1985 - 2007

 

55. Ufalme Na Biashara

Njia zilizotumiwa na wafanyabiashara wa kale, kwa ajili ya Injili leo

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Isaya 35

Mstari Wa Kukariri
Na biashara yake na ujira wake utakuwa wakfu kwa BWANA, hautawekwa hazinani wala hautawekwa akiba; bali mapato ya biashara yake yatakuwa mali zao wakaao mbele za BWANA, wapate kula na kushiba, na kuvaa mavazi ya fahari (Isa 23:18).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
 Ni wangapi wenu mnafanya biashara? Je, mnaweza kuomba na kuona namna biashara zenu zinavyoweza kufanyika chombo cha kupeleka Injili mbele?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Wapate wafanyabiashara wengi iwezekanavyo kutoka makanisa mbalimbali. Andaa tamasha lenye muziki, michezo ya kuigiza, na viburudisho. Lengo ni kuwashirikisha wafanyabiashara katika huduma ya umisheni.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Katika ukurasa mmoja andika upya theolojia ya biashara ya Ufalme kutoka Luka 19 ukitumia lugha ya kisasa na matumizi ya kisasa.

Tafakari Mistari Hii
Isa 19: 21-25

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Nigeria. Idadi ya watu ni 101,000,000 katika makabila 426. Wafanyabiashara wanazunguka ulimwengu mzima. Asilimia 50% ni Wakristo; asilimia 40% ni Waislamu. Kuna ukandamizwaji mwingi na rushwa.

 

Tumeshaangalia njia za asili na za kiroho ambazo mtendakazi wa saa ya kumi-na-moja anaweza kuzitumia kushiriki katika mavuno ya siku za mwisho katika shamba la Bwana la mizabibu. Hapa kuna njia nyingine zaidi:

Barabara Mpya Za Utakatifu

Je, uliwahi kuwaza kwamba njia za biashara zinaweza kutumika kwa makusudi ya Mungu? Kumbuka jinsi dini kuu za ulimwengu, ikiwa ni pamoja na Ukristo, zilivyoenea kwa kupitia Barabara ya Hariri kutoka Ulaya hadi Uchina. Fikiria kuhusu hili-

Uwezo Wa Mwanamume Na Mwanamke Wa Kifilipino

Moja ya bidhaa muhimu zinazouzwa nje kutoka katika taifa la Ufilipino ni nguvukazi ya maelfu ya Wafilipino wanaofanya kazi za uyaya na ubaharia katika mataifa ya ng’ambo na kutuma fedha nyumbani kwa familia zao. Mara nyingi wanafanya kazi katika mataifa ambako Injili imezuiliwa, mathalan Saudi Arabia. Wafilipino wengi wanamjua Bwana. Ingekuwaje kama makanisa yao yangewaandaa na kuwaombea watendakazi hao kuwa wamishenari; na kuzitumia ajira zao ng’ambo kama chombo cha kuwaweka huko wapate kumshuhudia Kristo! Kwa mkakati huu rahisi, nguvu ya umishenari ulimwenguni ingeweza kuongezeka maradufu kwa muda mfupi sana.

Ni Mfanyabiashara Au Mmishenari?

Baadhi ya wafanyabiashara wanaosafiri na mashirika ya ndege ya Air Afrique na Air India ni Wakristo, lakini je, yupo mtu aliyewahi kuwaambia kwamba wanaweza kutekeleza Agizo Kuu na wakati huohuo kufanya biashara? Na wanaweza wakafanya vizuri kama wanavyofanya wahubiri wengi, na pengine kuwazidi kwa sababu ya fedha zao na idadi kubwa ya watu wanaokutana nao baadhi yao hawajawahi kuingia kwenye jengo la kanisa.

Wanigeria Walioko London

Alfred Williams ni mwinjilisti kutoka Nigeria, lakini alikuja London kama mfanyabiashara akiagiza tangawizi na vinyago kutoka kwao. Faida yake ameitumia kugharamia kampeni ya kuwafikia watu ambao hawajafikiwa katika eneo fulani la London. Kanisa lililozaliwa ni kubwa, na hakuna tatizo la fedha. Bwana ameamua kutumia njia ya biashara kuubariki mji.

Wakorea, Wachina, Na Walebanoni

Wamishenari Wakorea huwaendea Wakorea wenzao wenye maduka katika nchi nyingine na kuanza kumtumikia Yesu kutokea hapo. Wakristo kutoka mataifa ya Uchina, Lebanon na India wamesambaa ulimwenguni mwote. Ni nini kingetokea iwapo makanisa ya nyumbani kwao yangewaandaa kuwa wamishenari, na kuwaruhusu wachungaji kufanya huduma ndani ya mighahawa yao, maduka yao na hoteli zao?

Jeshi Linalosubiri Kupokea Amri

Tunapoomba kwa ajili ya watendakazi, mara nyingi mawazo yetu yanaelekea kwa wachungaji au wainjilisti; lakini itakuwaje tukiombea jeshi la wafanyabiashara, au ‘washona mahema’ kama Paulo?

Biashara na Umisheni zimekuwa na ubia na ni mapacha kama mbegu mbili katika podo moja tangu zama za Barabara ya Hariri. Kumbuka jinsi injili ilivyofika Afrika na India kwa njia ya mashua za biashara za Waingereza. Wafanyabiashara wetu wangeweza kuhusishwa katika zoezi la kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi. Wengi wao wana hekima kuhusu tamaduni mbalimbali, au kufanya biashara nyumbani na kuchangia kazi mpya za umisheni.

Aina Tatu Za Biashara

Miguel Diez ana biashara ndogondogo zaidi ya 200 katika umisheni wake ulioenea katika nchi 31. Huwafundisha viongozi wake kufanya biashara katika kila nchi ambako Mungu anawapeleka. Yeye anasema kwamba kimsingi kuna biashara za aina tatu hapa duniani.

 

Biashara Za Kawaida

Hizo zipo kwa ajili ya kupata faida ambayo matumizi yake ni ubinafsi mtupu na pengine wenye mali na waliowekeza kutenda dhambi.

 

Biashara Ya Mkristo

Mwenye biashara hii hutoa zaka (10%) kanisani kwake, na mara kwa mara dhabihu. Lakini sehemu kubwa ya faida inabaki mikononi mwake.

 

Biashara Ya Ufalme

Katika biashara hii mbia mwandamizi ni Bwana. Baada ya mahitaji ya watumishi kushughulikiwa kikamilifu, faida yote hutumika kueneza Injili na kuwasaidia maskini wa ulimwengu huu.

Theolojia Ya Biashara Ya Ufalme

Katika Lk 19:11-27, kuna habari zinazomhusu Bwana Yesu; watumwa wamepewa maelekezo ya jambo la kufanya mpaka Bwana wao atakaporejea. Kila mtumwa amepewa rupia 5,000 - ni kama mshahara wa miezi mitatu, na maagizo kwamba fedha hizo zitumike kwa biashara, ya kununua na kuuza. Atakaporudi atataka kujua maendeleo ya biashara aliyowaachia.

Mtumwa mmoja ameinua mtaji wake kutoka rupia 5,000 hadi kufikia 50,000, ongezeko la mara kumi! Mfalme alisemaje kuhusu huyu mtumwa? Baadhi ya watu wanadhani kuwa kufanya biashara ni jambo la kidunia na kwamba linafaa kuepukwa. Baadhi ya wamishenari wamefundisha hivyo, wakisahau kwamba sehemu kubwa ya misaada wanayoipokea inatoka kwa wafanyabiashara walioko kanisani kwao nyumbani.

Lakini Mfalme Alisemaje?

Alisema, "Vema, mtumwa mwema na mwaminifu!” Alisema ni vema kufanya biashara na kwamba kupata mara kumi zaidi lilikuwa ni jambo dogo tu. Matokeo yake alimpa mtumwa yule miji kumi ili apate kuiendeleza miji hiyo kwa uwezo alionao. Yule mtumwa ambaye hakuzifanyia biashara fedha alizopewa alikemewa vikali na kupoteza kila kitu.

Hadithi Ya Kweli

Katika miaka ya hamsini mmishenari mmoja aliyekwenda kwenye nchi moja maskini sana huko Afrika Magharibi, aliwashauri waamini wapya kutokuwa wachungaji, na badala yake wawe wafanyabiashara wa Yesu, wakitumia uwezo wao kueneza Injili na kujenga majengo kwa ajili ya makanisa mapya. Wengine wakasema waamini wasifanye kazi za kulipwa; wazo ambalo lilipingwa karibu na watu wote. Alirudi kwao amekata tamaa. Ni kanisa moja pekee lililokumbuka alichosema na kuutafakari ushauri wake. Mfanyabiashara mmoja aliamua kutokwenda kwenye shule ya Biblia, badala yake akauza vyote alivyokuwa navyo akaenda Ghana kununua bidhaa ndogondogo na kuziuza.

Miaka kadhaa ilipita na mfanyabiashara yule akaendelea na wokovu, na pia akawa tajiri wa pili kwa ukubwa katika taifa lake. Leo hii, wakati sehemu kubwa ya nchi bado iko kwenye umaskini, makanisa ya wilaya aliyoishi huyo mfanyabiashara aliyeamua kufanya biashara kwa ajili ya Yesu, yana majengo mazuri, magari mazuri, shule, na yana uwezo hata wa kupeleka wamishenari nje ya nchi. Katika uzee wake mfanyabiashara huyo aliondoka siku za hivi karibuni kwenda kukaa na Bwana.

Sasa kwa kuwa unayafahamu haya mambo, utabarikiwa ukiyatenda (Yn 13:17).

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

 

Pakistan

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Bagri

Bagri

100,000

Balmiki

Panjabi, Western (Balmiki)

25,000

Bateri

Bateri

20,000

Deghwari

Dehwari

10,000

 




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk