1985 - 2007

 

75. Kanisa Lenye Kuubadilisha Ulimwengu

Je, hekalu lako ni nyumba ya maombi au ni pango la wanyang’anyi?

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Mk 11:12-17; Isa 56

Mstari Wa Kukariri
 “…Je, haikuandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala kwa mataifa yote?’ Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi” (Mk 11:17).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Hebu jadilini kwa kitambo kidogo mambo yote yanayoweza  kuwa kikwazo katika kufanya maombezi ya mara kwa mara kwa ajili ya mataifa. Je, kuna mnyang’anyi anayeshambulia maisha yako ya maombi? Wanyang’anyi hao ni akina nani na je, unaweza kuwachukulia hatua gani?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Andaa orodha ya mataifa na watu ambao utajitoa kuwaombea moja baada ya lingine, kwa muda maalumu kila siku. Tazama ramani ya makundi ya watu ambao hawajafikiwa. Je, unaweza kugundua nini kuhusu maeneo haya? Kitabu cha shule cha jiografia kinaweza kukusaidia, au magazeti au taarifa katika Televisheni.

Kazi Ya Stashahada
Chora au nakili kwa mkono ramani ya dunia. Andika au kupigia mistari majina ya nchi mbalimbali kama uwezavyo.

Tafakari Mstari Ufuatao
Habakuki 2:14

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Israeli. Idadi ya watu ni 6,000,000 Wayahudi na Waarabu.

Watu wa Mungu tangu zamani sana. Unabii umetimia kwa kurejea kwao nyumbani. Wako kwenye misukosuko lakini bado wanamtazamia Masihi wao. Ukristo haukubaliki.

 

Je, ulijua kwamba siku moja Yesu alipata hasira ya haki? Ilitokea wakati alipogundua kwamba nyumba ya Mungu inatumiwa kama soko badala ya kama kituo cha baraka kwa mataifa.

Mwaliko Kwa Mataifa Yote

Katika zama za Agano la Kale, Mungu alitaka nyumba yake, yaani hekalu la Yerusalemu, liwe ni mahali ambapo watu kutoka mataifa yote wangeweza kufika na kusali kwa furaha. Watu wake, yaani Wayahudi, watu wa mataifa mengine na hata wale waliokuwa wametengwa kijamii walialikwa.

Wakati Isaya aliposema ‘mataifa yote’, maneno hayo yangeweza kuwashtua Wayahudi kwa sababu wao katika hali ya wivu waliwazuia watu wengine kuingia hekaluni. Lakini moyo wa Mungu ulikuwa mkuu kuliko wao, uliwapenda watu wote wa ulimwengu mzima! (Isa 56:6-8).

Leo hii kanisa lipo katika kila nchi hapa duniani. Ibada kutoka duniani inaelekea kufanana na ile inayofanyika mbinguni ambako watu kutoka kila taifa, kabila na lugha tayari wanamwimbia Yesu mbele ya kiti cha enzi cha Mungu (Ufu 7:9,10).

Kutoka Mataifa Yote Kwenda Mataifa Yote

Yesu alisema kwamba nyumba ya Mungu ni mahali pa kufanyia sala kwa niaba ya mataifa yote. Kwahiyo watu kutoka mataifa mbalimbali bado wanaweza kuingia kwa furaha wakafanya maombi na watu wa mataifa yote wakabarikiwa (Mk 11:17).

 

Ethnos Ndilo Neno Muhimu

Katika lugha ya Biblia neno ethnos lina maana ya mataifa; sio mataifa ya kisiasa bali makundi ya watu wanaounganishwa na lugha au tamaduni. Na hili linatufanya tuelekeze maombi yetu hata kwa kabila dogo kabisa. Katika mataifa yaliyo mengi, kuna mataifa mengi. Hii ina maana kwamba katika taifa moja la kisiasa unaweza kukuta ethnos kadhaa. Kwa mfano nchini Burkina Faso kuna mataifa kama Mossi, Lobi, Gurunsi na Fulani. Hao wote ni ethnos wanaopatikana katika eneo moja la kijiografia na taifa moja la kisiasa lililoundwa na watawala wa kikoloni zaidi ya karne moja iliyopita.

 

Mungu Wangu, Na Mungu Wa Dunia Yote

Mungu ni wangu na ni wako pia lakini usisahau kwamba aliupenda ulimwengu. Kumbuka pia kwamba alimtuma mwana wake kuuokoa ulimwengu wa watu (Yn 3:16,17).

Kristo alikuja ulimwenguni (Yn 1:9).

Shamba ni ulimwengu wenyewe (Mt 13:38).

Je, Kuna Mataifa Katika Biblia?

Ndiyo, yametajwa mara 580, kwahiyo tunajua kwamba Mungu anajihusisha na hayo mataifa. Soma Mwa 12:3; Rum 4:17,18; Gal 3:8.

Mataifa ni uwanja wa mapambano ya kiroho (Efe 6:12). Kazi yetu ni kwenda kufanya wanafunzi katika mataifa yote, basi (Mt 28:19) (Ufu 5:9; 7:9,10). Uinjilisti kwa ulimwengu mzima ni ufunguo wa tarehe ya kurudi kwa Kristo, na ataleta haki kwa mataifa yote (Mt 24:14; 12:18). Mataifa yataendelea kubaki na utambulisho wao, na hatimaye kuna hitaji kubwa la uponyaji (Ufu 22:2; 21:24).

Siku Hizi Hekalu Liko Wapi?

Hatulazimiki tena kwenda Yerusalemu kwa sababu Paulo anatufunulia kwamba leo hekalu la Mungu linapatikana maishani mwetu (1Kor 6:19). Kwahiyo je, maisha yetu ni nyumba ya maombi au ni pango la wanyang’anyi?

 

Na Pango La Wanyang’anyi Ni Nini?

Ni cho chote, au ye yote anayekuibia huruma ya Mungu kwa ulimwengu wa watu.

Katika Yer 7:1-11 unyang’anyi ulikuwa unafanywa na dini na taratibu zake, udhalimu, ibada ya sanamu, na kutowatendea haki wageni na maskini. Yesu aliainisha mnyang’anyi mwingine kuwa ni tabia ya kupenda fedha.

Kupatikana Kwa Imani Ya Kuwaombea Mataifa

Je, tunaamini kwamba maombi yanaweza kufanya lo lote katika mipango ya Mungu kwa mataifa? Hebu na tuone baadhi ya mifano ~

Ibrahimu

Bwana alikuwa karibu na kuharibu kabisa miji miwili miovu lakini Ibrahimu alipogundua jambo hilo alifanya maombezi mara kadhaa ili kwamba watu wa miji hiyo wapate kuokolewa. Na aliona mwitikio wa Bwana kuwa ni mzuri (Mwa 18:17-33).

 

Amosi

Wakati Amosi alipoona kwamba Mungu anataka kuleta hukumu juu ya Israeli, alilia na kuomba akisema, “Ee Bwana Mungu, samehe nakusihi: Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. Bwana akaghairi katika jambo hili” (Amo 7:2-6).

 

Danieli

Danieli alitambua moyoni mwake kwamba ulikuwa ni muda wa kufanya maombi kwa ajili ya taifa, na akaomba. Mungu alijibu maombi haraka (Dan 9:2-23).

 

Na Katika Siku Zetu Pia

Yesu anatazamia sisi tujue ishara na majira (Mt 16:3). Ushindi katika Vita Vya Pili Vya Dunia, na kuporomoka kwa Ukomunisti kumehusishwa na miaka kadhaa ya kujitoa kwa ajili ya maombi; mfululizo wa vita vya kiroho katika kuomba kulikofanywa na Rees Howells, Samuel Howells na wanamaombezi wengine katika Chuo Cha Biblia cha Swansea huko Wales, miongoni mwa wanamaombi wengine wa ulimwengu mzima.

Maombi Yanaziweka Sawa Nyakati Za Mwisho

Katika Ufunuo 5:8 na 8:1-5 Biblia inajulisha kwamba mwisho wa historia ya mwanadamu upo mikononi mwa Bwana Yesu Kristo. Halafu tunagundua kwamba matukio ya siku za mwisho na maombi ya watu wa Mungu vimeunganishwa pamoja. Kuna ukimya mbinguni kwa ajili ya maombi ya watu wa Mungu, na kisha, muhuri wa saba wa kuogofya wa hukumu unafunguliwa.

Inasemekana kwamba historia iko mikononi mwa wanamaombi. Katika jina la Yesu tunayo mamlaka juu ya Shetani, kuzuia na kuharibu mipango yake, kubomoa ngome zake na kuwaweka huru mateka wake. Maombi yetu huubadilisha ulimwengu wetu, hufungua milango iliyofungwa, huwafanya watu wabishi wakubali kumpokea Yesu, huangusha na kuinua viongozi.

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Ukraine

Jina la Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Azerbaijani

Azerbaijani, North

34,000

Jat (Jati, Jatu)

Jataki

32,000

 




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk