1985 - 2007

 

80. Ufalme Wa Waliobarikiwa

Katiba ya Ufalme wenyewe ni mfululizo wa misimamo na wala si sheria

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index
 

Katika Biblia Yako Soma
Mt 5

Mstari wa Kukariri
Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu (Mt 5:11,12).

Baadaye Zungumzieni Jambo Hili
Je, unajisikiaje unapogundua kwamba watu wanatibuka kwa sababu wewe unamfuata Yesu na kwenda kanisani? Je, ukionesha misimamo ya ufalme unadhani watakuchukulia tofauti?

Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena
Mwombe Mungu akupe fursa ya kuonesha misimamo ya ufalme na kuichukua inapojitokeza. Uwe tayari kutoa ushuhuda mtakapokutana tena.

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada
Chora picha ya mlima kutoka ardhini kwenda juu, na uoneshe hatua mbalimbali za kuukwea hadi kufika kileleni. Onesha pia muhtasari wa maandiko.

Tafakari Mstari Huu Neno Kwa Neno
2Tim 3:12

Tumia Muda Mfupi Kuubadilisha Ulimwengu

Ombea taifa la Sri Lanka. Idadi ya watu ni 18,000,000 Wasinha na Watamili.

Asilimia 70% ni Mabudha, asilimia 7% ni Wakristo, na asilimia 0.45% ni Wainjili. Kumekuweko na vita vya wenyewe kwa wenyewe na mateso ya muda mrefu

 

Kwa mujibu wa Biblia yenye maelezo ya ziada, the Amplified Bible, kubarikiwa kuna maana ya, “kuwa na furaha, kuhusudiwa, kuwa na mafanikio ya kiroho, kuwa na uzima, fadhila za furaha na utoshelevu kutoka kwa Mungu na wokovu, bila kujali hali ya mwonekano wa nje.” Moja ya masomo ya awali sana ambayo Yesu aliwafundisha makutano ni namna ya kubarikiwa. Wengi wao walikuwa ni watu maskini, na wafanyakazi katika taifa lililokandamizwa kwahiyo akawafundisha jinsi ya kubarikiwa bila kujali mazingira ya nje (Mt 5:3-10) (Mt 5:1-7:29).

1. Kuwa Mwenye Heri Ni Kuwa Kwenye Msimamo

Yesu alitufundisha namna ya kujongelea maisha na jinsi ya kuishi katika msimamo utakaopelekea baraka. Hiyo ndiyo misimamo yake na inapasa kuwa misimamo yetu pia (Flp 2:5).

Kukwea Mlima Katika Ufalme
Zile heri ni ngazi nane za kuelekea juu kwenye kilele cha maisha ya baraka.

  1. Uwe mnyenyekevu, na kumhitaji Mungu kila mara (Mt 5:3).
  2. Uoneshe majuto, na maombolezo kwa dhambi zako na za watu wengine (Mt 5:4).
  3. Uwe mpole, ule utulivu wa nafsi iliyopumzika katika Mungu (Mt 5:5).
  4. Uwe na njaa, hamu ya chakula cha kiroho, uoneshe jinsi unavyokua    (Mt 5:6).
  5. Uwe mwenye huruma, kama Mungu mwenyewe, na kuonesha jambo la ziada (Mt 5:7).
  6. Uwe msafi wa moyo, ndiko mahali pa juu unakoweza kumwona Mungu (Mt 5:8).
  7. Uwe mpatanishi, upate kutuliza dhoruba katika maisha ya watu wengine (Mt 5:9).
  8. Uwe tayari kuteseka, kilele cha Manabii na Wafiadini (Mt 5:10-12).

2. Kuwa Maskini Katika Roho Ni Kubarikiwa

Ufalme wa mbinguni ni wao; lakini ni akina nani hao? Maskini ni ptochos lenye maana ya mtu wa hali ya chini, anayeteseka na asiyekuwa na mali, mvuto wala ushawishi, asiye na nafasi wala heshima, asiyekuwa na wema wala utajiri wa kudumu; mtu asiye na msaada wala uwezo, ombaomba asiye na elimu na aliye tegemezi kwa watu wengine (Mt 5:3). Kuwa maskini katika roho ni kujua kwamba hatuna uwezo na rasilmali za kwetu wenyewe na kwamba sisi tuna uhitaji mkubwa wa vitu vyote; na Mungu pekee anakuwa ndiye chanzo pekee cha mahitaji yake. Ni kupoteza ile hali ya kujitegemea na badala yake kuwa tegemezi kwa Mungu, na kutegemeana kila mmoja na mwenzake. Yesu alitenda yale tu aliyomwona Baba yake akitenda. Huo ndio uliokuwa umaskini wa kweli wa kiroho (Yn 5:19).

3. Kuwa Na Huzuni Ni Kubarikiwa

Watafarijiwa, lakini maana yake nini kuomboleza? (Mt 5:4). Yesu alihakikisha kwamba watu wanaelewa, kwahiyo akatumia neno lilelile ambalo tungelitumia penye msiba. Katika tamaduni nyingi kuomboleza kuna maana ya kutoa machozi, kulia kwa huzuni, kugumia, kupiga kite, kufunga kula, kujiinamia, kutembea peku na kichwa wazi. Lakini Yesu alikuwa hamaanishi huzuni inayotokana na kifo cha kimwili, bali alikuwa na maana ya msimamo wa huzuni kwa ajili ya dhambi ya mtu binafsi na ya taifa inayoleta mauti. Yesu alikuwa mtu wa huzuni, ingawa alipakwa mafuta ya furaha zaidi ya washirika wake (Isa 53:3) (Ezr 10:6) (Neh 1:3) (Yak 4:9,10).

4. Kuwa Mpole Ni Kubarikiwa

Wapole watairithi nchi, lakini ina maana gani kuwa mpole? (Mt 5:5). Neno la Kigriki cha kileo lenye maana ya ‘upole’ ni prautes. Neno hili linaelezea farasi kijana anapofundishwa na kudhibitiwa kwa ajili ya huduma. Yupo mtu anayemdhibiti na kujenga uhusiano naye, na kisha farasi ananyenyekea na kutii mamlaka na kumtumikia bwana wake, akavaa hatamu kwa ajili ya uelekeo. Upole hauzai udhaifu bali nguvu zilizodhibitiwa na kutumika vizuri. Halikadhalika mtu mpole ni yule anayechagua kuacha haki zake na matakwa yake binafsi, na kuzitumia nguvu zake kwa ajili ya Mungu na watu wengine.

5. Kuwa Na Njaa Ni Kubarikiwa!

Ikiwa una njaa na kiu ya haki, utashibishwa (Mt5:6) (Zab 42:1,2). Chakula na kinywaji ni mahitaji halisi ya mwili na bila hivyo mtu anaweza akafa. Hata hivyo tunapaswa kuwa na njaa kubwa na kiu kubwa ya Mungu, tukiutafuta kwanza ufalme wake na haki yake. Yesu alisema chakula chake ni kufanya mapenzi ya Mungu na kuimaliza kazi yake. Kwahiyo tunapaswa kwa kweli kuwa na njaa na kiu ya haki ambayo ni katiba ya kudumu ya Ufalme wa Mungu (Mt 5-7) (Mt 6:33) (Yn 4:34) (Mk 8:8).

6. Kuwa Mwenye Rehema Ni Kubarikiwa

Je, unataka kuhurumiwa? Mungu ni mwingi wa rehema, na kwa kadiri tunavyopokea rehema kutoka kwake ndivyo tunavyoweza kuwahurumia wengine, na hivyo kubarikiwa na Baba yetu mwenye rehema (Mt 5:7) (Efe 2:4) (Lk 6:36). Kuonesha rehema sio tu kumsikitikia mtu na kumwacha aende zake, bali ni tendo la kumhurumia, kumsamehe na kumpa msaada anaouhitaji.

7. Usafi Wa Moyo Huleta Baraka

Kuwa msafi wa moyo kuna maana ya kutokuwa na nia mbili, agenda za siri au viwango tofauti. Neno katharos lina maana ya metali safi isiyo na mchanganyiko; mvinyo usiochanganywa; jeshi lisilokuwa na watu waoga na wapinzani. Watu wenye mioyo safi wanamjua Mungu na makusudi yake kwa sababu nia zao ni safi (Mt 5:8) (Yak 4:8) (Zab 86:11) (Mit 4:23).

8. Uwe Mpatanishi Ili Ubarikiwe

Haitoshi tu kuwa mkimya lakini inapasa kufuatilia kwa dhati na kuhusika katika kutatua tatizo na kuleta ufumbuzi wa kuridhisha (Zab 34:14). Neno lililotafsiriwa amani ni eirene au shalom, yenye maana ya upatanifu, ustawi, na fadhila za Mungu. Ni wana wa Mungu pekee wenye uwezo wa kuleta amani (Mt 5:9).

9. Kuteswa Pia Ni Baraka!

Mateso ni matokeo ya mapambano kati ya Ufalme wa Mungu na ule wa Shetani ambapo falme hizi hupingana katika masuala ya kiroho, uadilifu, maadili,  katika imani na tabia. Watu wa kweli wa Ufalme huhisi joto la mapambano katika ubaguzi, matusi, mateso na katika uovu shutuma za kila namna. Yesu alisema kwamba hayo yatatokea lakini akataka tufurahi kwa sababu hayo pia yaliwapata manabii. Akasema pia kwamba thawabu yetu mbinguni ni kubwa (Mt 5:10,11) (2Tim 3:12) (Yn 15:20) (1Pet 4:13,14).

 

Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Ambao Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina

Uzbekistan

Jina la Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Persian (Irani)

Farsi, Western

26,000

Uzbek, Southern (Afghan Uzbek)

Uzbek, Southern

15,000

 




 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index to All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index

www.dci.org.uk