1985 - 2007

 

68. Kanisa La Nyumbani

Rafiki za Mungu, wao kwa wao na wale wanaowazunguka

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Mdo 10:22-48

Mstari wa Kukariri
Na sikuzote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa (Mdo 2:46,47).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Kama mateso yangekuja wilayani kwako kanisa lingetokewa na nini?
Je, unaweza kufanya nini ili kuwalinda hao watu?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Andaa mkutano wa kirafiki kwa mtindo wa seli katika moja ya nyumba zenu, na chakula. Waalike watu wa mitaani na kuona ni wangapi watakaohudhuria. Waambie kwamba kuna mtu atakayezungumza kwa dakika tano akielezea jinsi alivyokuja kumjua Kristo. Ona ni wangapi watakaokuja!

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika taarifa ya kurasa mbili ukielezea athari za muda mrefu kwa kanisa tangu mwaka 321 BK lilipofanywa kanisa rasmi na kurithi mahekalu na majoho.

Tafakari Mstari Huu Neno Kwa Neno
1Kor 14:26

Tumia Muda Mfupi Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Italia. Idadi ya watu ni 58,000,000. Kuna kudidimia kwa utamaduni wa Kikatoliki. Ipo miji 31,000 isiyokuwa na wafuasi wa madhehebu ya kiinjili

 

Mwinjilisti mmoja anaelezea jinsi kampeni zake katika jiji moja barani Afrika zilivyofanikiwa. Kulikuwa na baraka nyingi kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kuwahudumia waamini wapya. Alichoweza kusema ni, “Wakristo wanaoishi maeneo haya na haya nyosheni mikono yenu juu. Waamini wapya, kama mnaishi katika maeneo hayo kusanyikeni Jumapili ifuatayo majumbani mwa watu hawa”. Kisha akaendelea kutaja majina na kuwaelekeza watu. Alisema hiyo ndiyo iliyokuwa njia pekee ya kutunza salama mavuno makubwa kiasi hicho. Alichokifanya ni mpangilio wa kile tunachokiita Kanisa la Seli.

Ungefanya nini kama ghafla kundi kubwa la watu linaamua kumfuata Yesu? Je, ungepata wapi fedha kwa ajili ya majengo mapya?

1. Kanisa Katika Matendo Lilikuwa Ni Kanisa La Seli

Kanisa halikuwa na majengo hadi lilipofanywa kanisa rasmi la Utawala wa Kirumi mnamo mwaka 321 BK. Kwa hiyo likarithi mahekalu yote ya kipagani na majoho ya kikuhani na kubaki nayo tangu wakati huo. Mdo 2:46 inatuambia kwamba kanisa la kwanza lilikusanyika kila siku katika hekalu la Kiyahudi mjini Yerusalemu kumwabudu Mungu. Halikadhalika walimega mkate nyumba kwa nyumba, na kula pamoja kwa furaha na moyo mweupe, huku wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kanisa lilikuwa mitaani na watu, lilikuwa bado halijajificha ndani ya majengo ya kidini.

Siri Ya Kufanikiwa Sana Kwa Makanisa Ya Seli

Kwa kawaida kanisa la seli lina watu kati ya 5 hadi 15. Hii ina maana kwamba kila mmoja anajulikana na anapokosekana wengine wanaguswa kikwelikweli.

Kanisa la seli maana yake ni kwamba kila mshiriki ana jambo la kufanya kama muziki, kupangilia, kufundisha, kuongoza maombi, kupika, au kutunza watoto. Furaha ya kuhudumu haimo mikononi mwa watu wachache tu wasomi wa kidini au viongozi.

Kanisa la seli maana yake ni kwamba watu kamwe hawatajisikia wapweke kanisani kwa sababu mpangilio wa jamii unawaleta hadi kwenye moyo wa familia ya Mungu.

Kanisa la seli ni mahali pa asili pa kufundishia kwa uhuru kabisa na uzima wa kundi dogo.

Kanisa la seli ni mahali ambapo watu wanaweza kutumia vipawa vyao vya kiroho kwa sababu pana mazingira ya kirafiki na kiongozi mwenye upendo na familia ya kikristo inayotia moyo na kusaidia.

Kanisa la seli maana yake ni kwamba majirani ambao wasingekuwa tayari kwenda kwenye jengo la kanisa wanaweza kupata fursa ya kumgundua Yesu mahali anakopenda kuwa, miongoni mwa watu. Kwenye kanisa la seli upeo wa namna mbalimbali za ubunifu katika uinjilisti nyumbani hauna ukomo.

Kanisa la seli linaruhusu watu wenye karama kuwaendea waamini wengine ili kusaidia kuwaandaa.

Katika kanisa la seli ukuaji ni wa kasi na kamwe hauzuiwi na ukosefu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo. Ukuaji wa kikundi unapozidi watu 16 kwa mfano, inabidi kikundi kijigawe kuwa vikundi viwili katika nyumba mbili tofauti na kila kimoja na kiongozi wake. Kila kikundi kitakuwa haraka na mara kila kimoja kitakuwa na watu 15 na kujigawa tena.

Kanisa la seli maana yake ni maombi zaidi, kwa sababu watu wengi zaidi wataomba katika vikundi vidogovidogo, na wanaweza kukutana wakati wo wote. Utaratibu huu ni mzuri zaidi kuliko ule wa kukusanyika mahali pamoja mara moja tu kwa wiki, ambapo watu wengi wanashindwa kuhudhuria kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kazi.

Kanisa la seli maana yake ni kwamba wagonjwa au wenye uhitaji wanaweza kuombewa haraka bila kulazimika kumsubiri mchungaji.

2. Makanisa Ya Seli, Makusanyiko Na Sherehe

Kanisa la seli halimiliki jengo wala kufanya malipo yo yote; wala hakuna mkutano mkubwa kila Jumapili kwa sababu seli zenyewe ndizo kanisa. Hakuna nyaraka wala kumbukumbu zinazohifadhiwa, kwa hiyo pakitokea dhiki majina hayawezi kupatikana, hapatakuwepo na majengo ya kuchoma moto, makusanyiko hayataonekana na kufanyiwa mauaji ya halaiki kama yaliyofanyika nchini Rwanda miaka ya nyuma. Kanisa litakuwa salama zaidi.

Makanisa ya seli, viongozi na waamini wote wanapaswa kukusanyika mara kwa mara ama kwenye jengo la kukodisha au kwenye uwanja wa michezo, kwa ajili ya sherehe; na makanisa yote ya seli kwenye kanda moja yanaweza kukutana kwenye kusanyiko pengine mara moja au mara mbili kwa mwezi. Waangalizi wanapaswa kukutana na viongozi wa seli mara kwa mara, na pia kuyatembelea makanisa hayo.

3. Je, Kwenye Kanisa La Seli Kunafanyika Nini?

Lengo ni kuwa marafiki wa Mungu kupitia mfano wa Mdo 2:42 wa kudumu katika neno la Mungu, katika kusali, katika kuumega mkate na katika ushirika; halafu kuwa marafiki wenyewe kwa wenyewe; na kisha kufanya urafiki na watu wa mitaani ili wapate kugundua kwamba upendo wa Mungu haupo mbali nao.

Kumbuka Kuzingatia Mambo Manne Yafuatayo:

Kukaribishana - Wewe kwangu, na mimi kwako.

Ibada – Sisi tumwabudu Mungu.

Neno – Mungu ameachilia kwetu, kupitia Biblia, karama za kiroho, maombi na kuhudumiana.

Kushuhudia – Mungu anawafikia wengine kupitia kwetu.

4. Kuanzisha Kanisa La Seli

Ni jambo rahisi tu kwa mmishenari kuandaa utaratibu wa kanisa la seli kwa kuanzia nyumbani na kisha kukua na kuzidishwa. Ni vigumu zaidi kubadilisha mfumo wa kanisa uliozoeleka kwa sababu kanisa la seli Iinawapa watu uwezo wa kujali na kueneza injili, na hilo linaweza likawafadhaisha watumishi wanaolipwa. Mabadiliko hayo yanaweza kuwa tatizo pia kwa watu waliotulia na kustarehe, lakini ikiwa Mungu ametoa maelekezo, yafaa juhudi ifanyike kuleta mabadiliko hayo.

5. Namna Ya Kubadilika Kuelekea Kwenye Kanisa La Seli

Kunahitajika muda wa kutosha wa maandalizi, maombi, mpango na makubaliano.

·   Chagua viongozi wa seli na wasaidizi wao kwa kigezo cha unyenyekevu wao, moyo wa utumishi na uaminifu katika kuunga mkono.

·   Waandae mapema kwa kuwapa stadi za kichungaji, na jinsi ya kuongoza kikundi kidogo.

·   Wanatakiwa kujua mipaka ya mamlaka zao na ni nini la kufanya kunapotokea tatizo.

·   Igawe wilaya katika kanda, na kila kanda iwe na kiongozi wa dhati.

·   Igawe kila kanda katika seli, na kila seli iwe na kiongozi na watu.

·   Chagua muda wa kukutana, na kisha anza.

·   Fuatilia maendeleo mara kwa mara.

6. Maono Ya G12 Ya 2001

Hii ni hatua nyingine ya maendeleo katika kanisa la seli inayoleta mabadiliko makubwa katika nchi za Latin America, na sasa inaanzishwa Uingereza, Hispania, na Ulaya kwa ujumla. Zipo kanuni nne nazo ni; Mpate mtu, Mfanye mmojawenu, Mfanye mwanafunzi, na kisha Mwachilie. Na mkakati uliopo ni kwamba kila kanisa la seli lizae makanisa mengine 12. Kwa maelezo kamili ya kile kinachotakiwa kwa ajili ya G12 na ambacho kitakuwa ni sehemu ya somo hili, tembelea kurasa za mtandao wa kompyuta zifuatazo:

http://www.mci12.com/english/Home-engl.html ambao ni ukurasa wa kanisa la Mchungaji Cesar Castellanos nchini Colombia ambalo limekua kutoka watu 8 hadi kufikia 120,000 na lina kundi la vijana 30,000 kupitia mkakati wa G12.

http://www.revivaltimes.org/index.php/213.htm huu ni ukurasa kutoka Hekalu la Kensington/Kanisa la Jijini London ambalo limefanyia kazi maono ya G12 kwa ajili ya jiji la London na sasa unaonekana ukuaji usio wa kawaida katika mazingira ya kidunia.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Syria

Jina la Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Turk

Turkish

45,000

Turkmen (Turkoman)

Turkmen

98,000

 




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk