1985 - 2007

 

73. Kanisa La Watu

Uwezo uletao ushindi kwa kufanya kazi pamoja

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Matendo 22

Mstari Wa Kukariri
Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu (1Pet 2:9).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, ni kwa namna gani ninyi kama ukuhani wa kifalme mnaweza kutoa sadaka za kiroho za gharama ambazo tumeziona kwenye Biblia katika somo hili?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Kati ya sasa na hapo tutakapokutana tena mwombe Bwana akuongoze katika mazingira ambayo unaweza kufanya jambo alilolifanya Yesu. Halafu hali hiyo inapotokea kumbuka somo hili, usitafute visingizio bali jitokeze kwa imani na kwa uweza wa jina lake.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Andika maelezo ya kile Yesu alichoomba alipomwendea Baba ili kukuwezesha wewe kufanya huduma kwa namna ileile aliyofanya yeye (Yn 14:12).

Tafakari Mstari Huu Neno Kwa Neno
Yn 14:12

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Thailand. Idadi ya watu ni 60,000,000. 

Kuna tatizo kubwa la rushwa, ukosefu wa maadili, na madawa ya kulevya. Asilimia 93% ni Mabudha, na asilimia 1% tu ni Wakristo.

 

Wewe Ni Nani, Bwana?

Hili ndilo swali la kwanza alilouliza Sauli wakati alipoingia kwenye utukufu wa Mungu bila kutazamia, alipokuwa akisafiri kwenda Dameski (Mdo 22:8-10). Mara Sauli, baadaye aliitwa Paulo, alipotambua kwamba alikuwa katika uwepo wa Bwana Yesu mfufuka, aliuliza swali la pili ~

Nifanye Nini?

Swali hilohilo bado lipo midomoni mwa waamini wengi leo wanaotaka kumtumikia Bwana badala ya kufuata mambo ya ulimwengu huu. Ni huzuni kwamba si kila mmoja anapata fursa ya kuifanyia kazi imani yake kwa sababu katika baadhi ya makanisa kila kitu kinafanywa na watumishi wasomi wa mambo ya dini au viongozi wa kulipwa; na kuwaacha waamini wengine kukosa la kufanya isipokuwa tu kuhudhuria makusanyiko ya Jumapili na kulipa zaka na dhabihu bila hata maelezo ya jinsi zinavyotumika. Badala ya kuhamasishwa, kanisa, mara kwa mara linaduwazwa.

Kwa upande mwingine, wachungaji wengi wanalalamika kwamba hawana mtu wa kuwasaidia lakini wanashindwa kuona kile Mungu alichoweka mbele yao.

Nguvu Ya Umisheni Ipo Kwa Washirika

Kweli nguvu ya umisheni ipo kwa washirika lakini jeshi lisilotembea haliwezi kamwe kushinda. Katika historia ya Kanisa kunaonekana vilele viwili vya ukuaji wa ajabu. Utaweza kuona vilele hivyo katika karne ya kwanza, na ya 16, katika kile kiitwacho Matengenezo.

Katika nyakati hizo watu wa Mungu wengi, si viongozi pekee yao, walipewa motisha na kuhamasishwa kwenda mbali na kusambaa eneo kubwa ili kueneza habari njema na wakati mwingine katika mazingira ya mateso. Jeshi la Mungu likasonga mbele kwa uweza na kuutikisa ulimwengu.

Katika nyakati nyingine katika historia viongozi wa dini hawakuruhusu watu kusoma maandiko achilia mbali kufanyia kazi karama zao na imani. Hata leo watu wa Mungu wenye uwezo mkubwa wanaweza kufadhaishwa sana iwapo watafanywa watazamaji tu, wakiwa hawajui watakavyomtumikia Mungu kama wanavyohimizwa na mahubiri ya mara kwa mara. 

Historia inatufundisha pia kwamba mfadhaiko huo ukiongezeka, au ikijitokeza huduma mbadala,  kanisa lililowekwa kisheria linaweza likapoteza watu kwa haraka. Hata hivyo Biblia inatufundisha njia iliyo bora zaidi.

Kila Mshirika Awe Mhudumu
Mtume Petro anaandika hivi, "Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo" (1Pet 2:5, angalia pia ms 9). Kwa viwango vya Agano Jipya ukuhani ni kwa ajili ya waamini wote, na si fani ya baadhi ya waamini, na kisha lile neno lisilo la kibiblia – ulei. Na je, umeona ni kitu gani Yesu alisema waamini wanaweza kufanya katika Mk 16:16-18?

Je, Hii Ina Maana Kwamba Tusiwe Na Viongozi Wa Kanisa?

Hapana, sivyo hata kidogo. Biblia iko wazi kabisa kwamba Mungu huweka viongozi kanisani, (Efe 4:11,12), lakini wajibu wao mkubwa ni kuandaa kanisa lote na kuliachilia kwenye huduma ya ‘ukuhani’ ambayo Mungu alishaiandaa mapema kwa ajili ya kila mwamini (Efe 2:10).

Kuhani Anafanya Kazi Gani Basi?

Kazi yake ni kuonesha utakatifu wa Mungu na Kuhani wake Mkuu, Yesu (1Pet 1:15) (Ebr 7:26; 10:10).

Anafanya maombezi kwa ajili ya watu mbele za Mungu.

Anamwakilisha Mungu mbele ya watu.

Ndiyo, na ingawa hiyo ndiyo kazi ya kiongozi wa kanisa, lakini bado unaweza, na unapaswa kufanya mambo hayo yote kila siku; kuwa kuhani kwa watu palepale walipo.

Je, Tunaweza Kufanya Nini Tena Kama Makuhani?

Tunaweza na tunapaswa kutoa ‘sadaka za kiroho’ (1Pet 2:5).

 

Biblia inazitaja kuwa ni -

Sadaka za sifa kwa Mungu (Ebr 13:15).

Sadaka za fedha na mali nyingine (Flp 4:18) (Ebr 13:16).

Sadaka ya mwili wetu kwa Mungu (Rum 12:1).

Sadaka za kutenda mema (Ebr 13:16) (Mdo 10:38).

Mmishenari mmoja aliyependwa sana na watu alisikitika alipoona watu wachache tu wakiponywa na kufunguliwa alipowaombea. Baadaye alipoomba kuhusiana na jambo hilo, Bwana alimwelekeza kwenye Mdo 10:38 na kusema kwamba kama atafanya sehemu ya kwanza kwanza, kama Yesu alivyofanya- yaani kuzunguka akitenda mema, basi sehemu ya pili inayohusu uponyaji wa watu waliokandamizwa na Shetani itafuata. Hakika hivyo ndivyo ilivyokuwa baada ya mmishenari yule kujitoa kwa ajili ya shughuli ndogondogo za wema, ndipo Bwana alipolitimiza neno lake kwa miujiza.

Kila Mmoja Anaweza Angalau Kutenda Jambo Jema

Yesu alitenda mema mara nyingi sana na Paulo alimwagiza Tito awaambie watu wadumu katika kutenda mema (Tit 3:8,14). Soma pia (Efe  6:8; 2:10; 4:12) (Mt 5:16) (Yak 2:14-26).

Je, Una Imani Katika Yesu?

Soma alichosema Yesu katika Yn 14:12. Yesu alifundisha kwamba cho chote alichokifanya kila mmoja wetu mwenye imani katika yeye, anaweza kukifanya leo kwa jina lake.

Yesu Alifanya Nini?

Yesu alisema kweli na kufanya ~

 

Miujiza 23 ya uponyaji,

Mara tatu alifufua wafu,

Mara mbili aliwapa chakula maelfu ya watu,

Alikemea matukio ya asili,

Alilipa kodi kimiujiza,

Mara mbili aliwezesha kuvuliwa samaki kwa ajili ya kula, kwa ajili ya kuuza na kwa ajili ya akiba,

Aliwapa watu divai kwa ajili ya sherehe.

Kiongozi wa kanisa mwenye busara atajitahidi kuleta baraka nyingi na utoshelevu kwa watu wake kwa kuhakikisha kwamba kila mwanamume na kila mwanamke ameandaliwa kwa mafunzo ili awe kama Yesu; na kisha kuwaachilia ili watende kazi kama ‘wahudumu’ chini ya uangalizi, ama nyumbani au kama wamishenari nchi za mbali. Iwapo atafanya hivyo jeshi lote la Mungu litasonga mbele katika upendo na kuleta ushindi, na mchungaji hatalazimika kufanya kila kitu peke yake.

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Turkmenistan

Jina la Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Baluch, Western

Baluchi, Western

34,000

Tatar

Tatar

41,000

 




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk