 23:34).

Ni yeye huyo aliyeweka wengine kuwa mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na walimu (Efe 4:11).

Mungu Huchagua Kumpeleka Nani?

Andreu ni mtoto wa mchungaji na alikuwa kanisani masaa machache baada ya kuzaliwa kwake. Ni kwa nadra sana anakosa kuhudhuria ibada za Jumapili na kwa neema ya Mungu ameishi maisha yaliyobarikiwa; amejikabidhi kwa Yesu na kwa makusudi yake hapa ulimwenguni. Ungetazamia Mungu kumtuma Andreu kwenye huduma, na ndicho alichokifanya.

Lakini Mungu Anaweza Kuchagua Watu Kama Hawa?

Stefano, hakujua kusoma wala kuandika, lakini amekuwa mmishenari huko Hispania.

Miguel yule mcheza kamari, sasa ni kiongozi wa watu zaidi ya 7,000 katika mataifa 30.

Leo, kijana wa mitaani alikuja kuwa mwinjilisti hodari sana, kabla ya kufa kwa ukimwi.

Filipi, mwanakijiji maskini wa Kiafrika, sasa anaongoza watu 136,000 huko Afrika Magharibi.

Lidia, alizaliwa maskini katika mji maskini sana, katika jimbo maskini sana, katika nchi maskini ya Brazil; lakini sasa ameandaa na kuwapeleka kwenye huduma zaidi ya watu 600.

Kuinuliwa Kunatoka Wapi?

Si Kwa Kujiteua Mwenyewe

Kama alivyofanya Kora alipojiteua mwenyewe na kuongoza uasi dhidi ya viongozi waliochaguliwa na Mungu, na kusababisha maafa makubwa kwake mwenyewe na wale waliomfuata (Hes 16).

Si Kwa Kuteuliwa Na Mwanadamu

Kama ilivyokuwa kwa Sauli aliyeteuliwa na mwanadamu baada ya watu kuukataa utawala wa Mungu na kudai mfalme, ili wapate kufanana na mataifa mengine. Maafa mengine kwa wote waliohusika (1Sam 8).

Kuinuliwa Kunatoka Kwa Bwana Pekee (Zab 75:6,7)

Huu hapa ni mmoja wa mistari mizuri sana katika Biblia, “Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana” (Yn 1:6). Hapakutokea maafa, bali baraka kubwa kwa wengi.

Je, Unazo Sifa Za Kuinuliwa?

Zipo sifa tatu za msingi:

  1. Kushuhudiwa kwa habari ya dhambi, na toba ya kweli.
  2. Kubadilishwa kuwa wa Kristo.
  3. Ubatizo wa maji, wa Roho Mtakatifu na moto.

Hali ya moyo pekee ndiyo inayokufanya uwe na sifa, na wala si uwezo wa akili na kumbukumbu. Shule za Biblia ni nzuri, kama unaweza nenda ukasome, lakini kumbuka kwamba masomo hayo ni kama gari tu ambalo Mungu hulitumia kutenda kazi katika maisha yako kwa Roho wake na Neno lake. Na hapa pana sifa nyingine ya kushangaza:

Mungu Huwachagua Walio Dhaifu Na Wapumbavu

Mungu alisema jeshi la Gideoni lilikuwa kubwa mno na lenye nguvu sana kuweza kumletea ushindi. Gideoni akaamriwa na Mungu awaruhusu kwenda nyumbani wale wote wenye hofu; na hata hivyo ni wachache tu kati ya wale waliobaki ndio waliochaguliwa; na wakashinda! (Amu 7:2-7).

Mungu mwenyewe alikuja duniani akiwa mtu dhaifu (Isa 53:3).

Mungu huwachagua watu dhaifu (1Kor 1:26-29).

Mungu hupenda kutumia watu wanyonge kwa sababu uweza wake unakamilika katika unyonge wetu (2Kor 12:9).

Na halafu Mungu huwabadilisha watu wanyonge na kuwaongezea nguvu (Isa 40:29).

 

Je, Wewe Ni Dhaifu?

Je, watu husema nini juu yako; bado ni mdogo sana au ni mzee sana? Pengine hufai kwa sababu ya jinsia yako au rangi yako? Au pengine umepoteza sifa kwa kuoa au kuolewa, au kinyume chake? Je, wewe ni kilema? Furahi kwa maana udhaifu wako na kukataliwa kwako kunaonekana mbele za Mungu.

 

Mpango Wa Mungu Ni Kuziharibu Nguvu Zako

Soma Zab 66:12; 102:23. Anaruhusu hali ya umaskini na kusahaulika au kutokutambuliwa ikujie; na kuwafanya viongozi watarajiwa kuwa dhaifu na kumtegemea yeye zaidi. Lakini jaribio gumu zaidi ambalo wengi hushindwa, ni lile linalohusiana na matumizi sahihi ya mafanikio.

Sifa Kuu Ya Moyo

Mungu haangalii sura ya nje; uwe mrefu, au mweusi na mzuri; uwe umevaa vizuri au la, uwe mfupi au mweupe, mwembamba au mnene; vyo vyote vile. Mungu huuangalia moyo wa mwanadamu. Ndiyo maana akachaguliwa Daudi na si kaka zake (1Sam 16:7).

Petro alikuwa mtu asiye na utaratibu mzuri, mvuvi anayefanya maamuzi bila kutafakari matokeo yake. Hakuna mtu angependa kumchagua awe katika uongozi wa kanisa, lakini msimamo wa moyo wake ulikuwa sahihi. Halikadhalika mioyo ya watu hawa:

 

Yakobo na Yohana walikuwa wana wa ngurumo,

Thomaso alikuwa mwenye shaka,

Mathayo alikuwa mpenda fedha,

Simoni alikuwa mwanasiasa aliyetaka kufanikisha malengo yake kwa kutumia nguvu,

Paulo alikuwa adui wa Imani,

Mfalme Daudi alikuwa mtenda dhambi.

Mioyoni mwao walikuwa sahihi.

 

Yuda alikuwa rafiki na mtu wa karibu na Yesu, lakini msimamo wa moyo wake HAUKUWA sahihi.

Sifa Ya Kuwa Na Tabia Njema

Ni ajabu na kweli kwamba Mungu haangalii mambo yako ya kale ili kuamua yajayo. Hamkatai mtu kwa kigezo cha maisha yake yaliyopita. Anaangalia jinsi ulivyo sasa na utakavyokuwa kwa msaada wake. Soma Kut 18:21 na 1Tim 3:1-13; 4:12 upate kujua ni tabia zipi anazozitafuta Mungu. Unashauriwa kufanya maamuzi yafuatayo leo ili kuuvuta usikivu wa Mungu kwako:

Amua kumpenda Yesu zaidi kuliko mtu mwingine ye yote (Lk 14:26).

Amua kujikana mwenyewe na kuubeba msalaba wako (Lk 14:27; 9:2).

Amua kumkabidhi Bwana mali zako zote azitumie apendavyo (Lk 14:33).

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Nepal

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Kayort

Kayort

22,000

Kumaoni (Kumauni)

Kumauni

86,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk