1985 - 2007

 

60. Kukata Tamaa Kushindwe

Kwanini kujiinamia? Mtumaini Mungu!

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Yoshua 1

Mstari wa Kukariri
Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako (Yos 1:9).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, kuna mtu miongoni mwenu aliyevunjika moyo? Uwe mwaminifu kwa kuwa Mungu huwapa neema walio wanyenyekevu. Hudumianeni ninyi kwa ninyi.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Mwombe Mungu akuongoze kwa baadhi ya watu waliovunjika moyo, na kisha uwahudumie kwa kuwapa tumaini. Jitolee kuwaombea kulingana na majibu tuliyopata.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Tafakari sababu za watu kuvunjika moyo, halafu andika maelezo ya kurasa mbili kuhusu ni wapi sababu hizo zinakoweza kuonekana katika maisha leo.

Tafakari Andiko Hili Neno Kwa Neno
1Pet 5:6-11

Tumia Muda Mfupi Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Niger. Idadi ya watu ni 8,000,000 (Waafrika wanaoishi jangwani).

Asilimia 90% ni Waislamu wa dhati; asilimia 0.38% Wakristo walio huru kwa injili.

Kuna makabila yasiyopungua 19 ambayo hayajafikiwa.

 

Sikuzote nitamkumbuka rafiki yangu Yohana. Siku moja muda mfupi baada ya kuokolewa na maisha ya ulevi wa madawa, alisimama kuimba Zaburi ya 42 ms 1, 2, 5 na 6 kwa sauti nzuri na nzito.

"Nafsi yangu kwanini kuinama,

Na kufadhaika ndani yangu?

Umtumaini Mungu;

Kwa maana nitakuja kumsifu,

Aliye afya ya uso wangu, na Mungu wangu".

Miaka kadhaa baadaye nikasikia kwamba Yohana amestaafishwa, na kwamba amevunjika moyo sana. Ni nini kilichokuwa kimetokea?

Je, Umevunjika moyo? Huko Peke Yako!

Kuvunja watu moyo ni mojawapo ya silaha anazotumia Shetani, na amekuwa akiitumia katika vizazi vyote. Soma waliyoyasema watu hawa:

Kwahiyo Kwanini Kujiinamia?

Ujasiri huja kwa kutiwa moyo, na kinyume chake ni kuvunjika moyo na ni pale kitu fulani kinaposababisha ujasiri wetu kutoweka. Zifuatazo ni baadhi ya sababu zilizowafanya watu kwenye Biblia kuvunjika moyo ~

Ugumu Wa Safari Yenyewe

Katika Hes 21:4 wale watu walikuwa wamechoshwa na safari ya kuelekea kwenye nchi ya ahadi. Jangwa lilikuwa linawaletea madhara.

 

Takataka Za Zamani

Katika Neh 4:10 wale watu walikuwa wamechoka kwa kubeba kifusi na mawe ya zamani. Hilo laweza kuwa kweli hata kwetu pia ikiwa tabia za zamani zinaweza kuturudia na kutusababisha kuanguka.

 

Maneno Kutoka Kwa Adui

Katika Neh 4:11 maadui wenyeji waliongeza wingi wa maneno ya kukatisha tamaa.

 

Unapoacha Kumwangalia Yesu

Katika Zab 73:2,3 mwandishi anashuhudia kwamba ilikuwa nusura aanguke alipoacha kumtumaini Mungu na kuanza kutamani mafanikio ya watu waovu. Hatari!

 

Njia Za Siri Au Zidanganyazo

Katika 2Kor 4:2 Paulo anajua jinsi inavyoweza kukatisha tamaa wakati watu wanapofanya mambo yao ya aibu kwa siri.

 

Mungu Wa Dunia Hii

Huyo ni Shetani, aliyetajwa katika 2Kor 4:4. Mungu ndiye anayekupa saburi na faraja, Rum 15:5, ili upate kujua ni nani anayewaondolea hali ya kuvunjika moyo.

 

Kujijengea Himaya Binafsi

Hakuleti baraka za Mungu bali hupelekea kushindwa na kuvunjika moyo (2Kor 4:5).

 

Uchovu Na Udhaifu Wa Mwili

Katika 2Kor 4:7 Paulo anatufananisha sisi na vyombo vya udongo ili kuonesha jinsi tulivyo wepesi kuvunjika, na kwamba tunayo hazina tukufu ya Mungu ndani mwetu. Kumbuka kwamba vyombo vya udongo vina wepesi wa kuvunjika au kupata mpasuko; na vivyo hivyo miili yetu na akili zetu ikiwa tutazifanyiza kazi kupita kiasi.

 

Shughuli Za Mungu

Kama tutasahau kwamba Mfinyanzi Mkuu sikuzote yuko katika utendaji wa kutufinyanga, kutupa sura na kutunyoosha ili tufanane zaidi na Yesu, tunaweza tukakatishwa tamaa na baadhi ya mambo yanayofanyika katika karakana ya Mungu (2Kor 4:8-11).

Jinsi Ya Kushinda Kukata Tamaa

Halipo jambo moja pekee unaloweza kulifanya sikuzote kwa sababu kama tulivyokwisha kuona, sababu za kukata tamaa hazifanani. Lakini zifuatazo ni baadhi ya hatua unazoweza kuchukua:

Watambue Wababe Walioko Langoni

Wababe wawili wanaolinda lango la kuingilia kwenye nchi ya ahadi hata leo wanaitwa hofu na kukata tamaa. Ikiwa sasa unasikia sauti zao, na kuhisi msukumo wa ushawishi wao, basi ujue kwamba upo karibu sana na ahadi zako.

Katika kipindi hiki muhimu, kama ilivyokuwa kwa Yoshua, unapaswa kuwa hodari na moyo wa ushujaa na kusonga mbele katika neema anayokupa Mungu (Yos 1:9).

 

Elewa Kinachoendelea

Katika 2Kor 4:16,17 Paulo anasema tusilegee kwa sababu kwa kupitia dhiki yetu utu wetu wa ndani unafanywa upya. Anasema dhiki yetu nyepesi na iliyo ya muda mfupi tu, inatufanyia kitu chema katika Mungu.

 

Tumaini Kwa Mungu

Hata kama imani yako ni ndogo, bado unaweza kumtumaini Mungu na kuamini kwamba Mungu wa amani atamseta Shetani mara chini ya miguu yako (Zab 42:5) (Rum 16:20).

 

Kiri Hitaji Lako, Mshirikishe Mwenzako Kisha Mwombe

Katika Mhu 4:12 tunaona kwamba uwezo wa watu wawili ni mkubwa kuliko wa mtu mmoja. Usihifadhi tu mawazo yako, mshirikishe mwenzako na halafu mwombe pamoja, na kumfunga Shetani.

 

Pokea Kutoka Kwa Mungu

Fungua moyo wako na umwachie Roho Mtakatifu akuhudumie kwa habari ya saburi na faraja ya Mungu, tumaini, furaha na amani (Rum 15:5, 13).

 

Shughulikia Sababu Za Asili

Wakati Eliya alipokuwa amechoka na kukata tamaa, Mungu alimpelekea chakula na pumziko kabla hajashughulika na sababu zenyewe na kumpa neno jipya, mwelekeo mpya, na tumaini jipya (1Fal 19:3-18).

 

Simama Kwenye Ahadi Ya Mungu

Petro anatuasa kuwa wanyenyekevu chini ya mkono wenye nguvu wa Mungu, kumtwika Yeye fadhaa zetu, kuwa na kiasi, kumpinga Shetani na kuwasaidia wengine wanaoteseka. Anatupa tumaini kubwa kwa kusema kwamba Mungu wa neema yote atatujia mara ili kututengeneza, kututhibitisha na kututia nguvu (1Pet 5:6-11).

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Russia

Jina la watu

Lugha

Idadi yao

Andi (Qwannab)

Andi

10,000

Caucasian Mountain Jew

Tat, Kiebrania

15,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk