1985 - 2007

 

57. Kutoka Nje

Punda wapotevu wanaelekezwa kwa utawala wa Israeli

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
1 Sam 9 na 10

Mstari wa Kukariri
Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi (1Tim 4:12).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, umewahi kujiingiza mwenyewe kwenye matatizo kwa kusema sana, mapema sana na kwa watu wasiohusika? Hebu waeleze wenzako ni nini kilichotokea, na ulichojifunza kwa ajili ya siku zijazo.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Ni nani mtu wa Mungu unayefanya huduma chini yake na kuongozwa naye? Mwendee kwa unyenyekevu na kumhakikishia utayari wako. Mtunze, na ukaribishe huduma ya kinabii katika maisha yako.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika katika ukurasa mmoja sifa utakazotaka mtu wa Mungu awe nazo ili uweze kufanya huduma chini yake kwa furaha.

Tafakari Mistari Hii
1Kor 6:12,13

Tumia Muda Mfupi Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Uchina. Idadi ya watu ni 1, 215,000,000. Hawa ni asilimia 20% ya watu wote hapa duniani.

Kuna uamsho mkubwa sana katika baadhi ya maeneo, lakini kuna upinzani mkubwa pia katika baadhi ya maeneo.

 

Je, Kuna Kitu Kinakosekana Katika Maisha?

Kwa Sauli ilikuwa ni punda waliopotea, na katika kuwatafuta kulimfanya Sauli kuanza safari ya kuelekea katika uongozi wa taifa la Israeli (1Sam 9:3).

Sauli Aliijua Sauti Ya Baba Yake

Sauli alitii maelekezo ya baba yake; vivyo hivyo sisi nasi tunapaswa kusikiliza, kusikia na kuitii sauti ya Baba yetu.

 

Je, Unakwama?

Hata katika kutii kwake Sauli hakufika mbali, na alikuwa anakaribia kurudi zake nyumbani (1Sam 9:4,5). Jambo kama hili huwatokea watu wanaohisi kuitwa na Mungu lakini hawajui la kufanya. Mtumwa huyu alijua njia atakayoiendea hadi kufikia baraka za Mungu (1Sam 9:6), na kwa kufuata mwelekeo huohuo wa kiroho unaweza pia kujenga juu ya wito wa mwanzo wa Mungu, na kisha kuelekea kwenye hatima yako. Fuata hatua zifuatazo:

Anza Kwa Kumhudumia Mtu Wa Mungu

Yule mtumwa alisema, "…basi na tumwendee yule mtu wa Mungu, pengine atatuelekeza njia tutakayoiendea..." (1Sam 9:6).

Yoshua kwanza alimtumikia Musa. Elisha alimtumikia Eliya kwanza. Timotheo kwanza alimtumikia Paulo. Baadaye nao wakapewa huduma zao. Ishi chini ya jicho lake na chini ya upako wake wa kinabii na usiondoke, mpaka Mungu akutume, na hata baada ya kuondoka dumisha urafiki naye. Anaweza akawa na ujumbe wa mara kwa mara kutoka kwa Mungu kwa ajili yako (1Sam 9:15,16). Angalia uone kwamba walimpelekea zawadi, kwa sababu kama Yesu alivyosema kwamba ilipo hazina yako, ndipo na moyo wako utakapokuwa (Mt 6:21).

Je, Mtu Wa Mungu Kwa Ajili Yako Yu Wapi?

Yawezekana ikawa vigumu kumpata mtu wa kweli wa Mungu, hata Sauli hakumtambua Samweli mara moja (1Sam 9:11,18). Pengine Samweli hakuwa amevaa majoho ya kidini, pengine hakuonekana na hali ya kikarismatiki, au pengine hakuvaa nguo za gharama na hivyo ikawa vigumu kwa Sauli kumtambua?! Usiyatumainie macho yako, mwache Mungu akuelekeze kwa baba yako wa imani.

 

Utazamie Kutoka Kwa Bwana Mambo Ya Kushtukiza

Sikuzote ukumbuke kwamba njia za Mungu na mawazo yake ni tofauti na sisi (Isa 55:8,9), kwa hiyo endelea kunyenyekea katika wito wa Mungu hata kama atakushtua (1Sam 9:20,21) (Yer 1:7) (1Sam 16:7) (1Kor 1:27).

Anza Kumtafuta Mungu Kwa Bidii

Kwa Ajili Ya Mahitaji Yako

Katika Yesu mahitaji yako yote yameishatengwa kwa ajili yako, Yesu amekutangulia (Mt 26:32). Angalia uone kwamba lile paja, sehemu ya kuhani ilishatengwa na mapema kwa ajili ya Sauli, na halikadhalika sehemu yako imeshatengwa pia (1Sam 9:23,24).

 

Kwa Ajili Ya Ufunuo Wa Kinabii

Ufunuo wa maarifa, uongozi usio wa kawaida na uingiliaji kati wa kimbingu ndiyo mambo unayoyahitaji zaidi na juu ya ufahamu wa kawaida (1Sam 9:27) (Gal 2:2) (Mdo 16:6-10).

 

Kwa Upako

Huu ni uwezeshwaji wa kiroho na wa lazima unaoambatana na wito. Ni uwepo wa Roho Mtakatifu (1Sam 10:1) (Mdo 1:8).

 

Kwa Makusudi Aliyoyachagua Kwa Ajili Yako

Kama vile Sauli alivyopakwa mafuta kuwa kiongozi juu ya urithi Wake, (1Sam 10:1), Mungu ana makusudi na maisha yako na hatima ambayo ni lazima uifikie, hata kama ni katika kipindi chote cha maisha yako. Sikuzote ukumbuke wito wako, katika nyakati ngumu utahitaji kutiwa moyo (Yer 1:5).

Sasa Fuatilia Mambo Ya Mungu

Lo lote utakalojifunza katika Shule ya Roho Mtakatifu, yapo masomo matatu ambayo ni ya msingi kabisa kwa kila kiongozi mtarajiwa (1Sam 10:2-6) (Rum 6:3-8).

Kujikana

Sauli alikwenda kwenye kaburi la Raheli jambo linaloashiria kifo (Yn 12:24) (Lk 9:23).

 

Mabadiliko Ya Ndani

Kisha Sauli anapelekwa kwenye mwaloni wa Tabori mahali panaposemekana kwamba ndipo Yesu alipobadilikia sura yake. Na hilo lina maana ya mabadiliko ya ndani yanayosababishwa na Mungu. Angalia na uone pia somo la unyenyekevu na kujifunza kupokea kwa neema katika kuenenda kwako.

 

Maisha Mapya Ya Ufufuko

Hatimaye Sauli anapelekwa Gibea, kilima cha Mungu, na hii ina maana ya kukwea kufikia maisha mapya na kuwa mtu wa tofauti (1Sam 10:6). Aliwapata watu wa kuwa nao na mahali pa kutumia vipawa vya kiroho. Zingatia kwamba adui Wafilisti walikuwepo mahali hapo pia, kwa sababu kwa kadiri Mungu anavyotaka kutekelezwa kwa wito wake adui naye anakuwepo akileta upinzani.

Dumu Katika Hekima Ya Mungu

Hekima inaweza kuwa na maana ya subira. Sauli alitakiwa kusubiri hadi "hapo ishara hizi zitakapokutukia". (1Sam 10:7) (Mit 8:12). Mpaka hapo uwe mwangalifu ni nini unachosema na ni nani unayemwambia (1Sam 10:15).

Yusufu katika Mwa 36:6-9 alifanya makosa kwa sababu alisema mapema mno.

Yangempata yapi Maria kama angepita na kumweleza kila mtu yale aliyoambiwa na yule malaika? Badala yake alimwendea yule mtu mmoja ambaye angeweza kuelewa kilichotokea (Lk 1:26-45).

Mruhusu Mungu athibitishe wito wako kiroho na katika hali ya asili kabla hujajaribu kumwongoza mtu mwingine (1Sam 10:20-23; 11:15).

Kamwe Usiyafanye Yale Aliyoyafanya Sauli Baadaye!

Hekima ni kujifunza kutoka kwenye historia. Sauli alianguka na hakuinuka tena.

Sauli hakumtii mtu wa Mungu na akapoteza urafiki na msaada.

Alipokea mahitaji yake kutoka kwa wanadamu.

Alipokea maelekezo kutoka kwa wanadamu.

Aliishi katika mwili na si katika Roho.

Alipoteza upako na mwelekeo (1Sam 13-16).

Mungu alimpa mwanzo mzuri katika huduma. Alijua la kufanya lakini akawa na kiburi, akajiamini na kufanya kinyume kabisa na njia Mungu alizomfundisha katika ujana wake. Ni huzuni kwamba aliingiwa na mapepo akafa katika upweke baada ya kushindwa, kisha Daudi akachukua nafasi yake.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Pakistan

Jina la Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Shumashti

Shumashti

14,000

Turkmen (Turkoman)

Turkmen

10,000

Vlax Rom Gypsy (Arhagar)

Romani, Vlach

14,000

Wanetsi

Waneci

90,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk