1985 - 2007

 

63. Kulijenga Kanisa

Je, kanisa zuri linafananaje?

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Ufu 19:1-10; Efe 5:22,32

Mstari wa Kukariri
…ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho…(Efe 3:10).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Linganisha taratibu ngumu za vipindi na mipango kama zinavyoonekana katika kanisa siku hizi; na wepesi na umuhimu wa kuzitii amri za msingi za Kristo katika dhana ya mti wa uzima.

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Kama umeoa/umeolewa zungumza na mwenzako ili kuona kama ndoa yenu ina upendo wa kwanza, kujaliana na malengo kama yale Yesu aliyonayo kwa kanisa. Kama bado hujaoa/hujaolewa jiandae sasa na misimamo sahihi ya ndoa, na kufanya maombi, halafu tuone ni nini Bwana atakalokutendea.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Uchore ule mti wa uzima wewe mwenyewe na kisha andika pembeni mipango ya kanisa lako. Andika pia orodha ya mawazo yako.

Tafakari Mstari Huu Neno Kwa Neno
Yn 15:16

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Comoros. Idadi ya watu ni 500,000. Ni taifa la visiwa katika bahari ya Hindi. Ni nchi inayoendelea, maskini. Waislamu ni wengi; Wakristo ni kama 120 tu, nao wanateswa.

 

Kanisa Ni Nini?

Iwe tunazungumzia habari za kanisa la ulimwengu mzima, au kanisa la mahali fulani, lakini ‘kanisa’ sikuzote ni watu na kamwe si jengo hata lingekuwa zuri namna gani. Sisi ndio kanisa lenyewe, ‘Nyumba ya Bwana’ pekee.

Umuhimu wa Kanisa

Kanisa ni kusudi la Baba, (Efe 3:10).

Kanisa ni ahadi ya Mwana, (Mt 16:18).

Kanisa ni matokeo ya ujio wa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste, (Mdo 2:42-47).

Kanisa kule Antiokia lilianzishwa na waamini wa kawaida na kutiwa nguvu na waamini wenye karama, (Mdo 11:19-26).

Kuanzisha makanisa lilikuwa ni moja ya malengo makuu ya Paulo, (Mdo 13; 14:23; 19; 20:17).

Leo Mungu anabariki huduma za uanzishaji wa makanisa mapya ulimwenguni pote.

Kanisa Zuri Linafananaje?

Kiroho, Efe 5:25-27 inasema kwamba Yesu amelipenda kanisa na akajitoa kwa ajili yake kwa nia moja. Kanisa zuri huwa takatifu, safi, lenye neno la Mungu kwa wingi, linalostahili kupewa Yesu kama bibi-harusi mzuri, asiye na doa, kunyanzi, mawaa, wala lo lote kama hayo.

Lakini hata hivyo...

Ingawa kila mmoja atasema ‘Amina’ na kutaka kanisa lake lifanane hivyo, lakini angalia yanayosemwa hapa yanahusu ndoa. “Enyi waume, wapendeni wake zenu,…” Paulo anasema, kama Yesu naye alivyolipenda kanisa akajitoa kwa ajili yake, kiasi cha kuutoa uhai wake. Hivyo ndivyo tunavyopaswa kuwapenda, kuwalinda na kuwatunza wake zetu. Je, tunaweza kufanya vizuri zaidi?

Kwa uhalisi wake kanisa zuri linafananaje? Angalia mchoro ulioko hapo chini. Utadhani ni mnazi, lakini umepewa jina la ‘Mti wa Uzima’ na mchungaji mmoja Mwafrika ambaye alipokea ufunuo kutoka kwa Roho wa Mungu.

Chagua hapa > 63chart ili uweze kuuona mchoro wa ‘mti wa uzima’

 

Kanisa Kama Mti Wa Uzima

Mizizi Isiyoonekana Huenda Chini
Kanisa zuri lina mizizi isiyoonekana, iliyokwenda chini na ambayo daima inatafuta uzima ambao pekee unapatikana kutoka kwa maji yaliyo hai ya Mungu. Kwahiyo msingi imara ni muhimu, katika maombi, na hekima itokanayo na neno la Mungu, na upendo na uweza upatikanao kwa Roho Mtakatifu (Yer 17:7,8) (Zab 1).

Shina, Limegawanyika Katika Sehemu Tatu Zinazoelekea Juu
Shina ni sehemu ya mti inayoonekana vizuri sana. Hukua kwa hatua ukianzia pale mbegu inapochanua na kutoa majani, kisha hukua na kuwa mti wenye nguvu, unaodumu na kustahimili hata upepo mkali.

Msingi Katika Uinjilisti
Kanisa zuri huanza huduma inayoonekana kwa kufanya uinjilisti, na kwa kweli shughuli hiyo ya uinjilisti haikomi. Bila kuendeleza huduma ya uinjilisti katika sura zake nyingi watu wataendelea kubakia kwenye dhambi na ujinga wa kutokumjua Mungu. Kwanini tunafanya uinjilisti? Ni kwa sababu Yesu alituagiza kufanya hivyo (Mk 16:15,16).

Nguvu Ya Ufuasi
Sasa lile shina hukua na kuwa na uwezo wa kuutegemeza mti katika hatima yake ya kuzaa matunda. Bila kuacha hata wakati mmoja kutangaza habari njema, kanisa zuri litatumia muda mwingi kuwabadilisha waamini wapya kuwa wafuasi. Halafu litawabadilisha hao wafuasi kuwa viongozi watakaochukua jukumu la kuiendeleza kazi ya Mungu. Kwanini kuandaa wafuasi ni jambo muhimu sana kwetu? Ni kwa sababu Yesu alituagiza kufanya hivyo.

Soma Mt 28:19 na sehemu za Ufuasi katika mfululizo wa masomo haya

Kuwajali Maskini Kwa Namna Ya Kipekee
Bila kusitisha huduma ya uinjilisti hata mara moja, kanisa zuri sasa litaiga mfano wa Yesu katika Mdo 1:1 na Mdo 10:38 kwa kutenda mema. Zaidi ya mara 300 katika Biblia Mungu anatangaza upendo wake kwa watu maskini na wenye uhitaji. Anatazamia mwili wake ambao ni kanisa lake kuwa mikono yake inayojali na midomo yake. Si kila mtu ameitwa kuhubiri au kuongoza lakini kila mwamini anaweza kuonesha huruma ya Mungu kwa maskini, hasa kwa wajane na watoto. Kuwajali maskini ni muhimu kwa sababu ndivyo Yesu alivyosema. Tazama Mt 25:34-45, Yak 1:27, na somo kuhusu Huruma ya Mungu kwa Maskini.

Kivuli Cha Miti Kimefunika Uchumi Wa Ufalme

Hapa kuna jambo ambalo makanisa mengi hulipuuzia na ni hatari kwao. Hebu fikiria kidogo. Maombi na neema ya Mungu kwa ajili ya matatizo yanapatikana bure, lakini uinjilisti una gharama. Ufuasi una gharama zaidi, lakini kuwajali maskini kuna gharama kubwa zaidi. Je, hizo fedha zitapatikana wapi? Na sasa tafakari hili…

Katika Mdo 2:42-47 na Mdo 4:32-35 tunaona kwamba kanisa la Yerusalemu lilikuwa tajiri kiasi kwamba hapakuwa na mtu mhitaji miongoni mwao. Miaka kadhaa baadaye kanisa lilelile kuu lilikuwa kwenye umaskini kiasi kwamba ilibidi Paulo achangishe fedha kutoka kwa makanisa mapya katika bara la Ulaya. Kulitokea nini?

Katika Mdo 6:1-7 viongozi wa kanisa walikasimu masuala ya ubaguzi wa rangi na fedha kwa watu saba wenye asili ya Kiyunani, na pengine walikuwa ni wahubiri. Kwa hiyo viongozi hawakujihusisha tena na masuala ya fedha. Wahubiri wanapenda kuhubiri, si makaratasi. Mahubiri hayo, kwa huzuni kubwa, yalimgharimu Stefano uhai wake, na kisha Filipo akaenda zake Samaria. Katika wale saba wamebakia watano. Iwapo hao watano nao walikuwa wakihubiri au kama walitawanywa na ile dhiki ya Mdo 8:1, ni nani basi waliokuwa wakishughulikia masuala ya kiuchumi? Je, ni mtu ye yote? Sisi hatujui.

Wale maskini hakika walitoka mbali na katika eneo kubwa, kwa kusikia kwamba mahitaji yalipatikana; wakasikia injili, wakampokea Yesu na kujiunga na kanisa. Gharama ziliongezeka lakini kipato hakikuongezeka. Somo linaeleweka. Iwapo hatakuwepo mtu, mbali na mhubiri mkuu, atakayejihusisha kikamilifu na uchumi wa kanisa kwa imani na kwa matendo, umaskini utakuwa ukizengea mlangoni. Kwanini usimamizi wa fedha ni muhimu kiasi hicho? Ni kwa sababu tu Yesu alisema hivyo. Tazama Lk 19:11-26, na somo kuhusu Fedha Katika Ufalme Wa Mungu.

Tunda Lenye Mbegu
Kanisa zuri sikuzote huzaa tunda kwa msimu. Na tunda hilo litamletea Mungu utukufu utakaoonekana katika miti mipya michanga ya makanisa binti, yaliyo karibu au mbali kupitia umisheni. Kila mti mpya una mizizi yake kwa Mungu, ikiwa ni kwa uinjilisti, ufuasi, fedha zake na tunda.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Bado Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Senegal

Jina la watu

Lugha yao

Idadi yao

Gusilay

Gusilay

12,400

Jahanka (Diakhanke)

Azer

35,000




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk