1985 - 2007

 

58. Uaminifu

Mfalme Sauli hakuwa mwaminifu, lakini kijana Daudi alikuwa mwaminifu

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
(1Sam 16:1-13) (2Sam 7:8-11, 18-29)

Mstari wa Kukariri
Lakini Bwana akamwambia Samweli, ‘Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo’ (1Sam 16:7).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, yupo mpakwa mafuta wa Mungu mahali fulani ambaye unaweza kuungana naye ukamsaidia kuliongoza taifa kwa Kristo?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Soma habari nzima ya Daudi kutoka 1Sam 16 hadi 2Sam 24, upate kuona hasa njia inayoelekea Sayuni, na vituo vyote vya kusimama.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika maelezo ya ukurasa mmoja ukiainisha vipimo vya umaskini, kusahaulika na ustawi. Elezea mahali hatari zilipo.

Tafakari Mstari Huu Neno Kwa Neno
Mt 25:21

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Iraq. Idadi ya watu ni 22,000,000. Asilimia

95% ni Waislamu; asilimia 0.03% wafuasi wa madhehebu ya Kiinjili. Kuna adha baada ya Vita vya Ghuba.

 

Daudi alipakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli wakati alipokuwa kijana mdogo, lakini ilipita miaka mingi kabla hajashika hatamu za uongozi na kuhitimisha safari ndefu ya kuelekea Mlima Sayuni. Katika kipindi chote hiki alikuwa anaandaliwa na Mungu kuwa kiongozi.

Viongozi wa leo watasafiri kupitia njia ileile aliyoipitia Daudi. Sayuni yetu si kilele cha mlima kule Israeli, bali itakuwa ni mahali pa utawala wa kiroho ambapo tutawajibika na kushuhudia ukuaji. Sayuni yetu itakuwa mahali ambapo watu wapo tayari, na hasa vijana, kutawala adui zetu (Zab 110:2,3; 48:11). Barabara iendayo Sayuni ina vituo vingi njiani.

Bethlehemu

Daudi anapakwa mafuta kuwa mfalme katika 1Sam 16:13, lakini anarudi tena uwanjani kuanza mafunzo ya uongozi. Ilibidi Daudi ajifunze kuwa mwaminifu, na Bethlehemu ina uaminifu katika mambo madogomadogo:

Mwaminifu Katika Mambo Ya Asili

Anamtii baba yake wa asili bila maswali (1Sam 17:17,18).

Mwaminifu Katika Faragha

Anaua simba na dubu sirini bila hata kutuzwa (1Sam 17:35).

Mwaminifu Katika Mambo Madogomadogo

Daudi alichunga kondoo wachache tu wakati akisubiri hatima ya mafunzo yake (1Sam 17:28).

Uaminifu Huleta Fursa

Mungu huangalia uaminifu na kwa huo, huleta fursa (1Sam 16:17-19) (Zab 75:7). Habari za sifa za Daudi zilifika ikulu na jina lake likawekwa mbele. Kuinuliwa kwa Daudi na mafanikio yake hatimaye kulisababisha hasira na chuki kwa upande wa Sauli (1Sam 18:5-9; 19:10-13).

Adulamu

Daudi sasa akawa na hitaji kubwa la binafsi na akakimbilia kwenye pango la Adulamu (1Sam 22:1-3), na akawa kiongozi wa wanaume 400 waliojiunga naye.

Baadhi yao walikuwa wenye shida - wakiomboleza kwa kujihurumia!

Wengine walikuwa na madeni – na walihitaji msaada kulipa bili zao!

Wengine walikuwa watu wasiotosheka – walionung’unika daima!

Daudi aliwajali wazazi wake pia. Walikuwa ni wahitaji na walitumaini kwamba Daudi angeweza kuwasaidia, wakati Daudi mwenyewe alikuwa anahitaji msaada! Unapokuwa njiani kuelekea Sayuni, kituo kimojawapo ni Adulamu, mahali ambapo utajifunza kuwa mwaminifu kwa walio wahitaji wakati wewe mwenyewe ukiwa katika uhitaji mkubwa zaidi. Daudi aliwafundisha kuwa na nidhamu, nao wakawa jeshi (1Sam 23:5), na akawafundisha pia kuheshimu mamlaka, hata kama ni mfalme mwendawazimu asiyemcha Mungu (1Sam 24:3-7).

Tahadhari

Lakini chukua tahadhari, kwamba katika kituo cha Adulamu watu wanaweza kukujia ili uwatimizie shida zao kwa imani yako. Wanaweza kuja lakini si katika kukusaidia, na unapohitaji msaada wao hutampata hata mmojawao! Hayo ndiyo yaliyompata Daudi alipokuwa na watu wa Keila ambao aliwaokoa na mauti (1Sam 23:1-13). Sikuzote ukumbuke kwamba ni Yesu pekee anayekutana na kila hitaji, la kwako wewe na la watu ulio nao. Sikuzote waelekeze watu wenye uhitaji kwa Yesu.

Siklagi

Daudi alikuwa akiishi Siklagi wakati imani yake kwa ahadi za Mungu ilipokuwa inatikiswa. Siku moja wale watu waliporudi Siklagi iliwaka moto, na wanawake wote na watoto walichukuliwa. Watu wa Daudi walikasirika na wakataka kumwua! (1Sam 30:1-6). Akiwa Siklagi Daudi alijifunza kuwa mwaminifu kwa Mungu hata alipokuwa amepoteza imani, familia na marafiki. Daudi ‘akajitia moyo katika Bwana’, na katika hali hii ya chini kabisa, ndipo mambo yalipobadilika na kuanza kumnyookea.

Hebroni

Hapa ndipo Daudi alipojifunzia uaminifu katika mahusiano na watu wengine wapakwa mafuta ambao walikuwa wanajeshi wazoefu na wenye nguvu kwa mtazamo wao (1Nya 11 na 12). Waliweza kutambua ndani ya Daudi, upako wa Mungu, mamlaka na maono; kwa hiyo badala ya kuendelea na fani zao au ‘huduma’ zao, walimjia Daudi wakiwa wamedhamiria kabisa kumfanya mfalme wa Israeli. Baada ya uzoefu wa Adulamu Daudi aliwauliza maswali matatu muhimu:

Mmekuja kwa amani?

Mmekuja kunisaidia?

Mmekuja kuungana nami?

(1Nya 12:17,18)

Walipoingia kwenye umoja naye upako uliongezeka na riziki pia (1Nya 11:3; 12:39,40). Miaka saba baadaye, kwa pamoja waliyashinda majeshi ya Wayebusi, na kuutwaa Mlima Sayuni na kuuleta utawala wa Ufalme wa Mungu (2Sam 5:6-12).

Sayuni, Mwisho Wa Safari

Sayuni ni uaminifu katika kutawala, kutawala kama Kristo, bila kuwadhibiti watu isivyo halali kwa njia za ujanjaujanja. Daudi alifanya vema, lakini katika utawala wake alipata majaribu mengi ya uaminifu, lakini hakuweza kufaulu yote. Kwa mfano; alirejesha Sanduku la Agano kwa njia isiyo sahihi, na kusababisha kifo cha mtu mmoja. Alizini na Bathsheba, na kusababisha kifo cha mumewe na mtoto aliyezaliwa. Kijana wake Absalomu aliongoza maasi yaliyosababisha kifo chake mwenyewe na wengine wengi.

Mtihani Mgumu Kuliko Yote

Unapokuwa njiani kuelekea Sayuni unaweza ukabanwa na umaskini lakini ukaendelea kuwa salama kwa sababu uko jirani na Yesu. Unaweza kupata shida ya mfadhaiko wa kutokujulikana, lakini ukamtumikia Yesu katika yote na kubaki salama kwa kuepukana na kiburi. Ndani ya Sayuni ndiko kwenye mtihani mgumu kuliko yote kwa ajili ya kila kiongozi, na wengi wanashindwa. Ndani ya Sayuni kuna mafanikio na sifa, na kwa sababu ya hayo, ni ajabu kwamba viongozi wanaweza, na kwa kweli humwacha Yesu na kuanguka.

  1. Ukiwa Bethlehemu, uwe mwaminifu kwa mambo madogomadogo.
  2. Ukiwa Adulamu, uwe mwaminifu kwa watu wenye uhitaji.
  3. Ukiwa Siklagi, uwe mwaminifu hata unapokuwa umepoteza vyote.
  4. Ukiwa Hebroni, uwe mwaminifu katika mahusiano.
  5. Unapokuwa Sayuni, uwe mwaminifu kwa Mungu katika kutawala.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Ufilipino

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Malay (Melaju)

Malay

140,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk